Zitauzwa kwa wananchi wa kawaida, Waziri Tibaijuka aimwagia sifa NHC Watanzania wasio na viwanja sasa hawana sababu ya kuendelea kuhangaikia changamoto hiyo kwa vile Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kujenga nyumba za kuishi kwa ajili ya kuwauzia kwa bei nafuu.

Wiki iliyopita, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa 48 zenye thamani ya Sh bilioni nne, zinazojengwa na NHC eneo la Mchikichini, Ilala jijini Dar es Salaam. Kama ilivyo dhima ya kuanzishwa kwake, NHC imelenga nyumba hizo ziwanufaishe wananchi wenye kipato cha chini na cha kati.


Ujenzi wa nyumba hizo ulianza Agosti, mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Februari, mwakani. Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu, anasema walengwa wakuu kwenye ujenzi huo ni wananchi wenye kipato cha chini na cha kati. Kila nyumba ina vyumba vitatu vya kulala, sebule, jiko, stoo, msalani na maliwato.

 

“Uzinduzi wa mradi huu ni mwanzo wa uzinduzi wa miradi mingine mingi ya ujenzi wa nyumba zitakazouzwa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema Mchechu.

NHC imejipanga kuzindua miradi mingine ya aina hiyo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, yakiwamo ya Upanga, Ubungo, Chang’ombe na Kurasini. Mbali ya Dar es Salaam, NHC imejipanga kutekeleza mpango huo katika mikoa 14 nchini.


“Mpango wa ujenzi wa nyumba kwa ajili ya kuziuza kwa wananchi kwa bei nafuu ni agizo la Serikali, sisi NHC tumelipokea na tunalitekeleza kwa ukamilifu,” amesema Mchechu na kuongeza:


“Nyumba tunazojenga kwa ajili ya kundi la watu wenye uwezo wa chini jijini Dar es Salaam zitauzwa Sh milioni 35 hadi Sh milioni 40, lakini kwa upande wa mikoani (nje ya Mkoa wa Dar es Salaam) bei inapaswa kuwa chini ya kiwango hicho.”


Tayari Serikali imeielekeza NHC kutoa kipaumbele cha uuzaji nyumba hizo kwa wananchi wenye kipato cha chini, ikiwa ni jitihada za kupunguza tabaka la umikaji nyumba za kuishi kati ya wenye kipato cha juu na cha chini.


Kodi kwenye vifaa vya ujenzi imekuwa kilio, si tu wananchi wanaojenga, bali hata NHC. Kwa sababu hiyo, Serikali imeahidi kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi kwa vifaa vya ujenzi ili kuiwezesha NHC kutekeleza maagizo ya ujenzi wa makazi ya gharama nafuu na hivyo kuwawezesha wananchi wa kawaida wengi kumudu kuzinunua.


Profesa Tibaijuka ambaye alipata kutumikia Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifda (UN Habitat), ameipongeza NHC kwa mwitikio wa ujenzi wa nyumba hizo, akisema kitendo hicho kimemuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, aliyetoa kipaumbele kwa kuanzisha NHC.


“Hapa tunatekeleza Ilani ya CCM iliyowapa (NHC) changamoto ya kujenga nyumba 15,000 itakapofika mwaka 2015,” amesema Profesa Tibaijuka na kuendelea: “Nasikia mtajenga pia kule Kigamboni, kipaumbele cha kuuza nyumba kitolewe kwa waliokubali kupisha ujenzi wa nyumba za NHC, kwa sababu wangegoma tungeibuka na mgogoro.

 

“Kwa hiyo, hawa wakazi wa Mchikichini (waliopisha ujenzi) wameonesha mfano wa kuigwa. Mkurugenzi Mkuu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC muwawezeshe kupata nyumba. “Haitapendeza kuwaondoa na kuwapa wengine wakati wao walikubali kuondoka. Wapewe kipaumbele wenye uwezo wa kurudi hapa Mchikichini au maeneo mengine zinapojengwa nyumba za NHC.

 

“Ninasikia mnakwenda kujenga nyumba kule Oysterbay, kule lazima watu wa kipato cha juu, lakini hapa Mchikichini au Kigamboni, Magomeni, Morogoro na kadhalika, naomba kipaumbele kiwe kwa wenye kipato cha chini na kipato cha kati. Jamani hilo ni agizo naomba lifuatwe.”


Waziri huyo amewaomba Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali na NHC katika ujenzi wa nyumba hizo, akisema utaratibu huo unatekelezwa sehemu nyingi duniani, hata katika nchi zilizoendelea.


“Ndugu zangu, duniani kote, hata Marekani ambako wana vipato vya juu, hata China, hata uende Ulaya, hakuna mtu mwenye uwezo wa kuwa na fedha zote taslimu kupata nyumba, ukitaka kuendesha sekta ya nyumba, kwanza uendeleze mfumo wake wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kama hizi.


“Shirika letu la Nyumba linaenda vizuri kuhakikisha nyumba zinajengwa, lakini sisi kwa upande wa Wizara hatukulala, sheria zote zinazowezesha wananchi kupata mkopo wa nyumba kwa bei nafuu zimekwisha kukamilishwa.


“Rai yangu kwa mwananchi wa Mchikichini, Ilala, Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla, na wewe sasa fanya hima, anza kuweka akiba uweze kupata angalau kianzio, kinachohitajika,” amesema Profesa Tibaijuka.


Ameongeza, “Sasa nishauri kwa ninyi Watanzania, hasa vijana, nitoe wito kwa vijana, pamoja na kwamba ni muhimu tuwape viwanja, lakini ondokaneni na kasumba ya viwanja, tafuteni nyumba mchukue mkopo muanze kulipa polepole, ukiweza kupata down payment (kianzio) cha milioni Sh 16 unaingia hapa na hizi nyumba ni za kudumu.


“Mathalani, nyumba ya kipato cha chini na cha kati ni Sh milioni 30 au 40, kama ni Sh milioni 35 wewe unachokihitaji ni down payment (kianzio) Sh milioni 3.5 tu, hela nyingine yote inatoka benki, kwa hivyo unalipa polepole.


“Mwisho wa siku baada ya miaka mitatu unajikuta una nyumba nzuri ya kuishi. Lakini kusudi miradi yetu iwe shirikishi, ifanikiwe na iwe endelevu, sharti tuchukue nyumba zinazolingana na uwezo wetu (wa kipato).


“Kwa hiyo, nisingependa migogoro mingine kati ya NHC, nyumba zinakuja kunadiwa na benki. Hili nalo lazima tulizungumzie katika kutoa elimu kwa umma kwa sababu unapochukua mkopo benki usipolipa sheria zetu hivi sasa za kutafuta injunction (pingamizi) hakuna tena, benki inakuja na dalali, mnada (unapigwa) nyumba inakwenda, na wanapoinadisha hawakurudishii hela ambazo ulikuwa umelipa. Hilo nalo lieleweke.


“Lazima niendelee kuwapongeza NHC kwa kazi nzuri, ni kazi ngumu na kwa sababu mnachukua hela za benki, pia nieleze kwamba sisi uwezo wa Serikali kujenga nyumba za wananchi bure au kutoa ruzuku kwa NHC bado hatuna uwezo huo.


“NHC iko katika hali ngumu ambayo mimi ninaijua, kwamba mnatumia hela za benki kujenga nyumba hizi, wengi wanahoji na wengi wamenipigia simu kuuliza nyumba za NHC. Mimi ninakazana kuangalia angalau kama tunaweza tukapunguza kodi kwa vifaa vya ujenzi.

“Nashukuru kunialika kusimika nyumba za Mchikichini na kuwatakia wakazi wa Mchikichini mnaokuja- starehe na raha. Tutapenda pia kuwa na amani, usafi, maana nyumba ni kama mwili, kama hutunzi mwili mambo yanaweza kukwendea kombo.


“Mkurugenzi (Mchechu) naomba uweke bustani hapa, naomba upande miti, tuweke bembea za watoto kucheza na watakaokuwa hapa muwape amani na starehe. Kwa hayo, nawatakia kila la heri na mkandarasi nadhani anafuata viwango vya mkataba.”


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, ameikosoa Serikali akisema haikuitendea haki NHC kwa kuiagiza ijenge nyumba na kuziuza kwa wananchi kwa bei nafuu kabla ya kupunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi.


Hata hivyo, Lembeli ambaye ni Mbunge wa Kahama (CCM), ameahidi kushirikiana na Profesa Tibaijuka kuishawishi Serikali iharakishe uwezekano wa kupunguze kodi hizo ili kuiwezesha NHC kujenga na kuuza nyumba kwa gharama nafuu zaidi.


“NHC ni miongoni mwa mashirika ya umma ambayo Watanzania wanapaswa kujivunia. Ninashauri nyumba za zamani za shirika hili zisiuzwe kwani zimetokana na kodi zilizolipwa na Watanzania. Watu wanunue nyumba mpya zinazojengwa na kipaumbele kitolewe kwa wananchi wenye kipato cha chini,” amesisitiza Lembeli.


Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwamo wananchi wa kawaida walioonesha furaha kwa uamuzi wa NHC na Serikali wa kujenga nyumba kwa ajili ya kuwakopesha watu wenye kipato cha chini na cha kati.

By Jamhuri