Hasira hupunguza furaha katika maisha

Hasira iko tofauti na upendo, hasira iko tofauti na furaha, hasira iko tofauti na msamaha. Hasira iko tofauti na huruma, hasira iko tofauti na amani.

Ndugu wa hasira anajulikana, ndugu huyo ni hasara. Kila mmoja anaifahamu hasira, kila mmoja anafahamu ule msemo wa ‘Hasira ni hasara’.

Katika ndoa unaweza kuitwa baba upendo au baba hasira au ukaitwa mama hasira, kaka hasiradada hasira.

Jiulize kwa usikivu mwanana, je, majina  hayo yana utukufu wa Mungu ndani yake? Jibu ni hapana. Jiulize kwa usikivu mwanana kwa nini hasira ikushushie thamani ya utu wako? Kwa nini hasira ikuibulie majina mapya kila siku? Kwa nini hasira ikufanye uishi maisha ya kufungwa kana kwamba uko gerezani?

Elewa kwamba hasira inaweza kukufanya mahusiano yako na mke wako yakawa mabaya, hasira inaweza kukufanya mahusiano yako na majirani zako yakawa mabaya.

Hasira inaweza kukufanya mahusiano yako na watoto wako yakawa mabaya, pia hasira inaweza kukufanya mahusiano yako na wafanyakazi wenzako yakawa mabaya, hivyo inaweza kukufanya ukafukuzwa kazi.

Hasira inaweza kukufanya ukaogopwa na kila mtu, hasira inaweza kukufukuzia wateja wako, hasira inaweza kukufanya ukawa na mvuto mbaya kwa kuwa na makunyanzi ya kudumu usoni. Hasira inaweza ikakuharibia heshima yako kwa sababu ya kununa muda wote. Hasira inapunguza upendo.

                                                                                          

Zipo aina tatu za hasira ambazo ni:

(i) Hasira ya maumbile

Hii hasira ya maumbile tumeumbwa nayo ili itusaidie. Kwa mfano ile hasira aliyoitumia Yesu kuwafukuza wafanyabiashara kutoka hekaluni ilikuwa hasira ‘Takatifu’ na haikuwa na madhara kwa yeyote.

Ukivamiwa na majambazi ni lazima ukasirike ili uweze kujilinda (usipochukua uamuzi wa kujilinda unaweza kuuawa), hasira ya maumbile inakusaidia kujilinda. Hasira hii ya maumbile hata viumbe wengine wanayo.

Tutumie hasira ya maumbile kwa viumbe wengine kupitia kwa ndege aina ya kuku. Kuku akiwa na vifaranga ukimchokoza anakasirika ili kuwalinda watoto wake.

Hasira ya kuku inamsaidia kuwalinda watoto wake dhidi ya mwewe, hasira yake inamsaidia kuwalinda vifaranga wake wasikwapuliwe na mwewe. Hasira hii ya maumbile haina hasara yoyote.

 

(ii) Namna unavyochukulia mambo/uelewa wako kuhusu mambo

Kiwango chako cha kujua au kufahamu ndicho kinachokufanya ukasirike au usikasirike, uelewa wako juu ya jambo fulani unaweza ukakufanya ukakasirika ama usikasirike.

Kwa mfano, tusi, ni namna unavyolichukulia wewe, ukilichukulia kama kudhalilishwa utakasirika, lakini ukilichukulia kama moja ya upungufu wa kibinadamu utaipoza hasira yako. Utapotezea.

Tusi halina alama lakini linaujeruhi moyo. Iko hivi, wewe ni Mkristo na tabia inayomtambulisha Mkristo ni tabia ya unyenyekevu. Unapokuwa umetukanwa ama umeudhiwa kupita kiasi nyamaza.

Lakini unyamavu wako uwe ni sababu ya kumwombea aliyekutukana ama aliyekuudhi. Kuna mtu anaweza akawa anatenda kosa lakini akawa hajui kama anatenda kosa. Vilevile kuna mtu mwingine anaweza akawa anatenda kosa na akawa anafahamu wazi kwamba anatenda kosa.

Wote hawa ni wa kuhurumia kwa sababu hawajui walitendalo. Washangaze maadui zako kwa zawadi ya msamaha. Shinda ubaya kwa wema, usilipe kisasi.

Ni rahisi kwa mtu mwema kama wewe, kutendewa usiyoyapenda, wakati mwingine utajikuta unakosolewa hadharani hata kama uko sahihi. Unachekwa isivyostahili, unadharauliwa na kutukanwa waziwazi. Tafadhali vumilia, usilipe ovu kwa ovu, chukia tabia ya kuwa na maadui wengi.

Pigania jambo kwa ajili ya kupata faida na si ufahari. Kaa mbali na malumbano yasiyo na faida maishani mwako.

Malumbano hayana faida katika maisha, yaepuke, yakimbie, yakatae. Usililie ulichokipoteza, pigania ulichonacho, usililie kilichokufa, pigania kinachozaliwa katika wewe.

Usimlilie yule aliyekuacha, mpiganie yule aliyeko na wewe. Usiwalilie wale wanaokuchukia, wapiganie wale wanaokupenda. Usiililie jana yako, pigania juhudi zako za sasa. Usililie mateso yako, pigania furaha yako.

Mambo mengine unapaswa kupotezea kama hauoni kitu, hii ni njia mojawapo ya kuonyesha ukomavu wako wa kiroho na kiakili katika kukabiliana na vionjo vyako vya kimaumbile.

Kuelewa kwako na kutafsiri kwako mambo kunaweza kukusaidia usikasirike au kunaweza kukufanya ukakasirika. Kwa hiyo jaribu kutafsiri mambo katika miwani  chanya.

Please follow and like us:
Pin Share