Msanii wa Nigeria kutangaza utalii

Dar e Salaam

Na Mwandishi Wetu

Msanii nyota wa filamu wa Nigeria, James Ikechukwu Esomugha, maarufu kama ‘Jim Iyke’ anatarajiwa kuwasili nchini baadaye mwezi huu kwa ziara maalumu ya kikazi.

Iyke, anayetamba na filamu yake mpya iitwayo ‘Bad Comments’, akiwa nchini atatembelea Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) na kushiriki uzinduzi wa tamasha la Wamasai linalofahamika kwa Kiingereza kama ‘Maasai Festival’.

“Atawasili nchini Januari 27, mwaka huu. Iyke atafanya utalii nchini wakati huo huo akiangalia fursa za kibiashara zilizopo Tanzania,” anasema Ofisa Mtendaji Mkuu wa SMR Group, Said Rukemo, katika mazungumzo na JAMHURI. 

Anasema Bodi ya Utalii nchini (TTB) inashirikiana na SMR Group, kampuni ya burudani, masoko na matukio, kufanikisha ujio wa msanii huyo na kutoa fursa kwa wasanii wa Bongo Movie kufanya naye kazi; huku safari yake ya Ngorongoro ikidhaminiwa na Kampuni ya Wonderland Africa.

Iyke anayeng’ara na kutikisa katika tasnia ya filamu Afrika, ni mmoja wa nyota walioigiza kwa umahiri mkubwa filamu maarufu ya ‘Last Flight to Abuja’ akiwa na kina Omotola Jalade Ekeinde na Hakeem Kae-Kazim.  

“Filamu yake mpya, Bad Comments, kwa sasa ndiyo bora na kubwa zaidi nchini Nigeria, ikiigizwa kisasa kabisa. Iyke anataka kutengeneza Bad Comments Part II na akiwa nchini ataangalia namna ya kuwashirikisha wasanii wa Tanzania katika sehemu hiyo ya pili,” anasema Rukemo.

Kwa sasa filamu hiyo bado inaonyeshwa kwenye majumba ya sinema nchini kwao kabla ya kuachiwa rasmi kwenye video na runinga kwa ajili ya mashabiki wa filamu kote duniani.

Mbali na hayo, msanii huyo atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa serikali kwa nia ya kufanya uwekezaji wa kibiashara nchini na Rukemo anasema: “Itakuwa ni ziara ya kitalii, kikazi na kibiashara.”

Baada ya kutoka Ngorongoro, kwa mujibu wa TTB na SMR Group, Iyke atarejea jijini Arusha na kushiriki uzinduzi wa ‘Maasai Festival’; tamasha kubwa la kitamaduni la aina yake kuwahi kufanyika.

Tamasha hilo litakafanyika katika Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha. 

Kuhusu sababu zilizomfanya Iyke kukubali mwaliko wa kutembelea Tanzania, Rukemo anasema hilo limewezekana kutokana na uamuzi wa SMR Group pamoja na TTB kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kimataifa utalii wa Tanzania.

“Mimi nilimhamasisha kuja na yeye alipomwona Mama Samia katika ile Royal Tour alihamasika na ndiyo maana sasa anakuja,” anasema.

Anamnukuu Iyke akisema: “Lengo kuu la kuja Tanzania ni kutalii na kuifahamu Tanzania ilivyo na kwa kuwa ninafahamu kuwa tasnia ya filamu Tanzania kwa sasa imekua, basi ninaamini nitapata nafasi ya kufanya kazi na Watanzania.”

Msanii huyu ni nani?

James Ikechukwu Esomugha, anayefahamika zaidi kama Jim Iyke, ni muigizaji mkubwa wa ‘Nollywood’; yaani filamu za Kinigeria zilizojizolea umaarufu barani Afrika.

Msanii huyu alizaliwa Septemba 25, 1976 huko Libreville nchini Gabon kwa Bwana na Bibi Stephen Okolue.

Ubini wa baba yake ambaye anatoka katika Kijiji cha Ogwugwu huko Enugu Agidi, Jimbo la Anambra, alibadilika na kuwa Esomugha. 

Jim ndiye mtoto wa kiume pekee katika familia ya watoto wanane. Kuanzia mwaka 1985 hadi 1991 alisoma katika Shule ya F. G. C. Kwali jijini Abuja, kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Jos.

Akiwa chuoni hapo, msanii huyo atakayekuwapo nchini kwa takriban siku tano, alihitimu na kutunukiwa diploma katika masuala ya Fedha na Benki, kisha kuchukua shahada ya sayansi katika falsafa.

Jim Iyke aliingia katika uigizaji mwaka 2001, na sasa ni miongoni mwa waigizaji wa Nollywood anayelipwa kiasi kikubwa sana cha fedha akishiriki katika filamu zaidi ya 150. 

Mwaka 2007 alianzisha kampuni yake inayojulikana kama ‘Untamed Productions’ pamoja na ‘lebo’ yake ya muziki, ‘Untamed Records’.