Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam imeeleza kuwa ina upungufu wa damu kwa asilimia 60 kutokana na kiwango kidogo cha upatikanaji wa damu ikilinganishwa na uhitaji wa damu kwa siku.
Ilisema wastani wa upatikanaji wa damu kwa siku ni chupa 30 lakini mahitaji ya damu kwa siku ni kuanzia chupa 150 hadi 180.
Ofisa Uhamasishaji wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama wa hospitali ya Muhimbili, Richard Masamu alisema hayo jana wakati wa uchangiaji wa damu katika Benki ya KCB, Dar es Salaam.
Alisema upungufu huo unatokana na jamii kutojitoa kikamilifu kushiriki katika uchangiaji wa damu.
Kufuatia hali hiyo Masamu alitoa wito kwa jamii, taasisi na vikundi mbili kujitokeza kuchangia damu kwa ajili ya kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu kwa dharura wakiwemo wajawazito, wagonjwa wa upasuaji, watoto na majeruhi wa ajali.
Kwa upande wake, mfanyakazi wa KCB, Joshua Sanga alisema uchangiaji damu ni muhimu kwa jamii kwa sababu kila siku kwenye jamii wagonjwa wanaohitaji damu wanazidi kuongezeka.
Alitoa wito kwa wananchi kuhamasika kuchangia damu kwa kuwa kitendo hicho hakina madhara yoyote na ipo siku ndugu na jamaa watakuwa na uhitaji wa kuchangiwa damu.
Naye Mhasibu wa Benki hiyo, Vanessa Ngowi alisema kuchangia damu ni jambo nzuri kwa jamii na kinaonesha upendo kwa jamii zetu.
Alitoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kufika katika hospitali kwenye kitengo cha damu salama kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine hususani wanawake wenzao ambao wanapoteza damu wakati wa kujifungua au katika matukio mengine yanayosababisha wapungukiwe na damu.

Kwa upande wake, mfanyakazi wa Benki ya KCB, Ally Hamis alitoa wito kwa jamii kuondoa hofu kuhusu utoaji wa damu kwani uchangiaji damu hauna changamoto yoyote. Kuchangia damu ni kuokoa maisha ya watu wengine wenye uhitaji wa damu.
Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Rasilimaliwatu Benki ya KCB, Monde Lushako alisema benki hiyo imekuwa na programu tofauti tofauti ikiwemo kupanda miti, kukuza vipaji na kujali afya kwa wafanyakazi na jamii.
Alisema pia kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wameendesha uchangiaji damu ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji.
Alisema wameamua kufanya hivyo katika ofisi zao ili kuwapa nafasi wateja na wafanyakazi wa benki hiyo kushiriki kuchangia damu.
“Wote tunafahamu kuwa damu ni muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha ya ndugu zetu wenye uhitaji na sisi tukiwa sehemu ya jamii tumeona ni vyema kuunga mkono ili kuwezesha lengo la hospitali zetu kuwa na akiba ya damu ya kutosha,” alisema Lushako.