Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (TSNP) na mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Abdul Nondo ambaye alikuwa ameripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, usiku wa kuamkia jana aliripotiwa kupatikana mkoani Iringa.

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Juma Bwire amethibitisha kupatikana kwa Nondo. Nondo alikwenda kituo cha polisi Mafinga baadaye kudaiwa kuzinduka kutoka usingizi akiwa hajui alipo, ndipo akauliza wenyeji wa eneo hilo.

Nondo amefunguliwa jalada la uchunguzi mkoani Iringa ambapo kwa sasa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mkoa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alisema kuwa, uchunguzi wanaoufanya unalenga kubaini ukweli wa tukio hilo, ili hatua za kisheria dhidi ya wahusika ziweze kuchukuliwa.

Hata hivyo Kamanda Bwire alisema kuwa, endapo watabaini kuwa mwanafunzi huyo alitoa taarifa za uongo kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kufanya vurugu, atashughulikiwa kama wahalifu wengine.

“Kama kweli alitekwa, sisi polisi tunaahidi tutawapata watuhumiwa na sheria itachukua mkondo wake.”

Kamanda aliongeza kuwa, “Tunaendelea na uchunguzi, kama alitoa taarifa za uongo, kwa lengo la kutaka kuhamasisha wanafunzi wenzake ili kuleta uvunjifu wa amani nchini, tutamshughulikia kama mwalifu mwingine.”

Katika upelelezi, Kamanda Bwire amesema kuwa watafuatilia maeneo yote ambayo amepita, na hivyo amewasihi wananchi wenye taarifa yoyote kuhusu tukio hilo kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda Bwire alizuia Nondo aliyekuwapo mkutanoni hapo asiulizwe maswali kutokana na uchunguzi unaoendelea dhidi yake.

Baada ya mkutano huo, Nondo alirejeshwa katika Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Please follow and like us:
Pin Share