Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa akiteta na Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani, Bernard Membe walipokutana leo katika msiba wa mama mzazi wa Askofu Josephat Gwajima nyumbani kwake Salasala, Dar es Salaam.

Kutoka kushoto ni  Mbunge wa Vunjo, James Mbatia;  Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema,  Bernard Membe  na Lowassa wakiwa kwenye msiba huo.

 

WAZIRI Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa wamekutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani, Bernard Membe leo katika msiba wa mama mzazi wa Askofu Josephat Gwajima nyumbani kwake Salasala jijini Dar es Salaam.

 

Lowassa na Membe ni miongoni mwa viongozi waliochukua fomu kusaka ridhaa ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa 2015, ambapo jina la Lowassa lilienguliwa huku Membe akiingia hatua ya tano licha ya kushindwa katika hatua ya tatu bora.

 

Baada ya jina lake kuenguliwa Lowassa aliamua kutimkia Chadema ambako alipata ridhaa ya kukiwakilisha chama hicho katika ucghaguzi huo mkuu lakini alishindwa na Dkt John Magufuli ambaye alinyakua kiti hicho cha urais.

Kwa upande wa Membe, yeye alipotea kidogo katika anga za siasa ambapo hata hivyo ameanza kuonekana mwaka huu kwenye uchaguzi Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi uliofanyika hivi karibuni makao makuu ya CCM, Dodoma.

 

Mama mzazi wa Askofu Gwajima aitwaye Bi. Ruth Basondole Gwajima, alifariki  Jumapili iliyopita,  Januari 21, akiwa na umri wa miaka 84. Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika leo Alhamisi ya Januari 25, Salasala jijini Dar es Salaama.

By Jamhuri