Mwendokasi wa magari sasa ujangili mpya Hifadhi ya Taifa Mikumi

Umewahi kuendesha gari katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na ukamgonga mnyama yeyote ndani ya hifadhi? Unakumbuka kama ulilipa faini za kumgonga mnyama? Basi kwa taarifa yako magari ndiyo yamekuwa majangili wapya katika hifadhi hiyo.

Wakati Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) wakishusha kiwango cha ujangili katika hifadhi hizo, sasa ujangili mpya ni ule unaohusisha magari. Magari ndani ya Mikumi yamekuwa yakisababisha ajali, kwa mujibu wa takwimu mnyama mmoja anakufa kila siku.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Godwell Meing’ataki, anasema hali ya wanyama kugongwa ndani ya hifadhi ni mbaya.

“Hifadhi yetu ya Mikumi sasa ina jangili mkubwa anaitwa barabara, huyu kwa wastani anaua mnyama mmoja kila siku, chati ya wanyama wanaouawa kwa ujangili imeshuka lakini wanyama wanaouawa kwa kugongwa na magari inapanda kila siku,” anasema mhifadhi huyo.

Anasema uwepo wa barabara ya kimataifa ya TANZAM, inayokatisha katikati ya hifadhi hiyo ikielekea Zambia na Malawia ni changamoto kwa uhifadhi katika Hifadhi ya Mikumi.

Pamoja na barabara hiyo kusaidia kuleta maendeleo na kuifanya hifadhi hiyo kufikika kirahisi, imekuwa na changamoto nyingi, vikiwemo vitendo vya magari kugonga wanyama na wasafiri kutupa taka.

Mhifadhi huyo anasema wastani wa mnyama mmoja hugongwa kila siku. Ambapo idadi hiyo kwa mwaka inakadiriwa kuwa wanyamapori zaidi ya 360 wanagongwa.

Vitendo vya wanyama kugongwa na utupaji wa taka hufanyika kuanzia Kijiji cha Doma ambacho kimepakana na hifadhi hiyo kama mtu anatokea Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mhifadhi wa Mikumi, gari likimgonga mnyama katika hifadhi litatozwa faini mara mbili, yaani faini ya gari husika na faini ya kusababisha kifo cha mnyama kinachotokana na kugongwa.

Anaitaja faini ya gari lililosababisha ajali kuwa ni Sh 200,000 huku akibainisha kuwa faini zinazotolewa kwa wanyama wanapogongwa zinazingatia aina na thamani ya mnyama husika.

Meing’ataki anasema kuwa viwango vya faini hizo vimewekwa kwa mujibu wa kanuni na sheria inayosimamia uwindaji katika maeneo yenye hifadhi.

Anaainisha viwango vya faini hizo kulipwa kwa mfumo wa dola za Marekani, na kwamba gari likimgonga tembo au twiga faini yake ni dola za Marekani 15,000 sawa na zaidi ya Sh milioni 34.

Anasema faini inayotozwa kwa mnyama kama nyati thamani yake ni dola za Marekani 1,600, huku simba faini yake akiitaja kuwa ni dola za Marekani 4,900.

Faini za wanyama wengine kama nyani, anaitaja kuwa ni dola za Marekani 120, chatu dola za Marekani 360, korongo dola za Marekani 2,550, ngiri ni dola za Marekani 450 na mbwa mwitu ni dola za Marekani 1,200.

Anaeleza kuwa korongo ni wanyama ambao wanagongwa hovyo, hivyo viwango vyao vimewekwa juu kwa ajili ya kuwalinda.

Ameongeza kuwa thamani ya wanyama wadogo kama kobe, faini yake ni dola za Marekani 70, chura dola za Marekani 20, huku akiitaja faini ya kipepeo kuwa ni dola za Marekani 10 na kwamba akibainika aliyehusika kumgonga ni lazima atalipa faini hiyo.

Kwa upande mwingine anaeleza kuwa faini ya mnyama kama kiboko ni  dola za Marekani 1,500, huku chui faini yake ikiwa ni dola za Marekani 3,500.

Mhifadhi huyo anasema faini hizo zinatozwa kwa mujibu wa sheria ya kuwalinda wanyama ya mwaka 2009, Kifungu namba 5 na kwamba utekelezaji wake unafanywa kwa kuzingatia sheria inayoratibu matumizi ya nyara za serikali ya mwaka 2011.

Ameeleza kuwa fedha zinazokusanywa kutokana na makosa hayo ya kuwagonga wanyama huingizwa katika mapato ya serikali, ambapo malipo hayo hufanyika benki kupitia akaunti za Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) katika Hifadhi ya Mikumi.

Urefu wa kipande cha barabara kinachopita kwenye hifadhi hiyo ni kilometa 50, ambapo urefu huo unaishia Kijiji cha Kidoma kilichopo Kata ya Mikumi.

Meing’ataki anasema wanyamapori wa kila aina hugongwa katika kipande hicho huku akiwataja wanyama aina ya swala kugongwa kwa wingi.

Anabainisha kuwa huenda takwimu hizo zikawa ndogo kutokana na matukio mengi ya kugonga wanyama kutokea usiku.

“Kuna wanyama wanaogongwa usiku na kuangukia porini na sisi hatuwezi kuwaona, kuna uwezekano mizoga hiyo inaliwa na wanyama kama fisi,” anasema Meing’ataki.

Anaongeza kuwa wanyama kama nyoka, mijusi, kobe na wadudu kama vipepeo nao wanagongwa na kwamba endapo wakiwahesabu idadi ya wanyama wanaokufa kwa kugongwa inaweza kuwa kubwa zaidi.

Mbali na wanyamapori kugongwa na magari, changamoto nyingine kwa Hifadhi ya Mikumi inayoletwa na barabara hiyo ni utupaji wa taka unaofanywa na wasafiri. Meing’ataki, anasema uchafu unaotupwa pembezoni mwa barabara hiyo ni wastani wa kilo 138 kwa siku. Anaeleza kuwa kilo hizo hupatikana baada ya kukusanywa na kupimwa kwenye mizani ili kupata kiwango cha uharibifu wa mazingira ya hifadhi kinachofanywa na wasafiri hao.

Meing’ataki anazitaja taka za vyakula na matunda kuwa na madhara makubwa kwa hifadhi hiyo huku akizieleza kuhatarisha ustawi wa uoto wa asili uliomo katika hifadhi. Anaeleza kuwa mbali na taka hizo kuharibu uoto wa asili wa hifadhi, kuna hatari ya wanyamapori kubadilika kitabia kutokana na taka hizo.

“Wasafiri wanaopita katika barabara hii ni wa kila aina na kila mmoja anakuwa na vyakula, wapo wanaobeba chips (viazi ulaya vilivyokaangwa kwa mafuta) ikiwemo nyama ya kuku.

“Wako wengine wanapita hapa wamebeba matunda ya kila aina, maembe, nyanya, matikiti maji, maboga na machungwa, matunda hayo mbegu zake zinapodondoka kwenye hifadhi na kuota zinaharibu uoto wa asili ndani ya hifadhi.

“Kwa sababu mimea hiyo ni vamizi kwa uoto wa eneo hili, tunapata tabu ya kuzunguka hifadhi yote ili kuibaini na tukiiona tunaing’oa,” anasema Meing’ataki.

Mhifadhi huyo anasema kuwa wanyamapori wanapokula vyakula na matunda hayo yaliyotupwa na wasafiri kuna hatari ya kubadilika kitabia.

Anasema wanyama hao wanaweza kuanza kutoka katika maeneo yao ya asili na kuja kukaa barabarani wakisubiri mabaki ya vyakula na matunda hayo.

Athari itakayojitokeza kutokana na wanyama hao kubadilika kitabia ni pamoja na hifadhi kukosa wageni wanaokuja kutalii, hivyo Hifadhi ya Mikumi kushindwa kuchangia pato la taifa, kwa sababu wanyama wote watakuwa wanaonekana kwa urahisi.

Mhifadhi huyo anasema kuwa hamasa ya watu kutaka kuingia kwenye hifadhi kutalii itapungua kutokana na sababu ya wanyama kuonekana kirahisi pembezoni mwa barabara.

Madhara mengine anayataja kuwa ni vifo vya wanyama vitokanavyo na kula taka hizo, anawataja wanyama kama fisi kwamba wao hula kila kitu wanachokutana nacho, hivyo wamo hatarini kufa kwa sababu ya kula mifuko ya plastiki inayotupwa ikiwa na vyakula.

“Wakila mifuko inaweza kukwama kwenye koo la hewa, na kwa sababu wanyama hawaongei unaweza kushangaa tu wanakufa bila kujua chanzo cha vifo hivyo,” anaeleza.

Meing’ataki anaongeza kuwa baadhi ya taka zinakuwa ni matapishi ya watu na vinyesi vya watoto, hivyo hali hiyo inahatarisha afya za wanyamapori katika hifadhi.

Anaeleza kuwa matapishi hayo kama ni ya mtu mgonjwa, ugonjwa huo unaweza kumshika mnyama akiyala na kwa sababu mbuga ni kubwa athari ya ugonjwa huo inaweza kuenea hata kwa wanyama wengine.

Meing’ataki anasema ili kudhibiti vitendo vya kuwagonga wanyama na utupaji wa taka katika hifadhi wanashirikiana na Jeshi la Polisi – Kikosi cha Usalama Barabarani.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe, ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa ili kuepukana na vitendo hivyo vya utupaji taka na kugonga wanyama, mpango wa kuchepusha barabara hiyo umekwisha kuanza.

Amesema barabara inategemewa kujengwa kwa ajili ya watu wanaosafiri kwenda mikoa ya Iringa na Mbeya pamoja na nchi ya Zambia na Malawi, na kwamba itaanzia Melela kwenda Kilosa hadi Mikumi ikipita pembeni mwa hifadhi.

“Hiyo barabara inayopita mbugani tuna mpango wa kuachana nayo ili ibaki kwa watumiaji wanaoingia mbugani kutalii peke yake,” anaeleza Mhandisi Kamwelwe.

Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro (RPC), Wilbroad Mutafungwa, amelieleza JAMHURI kuwa wanashirikiana na wahifadhi wa Mikumi kudhibiti vitendo vya wanyama kugongwa.

Kamanda Mutafungwa anasema ili kudhibiti vitendo hivyo inahitajika elimu kubwa kwa madereva na watu wanaomiliki vyombo vya usafiri pamoja na wasafiri kwa ujumla.

“Sisi Jeshi la Polisi tunashirikiana na askari wa wanyamapori vizuri, tunahakikisha kwamba alama zilizowekwa katika hifadhi hii zinazingatiwa na madereva, lakini mara nyingi matukio ya kugonga wanyama hutokea usiku na usiku hatufanyi doria ya kupima mwendo wa vyombo vya moto.

“Kuna sheria inayomtaka dereva kuendesha gari kwa mwendo wa kilometa 70 kwa saa akiwa kwenye hifadhi wakati wa mchana na kilometa 50 kwa saa wakati wa usiku na vingine vinapima hadi mwendo kasi wa kilometa 30 kwa saa kulingana na eneo hilo kuwa na wanyama wengi wanaovuka barabara, tunajitahidi kuelimisha madereva ili huo mwendo uzingatiwe,” anasema Mutafungwa.

Hata hivyo anasema hana kumbukumbu sahihi za takwimu kuhusu wanyama waliogongwa kwa miaka ya hivi karibuni, pia matukio ya watu na madereva kukamatwa na kutozwa faini.

Pia ameongeza kuwa makosa ya kuvunja sheria za usalama wa barabara hiyo inayopita kwenye hifadhi yapo lakini hana kumbukumbu ya idadi yake. Kwa upande mwingine, Kamanda Mutafungwa anasema wanashirikiana bega kwa bega na askari wa wanyamapori kudhibiti vitendo vya ujangili katika hifadhi hiyo na vimepungua kwa kiasi kikubwa.

Akizungumzia kuhusu hali ya ujangili wa wanyamapori, mkuu wa hifadhi hiyo alilieleza JAMHURI kuwa ujangili kwa ajili ya biashara umepungua ila umebaki wa kuwinda wanyama kwa ajili ya kitoweo.

“Kwa miaka mitatu sasa hatuna ujangili wa meno ya tembo katika Hifadhi ya Mikumi, hapa ujangili ulikuwa ni mkubwa, tembo walikuwa wanawindwa hadi karibu na ofisi zetu.

“Rais Dk. John Magufuli aliwahi kusema majangili wadhibitiwe hadi wenyewe wakiwaona tembo wawe wanawakimbia…nakuhakikishia shughuli hiyo tumeifanya kikamilifu, ujangili uliobaki ni wa kuwinda kwa ajili ya nyama.

“Hata huo nakwambia tutaudhibiti kwa sababu jinsi unavyofanyika tunajua na wanaofanya tutazidi kuwafuatilia ili tuwabaini,” anasema Meing’ataki.

Anaongeza kuwa, kwa sababu Hifadhi ya Mikumi ni eneo ambalo wanyama huingia na kutoka ‘eco system zone’, hivyo ni vigumu kuwa na takwimu sahihi za wanyama waliomo.

Anabainisha kuwa wakati wa kiangazi maji yanakuwa tatizo kubwa katika hifadhi hiyo, hali inayowaathiri wanyama na kusababisha baadhi wahame kwa ajili ya kuafuta malisho na maji ya kutosha. Na kwamba ili kukabiliana na changamoto hiyo wamechimba mabwawa ya kutunza maji ya mvua zinazonyesha kipindi cha masika.

Samwel Mgohachi, ni Mwikolojia wa Hifadhi ya Mikumi, anaielezea hifadhi hiyo kukosa chanzo cha kudumu cha maji kabisa. Kukosekana kwa chanzo cha maji cha kudumu katika hifadhi hiyo anasema ni changamoto hata kwa mimea iliyomo.

Anaeleza kuwa kipo chanzo cha maji kinaitwa Mto Mgeta, kilichopo kwenye Msitu wa Malundwe na kwamba kinapitisha maji yake karibu na hifadhi, lakini badala ya kuingiza maji hifadhini kinayatoa nje ya hifadhi.

Mwikolojia huyo anathibitisha kuwa tatizo la kugongwa kwa wanyama katika hifadhi hiyo linasababisha kukosekana kwa usawa baina ya wanyama na mazingira ya hifadhi kwa ujumla.

Hata hivyo anathibitisha kuwa taka nyingi zinazotupwa katika hifadhi hiyo ni taka ngumu yakiwemo matairi ya magari, vyuma na chupa za plastiki, na kwamba taka hizo athari yake ni ndogo kwa wanyamapori, zaidi zinaharibu muonekano wa mazingira ya hifadhi.

Amewataka madereva kuwa makini na utupaji wa vipande vya sigara pale wanapomaliza kuvuta, kwani vimekuwa na madhara ya kusababisha moto unaoteketeza uoto wa hifadhi na kusababisha vifo vya hovyo kwa wanyama wasio na uwezo wa kukimbia haraka.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) chini ya  ufadhili wa USAID protect.