Na OWM – TAMISEMI,Mtwara

Mkoa wa Mtwara umeendelea kupiga hatua katika kuboresha Sekta ya Elimu kufuatia utekelezaji wa Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), unaosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, huku ukifadhiliwa na Benki ya Dunia.

Akizungumza wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa pamoja wa utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa Mradi wa SEQUIP kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Bw. Richard Makota, alisema shule za Mkoa wa Mtwara zimeonyesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mradi.

“Matokeo yanaonekana wazi, hasa katika ongezeko la ufaulu wa wanafunzi kwenye masomo ya sayansi na hisabati, pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika ufundishaji,” alisema Bw. Makota.

Alisema kupitia SEQUIP, maboresho makubwa yamefanyika ikiwemo ujenzi wa miundombinu mipya ya shule, upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya TEHAMA kama mbao janja (smart boards) na kompyuta, pamoja na utoaji wa vifaa vya maabara na kemikali kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi, Hatua iliyoongeza ufanisi katika ujifunzaji na ufundishaji, hasa katika masomo ya sayansi na hisabati ambayo yamepewa kipaumbele maalum ndani ya mradi huo.

Alizitaja baadhi ya shule zilizonufaika kuwa ni Shule ya Ufundi Mtwara, Shule Mpya ya Sekondari Mkanaredi, Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara na Shule ya Sekondari Sabasaba, ambayo pia ni kituo cha wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali.

Aidha, alieleza kuwa mradi huo umeweka mkazo katika kuwasaidia wanafunzi waliorejea shuleni (re-entry students) kwa kuwapatia mazingira rafiki ya kuendelea na masomo yao bila vikwazo, hatua inayolenga kuhakikisha kila mwanafunzi anapata haki ya elimu.

Katika hatua nyingine, serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa shule mpya za sekondari ngazi ya kata, ikiwemo shule ya bweni ya wasichana katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu na shule ya sekondari ya amali katika Halmashauri ya Mji wa Masasi.