Mwili wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis umehamishwa hadi kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro ambapo maelfu ya watu watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kwa muda wa siku tatu.
Ni kwa nyimbo za ibada huku Kengele za Kanisa la Mtakatifu Petro zikilia, ndivyo jeneza la mbao na la wazi la Papa Francis lilibebwa katikati ya umati wa watu waliojaa katika uwanja wa kanisa hilo wakisindikizwa na makadinali waliovalia mavazi mekundu na kusindikizwa na Walinzi wa Vatican wanaofahamika zaidi kama “Vikosi vya Uswisi”.
Waumini, mahujaji na watalii walipiga picha za ukumbusho, huku wengine wakipiga makofi kama ishara ya heshima kwa Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki wakati msafara huo ukipita kutoka kwenye makazi ya Mtakatifu Marta, ambapo papa huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 88 alifariki Jumatatu baada ya maradhi ya muda mrefu na ambako aliishi kwa miaka 12 ya uongozi wake.
Mauro raia wa Italia na Jose Rojo kutoka Mexico ni miongoni mwa walioshuhudia jeneza hilo la Papa Francis likiwasili katika kanisa la Mtakatifu Petro siku ya Jumatano na walikuwa na haya ya kusema:
” Binafsi nilimchukulia kama mtu ambaye aliwakilisha enzi za mabadiliko kwa imani ya Kikristo ambayo tunapaswa kudumisha, na ndiyo sababu sikuweza kuikosa fursa hii.”
” Nimejawa na hisia ya huzuni kuona kwamba papa hayuko nasi tena. Papa alikuwa karibu sana na vijana pamoja na watu wa Amerika ya Kusini.”
