*Kisa kakataa kutoa rushwa

 kwa maofisa wa PSRC

Dar es Salaam

Na Dennis Luambano

Kundi la kampuni za Wellworth Hotels and Lodges Limited limenyimwa hatimiliki na ‘share certificates’ za Hoteli ya Kunduchi Beach and Resort pamoja na nyumba za wafanyakazi tangu mwaka 1997 walipozinunua kutoka kwa iliyokuwa Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kwa bei ya dola 1,100,000 za Marekani.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Wellworth, Zulfikar Ismail, amesema kupitia kundi la kampuni hizo zinazomiliki pia hoteli zaidi ya 10 hapa nchini ikiwamo Zanzibar Beach Resort na Oldeani Ngorongoro Mountain Lodge waliinunua Hoteli ya Kunduchi Beach kwa bei hiyo kupitia Kampuni yao nyingine ya AC Gomes (1997) Ltd.

Mwekezaji huyo wa ndani amesema licha ya kununua kutoka kwa PSRC na kufuata taratibu zote za kisheria na masharti ya uwekezaji, ikiwamo kulipa asilimia 50 ya bei ya ununuzi na kufanya ukarabati mkubwa wa hoteli hiyo lakini walinyimwa hatimiliki na ‘share certificates’.

Amesema baada ya hatua ya kulipa asilimia 50 kukamilika lakini hawakukabidhiwa hatimiliki na ‘share certificates’ ndipo mwaka 2000 wakaingia katika makubaliano mapya huku PSRC wakiwa bado wanawadai dola 550,000 za Marekani na baadaye wakakubali kupunguza dola 450,000 za Marekani katika deni hilo kama fidia kwao baada ya kukiuka makubaliano ya mkataba na likabaki deni la dola 100,000 za Marekani.

 “Tunasikitika kwamba tangu kipindi hicho tulipoinunua hoteli hiyo zaidi ya miaka 25 iliyopita hadi sasa hatujafanikiwa kupata hatimiliki na share certificates kutoka serikalini licha ya sisi kutimiza masharti yote ya ununuzi kama ilivyotakiwa.

“Jambo hili kisheria linatunyima umiliki wake kwa sababu hatujakabidhiwa Kampuni ya Kunduchi Beach Hotel Limited licha ya kulipa asilimia 50 ya bei ya ununuzi kama taratibu zilivyotaka kwa kuwa hatukupewa hatimiliki na share certificates.

“Pamoja na kwamba tumefanya juhudi kubwa za ufuatiliaji ikiwamo kuandika barua nyingi katika mamlaka mbalimbali serikalini na hata kufanya vikao vingi lakini hakuna mafanikio,” amesema. 

Ismail amesema baada ya ununuzi wa hoteli hiyo iliyokuwa katika hali mbaya baada ya sehemu yake kubwa ya ardhi kumegwa na maji ya bahari na kuchakaa baada ya kutelekezwa ndipo wakalazimika kufanya ukarabati mkubwa.

“Ikumbukwe kuwa wakati hoteli hii ikiuzwa kwetu ilikuwa katika hatari ya kumezwa kabisa na bahari. Hali hii ilitulazimu kuchukua hatua za haraka za kuinusuru kwa kuuza baadhi ya mali zetu na hata kuweka rehani baadhi ya mali zetu ili kazi ya ukarabati ianze bila kuchelewa. Tulilazimika kutumia mali zetu kuweka rehani baada ya kutopatiwa hatimiliki,” amesema.

Pia amesema walilazimika kuanza mchakato wa kutafuta wataalamu washauri wa masuala ya ujenzi kisha baadaye wakaingia katika mchakato mwingine wa kutafuta mkopo uliowahusisha wataalamu wa masuala ya kifedha (financial consultants) na hatua zote walilipa gharama zake. 

Ismail amesema baada ya kukamilisha hatua hiyo waliomba mkopo kutoka Benki ya EADB uliopitishwa kwa sharti la kuilipa benki hiyo asilimia tatu ya thamani ya mradi wote ili waweze kupata mkopo huo. 

“Hii ilikuwa ni baada ya mkopo kupitishwa (appraisal fee), tuliwaajiri pia wataalamu wa masuala ya bahari wakiwa chini ya Profesa Mtalo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) nao pia tuliingia gharama kubwa ya fedha,” amesema na kuongeza: 

“Pamoja na juhudi zote hizo lakini bado hatukupewa mkopo huo ambao tayari awali ulishapitishwa na sababu kubwa ya kutopatiwa mkopo ilitokana na PSRC kutotupatia hatimiliki ya Hoteli ya Kunduchi Beach.

“Hivyo mkopo ulifutwa na tukapoteza ile asilimia tatu tuliyokuwa tumelipa benki, kitendo kilichotokana na kukosekana kwa dhamana ambayo ni hatimiliki, hali hiyo ilituletea usumbufu na adha kubwa.”

Pia amesema wakati bado wanahangaika namna ya kupata hatimiliki na ‘share certificates’ hizo ndipo maofisa wawili waandamizi wa PSRC (majina yanahifadhiwa) wakawadokeza kwamba wawape fedha ili mchakato wa kukabidhiwa ufanikiwe.

“Jambo hili lilitushangaza na mzee wetu Gulam Ismail ambaye ndiye Mwenyekiti wa Wellwort akakataa kutoa hizo fedha zilizoombwa kwa sababu alisema hawezi kutoa rushwa ya kupata hizo hati kwa kuwa Hoteli ya Kunduchi Beach tumeinunua kwa kufuata taratibu zote za kisheria kama zilivyowekwa na serikali.

“Kwa hiyo baada ya kukataa kutoa fedha tulizoombwa ndipo tukaanza kuhangaika namna ya kupewa hatimiliki na share certificates hiyo. Imefikia hatua hadi tunafikiria pengine hatimiliki na share certificates hiyo hazipo tena labda zilifichwa na wale maofisa waliotuomba tuwape fedha, tunajiuliza kwanini hatupewi?” amehoji.

Katika hatua nyingine, amesema kitendo hicho kilisababisha Oktoba 19, 1999 wao kuingia katika makubaliano ya maridhiano kwa kuwa yale ya awali ya mwaka 1997 yalikiukwa na PSRC baada ya kushindwa kuwakabidhi hatimiliki. 

Ismail amesema katika makubaliano hayo mapya ya mwaka 1999 kwa mujibu wa kipengele cha tatu waliweka utaratibu wa makabidhiano ya hatimiliki kwa utaratibu wa kufanya malipo ya kiasi cha dola 100,000 za Marekani.

Amesema kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni salio la thamani ya ununuzi wa Hoteli ya Kunduchi Beach kwa sharti la kubadilishana na hatimiliki kwa maana ya mkono mmoja kutoa fedha na mkono wa pili kupokea hatimiliki na ‘share certificates’. 

“Tukamjulisha kuwa siku 14 kabla ya siku ya makabidhiano yetu na tuliwakumbushia tena PSRC kupitia kwa Wakili wetu Nyange Advocates juu ya utayari wetu wa kulipa fedha na kubadilishana na hatimiliki. 

“Hatukuishia hapo, bali siku tatu kabla ya kufikia ukomo wa muda (deadline) wa makabidhiano tuliwaandikia tena PSRC barua yenye kumbukumbu namba: WWHL/68/04/2000 ya Aprili 06, 2000 tukiwakumbushia juu ya utayari wetu wa kubadilishana hati na fedha. Pamoja na kuwakumbushia lakini hatukuweza kupata mrejesho wowote kutoka kwao,” amesema. 

Ismail amesema kitendo cha PSRC ambayo baadaye ikavunjwa na majukumu yake kuchukuliwa na Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) kukataa kupokea fedha hizo hakikuwa cha bahati mbaya bali ni mwendelezo wa ukiukwaji wa makubaliano yao.

“Mei 7, 2010 tuliwaandikia CHC hundi ya Benki M yenye namba 001377 ya thamani ya dola l00,000 za Marekani na kumkabidhi Wakili wetu Kampuni ya IMMMA Advocates kwamba hatimiliki na share certificates hizo zitakapokuwa tayari nao wakachukue hizo fedha.

“Lakini zaidi ya mara tatu hawakufanya hivyo na kuleta urasimu wa hali ya juu na ikapita miezi sita ile hundi ika-expire na wale PSRS/CHC hawakwenda kuichukua,” amesema. 

Pia amesema pamoja na maridhiano na kupita zaidi ya miaka 13 lakini bado PSRC/CHC walishindwa kuyatekeleza maridhiano hayo na kusababisha kutopata haki yao.

Kutokana na hali hiyo, amesema hawakuwa na namna nyingine yoyote ya kupata haki bali kulazimika kwenda katika usuluhishi (arbitration) kwa mujibu wa makubaliano.

“Kabla ya kwenda arbitration tulisita kufanya hivyo kwa sababu hatukutaka kuharibu uhusiano wetu mzuri na serikali,” amesema Ismail na kuongeza: 

“Ikumbukwe kuwa hii ilikuwa ni baada ya kufanya juhudi kubwa za kushirikisha serikali yetu ikiwamo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa njia mbalimbali ya mawasiliano ya barua na hata vikao ili tuweze kupatiwa hatimiliki na share certificates.

“Juhudi hizi bado hazikufanikiwa. Hata hivyo, wakati tukiwa katika mchakato huo wa mawasiliano na serikali kulitokea mabadiliko ya PSRC kuvunjwa na kuanzishwa kwa CHC.”

Amesema baada ya kwenda ‘Arbitration’ jopo la waamuzi watatu liliamua kuwa wapewe hatimiliki na ‘share certificates’ kwa kubadilishana na fedha. 

“Pamoja na mwenendo wa arbitration kutoturidhisha kwa mfano mmoja wa waamuzi kutoweka wazi mgongano wake wa masilahi kwa PSRC/CHC kabla ya kushiriki kwake katika kuunda jopo hilo.

“Lakini bado uamuzi wao wa kutaka tupewe hatimiliki na share certificates kwa kubadilishana na fedha haujatekelezwa na PSRC/CHC hadi sasa, sisi kwa upande wetu bila kuchelewa tulitimiza wajibu wetu huu kwa kumkabidhi Wakili wetu IMMMA Advocates hundi yenye thamani ya fedha hizo,” amesema.

Aidha, amesema kwa mara nyingine na kwa sababu wasizozijua hadi sasa PSRC/CHC ilipuuza maelekezo ya waamuzi na kukataa kupokea hundi yao pia wakashindwa kuwakabidhi hatimiliki na ‘share certificates’ hadi wakati huu. 

Amesema jambo hilo linawapa shaka kubwa kwamba pengine kuna kitu kimejificha nyuma ya hatimiliki pamoja na ‘share certificates’ hiyo ndiyo maana inakuwa vigumu kukabidhiwa haki yao. 

Kutokana na urasimu huo, amesema wanaendelea kukwamishwa huku wakishindwa kupata mikopo itakayowawezesha kampuni hiyo kutanuka zaidi. 

Pia katika hali ya kushangaza, amesema Desemba 31, 2015 Ofisi ya Msajili wa Hazina iliyochukua majukumu ya CHC baada ya kuvunjwa iliwachafua kupitia vyombo vya habari kwamba wameitelekeza Hoteli ya Kunduchi Beach.  

“Pamoja na kukwamishwa kote huko lakini tumefanikiwa kufanya uwekezaji wa mfano, hali tuliyostahili zaidi pongezi lakini Ofisi ya Msajili wa Hazina ilitoa taarifa yenye kutuchafua kupitia vyombo vya habari kwa kudai kuwa tumeitelekeza Hoteli ya Kunduchi Beach na tumevunja mkataba,” amesema Ismail na kuongeza:

“Wakati si kweli kwa sababu tangu tulipoinunua mwaka 1997 tulianza ukarabati mkubwa hadi tulipomaliza mwaka 2005 na ikafunguliwa rasmi na kuanza kupokea upya wageni na wateja na ikafanya kazi mfululizo hadi mwaka 2019 tulipoifunga kutokana na mlipuko wa ugojwa wa Covid-19 na baada ya kuifunga tukaamua kufanya ukarabati mwingine kwa mara ya pili.  

“Jambo hilo lilichafua taswira yetu nzuri kibiashara kwa sababu tuko katika ngazi ya juu (A1) kwenye credit reference bureau na kutokana na kitendo cha kuchafuliwa tulifanya juhudi kubwa ikiwamo kumwandikia Msajili wa Hazina kwa lengo la kutaka tusafishwe, kwa sababu tuhuma hazikuwa za kweli.

“Lakini hakufanya hivyo ndipo tukalazimika kwenda kwenye arbitration ili kulinda hadhi yetu. Tungependa ieleweke kuwa kabla ya kwenda arbitration tulitumia zaidi njia za kidiplomasia ili kutaka kusafishwa kwa kuombwa radhi kwa kitendo hicho.

“Hata hivyo pengine kwa bahati mbaya au kwa kudhamiria Ofisi ya Msajili wa Hazina hawakujali kutuomba radhi ili walau kulinda heshima na hadhi ya biashara yetu.” 

Wiki iliyopita Gazeti la JAMHURI liliwasiliana na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Ofisi ya Msajili wa Hazina, Eric Anthony, ambaye pamoja na mambo mengine amesema anachofahamu ni kwamba mwekezaji huyo wa ndani anadaiwa dola 100,000 za Marekani ndiyo maana hadi sasa bado hajapatiwa hatimiliki na ‘share certificates’.

“Nafuatilia hilo suala lakini kwa maelezo ya haraka ni kwamba huyo mwekezaji hajamaliza kulipa gharama za dola 100,000 za Marekani,” amesema.

Hata hivyo, mwandishi wa habari hii akamwaleza Anthony kwamba mwekezaji huyo ameshafanya juhudi za kulipa kiasi hicho cha fedha siku za nyuma lakini CHC ikashindwa kuzichukua.

“Sisi ni wageni tulirithi haya majukumu kutoka CHC. Kuna vitu vingine hatuvijui, kutoa hati si tatizo kwetu, lengo letu sisi ni kutoa hati, inabidi huyo mwekezaji atenge tu muda wake aje hapa ofisini tuzungumze naye,” amesema.

Baada ya kusema hivyo akawapangia miadi ya Alhamisi wiki iliyopita saa nne asubuhi kukutana na Mkurugenzi wa Ubinafsishaji, Ufuatiliaji, Tathmini na Utafiti wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohammed Nyasama.

Siku ilipofika, Mwenyekiti wa Wellworth, Gulam, aliongozana na maofisa wengine akiwamo Ismail, Ofisa Utawala, Simon Nguka na Katibu Mtendaji, Henry Massaba, kwenda kukutana na Nyasama lakini kikao hicho hakikufanyika na wakakubaliana kupanga siku nyingine ya kukutana.

By Jamhuri