Na Alex Kazenga, JamhuriMedia, Morogoro

Urahisi wa kuwaona tembo, simba, twiga na chui katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kimekuwa kichocheo kwa watalii wa nje kuitembelea wengi wakitokea Zanzibar, Jamhuri limeelezwa.

Kamanda wa hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Augustine Masesa akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni ofisini kwake amesema kwa kipindi kirefu watalii wa ndani ndio waliokuwa wakishikilia rekodi kuitembelea lakini kasi ya watalii wa nje wanaofika Zanzibar na baadaye kuja Mikumi inaongezeka kila siku.

“Maeneo yanayotupatia watalii kwa wingi ni Dar es Salaam na Zanzibar. Wapo wanaokuja kwa njia ya anga na wengine kwa usafiri wa magari.

“Katika hifadhi yetu ni rahisi kuwaona ‘big 4’ ndani ya muda mfupi, kuna uwezekano ukija ndani ya saa mbili ukawa tayari umewaona wote,” amesema Masesa huku akitoa wito kwa Watanzania kuutumia msimu wa siku kuu ikiwamo pasaka kutembelea hifadhi hiyo kujionea vivutio.

Hifadhi ya Mikumi yenye jumla ya kilometa za mraba 3230 ni ya tisa kwa ukubwa kati ya hifadhi 21 zilizopo nchini na sasa ipo kwenye mkakati wa kuhakikisha watalii wa ndani na nje ya nchi wanaongezeka na kuifanya serikali inayafikia malengo yake ya kuwa na watalii milioni tano kwa mwaka.


Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi Mkuu, Kitengo cha Utalii katika hifadhi hiyo, Herman Mtei, amesema kwa mwaka wa fedha 2023 /2024 wanafanya vizuri ambapo tangu Julai 24 mwaka jana hadi Februali 19 mwaka huu wamepokea watalii 92,000.

“Malengo yetu kwa mwaka huu hadi kufikia Julai tuwe tumefikia idadi ya watalii 123,000, naona tunaenda vizuri. Kile kipindi cha mlipuko wa ugonjwa covid- 19 hatukuwa na wageni kabisa tulikuwa tunapokea ndege inayoleta wageni kutalii lakini sasa hali ni tofauti tunapokea ndege kuanzia tano kwa siku,” amesema Mtei.

Ali Said ambaye ni msaidizi wa rubani wa ndege ya kampuni ya Unity Air Zanzibar amethibitisha hilo muda mfupi baada ya ndege yao kutua na kushusha abiria zaidi ya 30 katika uwanja wa Kikoboga ulipo hifadhini Mikumi akiisifia serikali kwa kuutangaza utalii ndani na nje ya nchi.

“Wageni wengi wanaoitembelea Zanzibar wakitaka kutembelea bara kujionea vivutio, waongozaji huwaelekeza kuja Mikumi, sababu kubwa inayochochea waongoza watalii kuichagua Mikumi ni urahisi na uharaka wa kuwaona wanyama kwa muda mfupi.

“Pia, wenye kampuni za ndege nao hupendelea kuleta wageni wao hapa na kwenye hifadhi ya Nyerere kwa sababu zipo karibu mno na visiwa vya Zanzibar,” amesema Said.

Kwa usafiri wa anga, amesema ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 120 hutumia dakika 40 kuruka kutoka Zanzibar hadi hifadhini Mikumi huku ndege hiyo hiyo ikitumia dakika 120 kuruka kutoka Zanzibar hadi hifadhini Serengeti.

Kwa ndege ndogo yenye uwezo wa kubeba abiria 14 amesema marubani wanatumia dakika 50 hadi 60 kusafirisha watalii kutoka Zanzibar hadi hifadhini Mikumi.

“Tunaowaleta kutokea Zanzibar wakifika maeneo haya ya mbuga wanachanganyikiwa kabisa, wanatamani ndege isimame angani pale pale wao washuke kabisa.
“Wakishuhudia vivutio vilivyopo hifadhini kipindi wakirejea kwao huwashawishi wenzao nao waje kuitembelea Mikumi,” amesema Said.

Kwa upande wake Mwongoza watalii, Said Michael akithibitisha kinachosemwa na Said amesema kinachoifanya hifadhi ya Mikumi kuwa kivutio cha kipekee kwa wageni wa nje ni eneo lake kuwa na ukubwa wa wastani unaosababisha wanyama wote kuonekana kwa urahisi wakiwa kwenye makundi yao.

Anaitofautisha Mikumi na hifadhi nyingine zilizopo akidai mgeni akiwa mbugani ni rahisi kuwaona simba na chui, japo anakiri pia kuwa muda mwingine uonekanaji wa chui katika mbuga hiyo huwa unasumbua.


“Anasumbua kumuona nyakati za mchana, mara nyingi huwa anajificha, lakini kwa wageni ambao wamekuja na bahati huwa anaonekana tu bila kushinda mbugani wakimvizia katika vichaka vyake,” amesema Michael.
Naye, Afisa Uhifadhi daraja la Pili, katika hifadhi ya Mikumi, Fatuma Mcharazo amesema kutokana na kasi ya kuongezeka kwa wageni siku hadi siku wanampango wa kuongeza njia za kutalii hifadhini.

“Kwa wanaotumia usafiri wa magari tunataka kufungua lango la Doma na lango la Kikwalaza ili wawe wanaifikia hifadhi bila kutumia barabara ya lami, tunataka wakifika kijiji cha Doma au Kikwalaza wawe wanaingia kwenye lango tutakalo watengenezea wapite hifadhini mpaka zilipo ofisi zetu,” amesema Fatuma.

By Jamhuri