Nchi yetu haina dini. Haya ni maneno maarufu katika masikio ya Watanzania. Mwasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake maneno haya aliyasema mara kwa mara. Katika moja ya hotuba zake, alisema:
“Siku moja nikiwa Zanzibar, kuna masheikh, wamevalia baragashia, nikawa nimealikwa kama mgeni rasmi. Nilipowaona wale masheikh nikasema hapa nitarudia ile ile… nikasema, nchi yetu haina dini. Nilipotoa kauli hiyo, masheikh wakainama kwa chini chini wakisema astaghafruhai, astaghafurahi… nikafafanua kuwa wananchi mmoja mmoja wana dini zao ila nchi yetu haina dini.”
Ibara ya 19 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema: “Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.”
Sitanii, Mwalimu Nyerere na msingi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), imejikita na inalenga katika kuondoa hisia za udini katika jamii. Amani tunayoishuhudia leo, imejengwa kwa jasho na akili kubwa. Tangu Mwalimu Nyerere afariki dunia, zimekuwapo hatua za makusudi za kubomoa misingi ya amani ya nchi yetu.
Mwalimu Nyerere aliishi maisha ya kupambana na udini, ukabila, ubaguzi, ubabe wa aina mbalimbali na uvunjaji wa sheria. Nikisafiri katika nchi kadhaa, nchi nyingi zinaisifia Tanzania kwa amani tuliyonayo, uvumilivu wa kisiasa, upendo, umoja na udugu. Kwa Kenya hadi leo, wanaamini sisi Watanzania tunaitana, na kiuhalisia ni ndugu.
Lakini leo ninavyoandika makala hii, hali hii inayeyuka kwa kasi. Ilianza kidogo kidogo. Wabunge waligoma kuitwa ndugu, wakapitisha hadhi ya kuitwa Mheshimiwa. Hili lilipopita, wakanogewa. Wakifika polisi, au hata harusini wakati wa kujitambulisha wanasema wazi. Utasikia mtu anasema “Mimi naitwa Mheshimiwa…”
Baada ya kuvuka mstari wa uheshimiwa, tunakijita katika mazingira ambayo viongozi wetu wameanza kutafuta mbinu nyepesi za kupata uongozi. Msomaji utanisamehe. Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Peter Kayanza Pinda sasa anashiriki kwa kasi kubomoa misingi ya nchi hetu. Kwa sasa anapigia chepuo Mahakama ya Kadhi.
Pinda anasema mahakama hii itashughulikia mirathi na ndoa. Muswada unapelekwa katika bunge linaloanza leo, kuwapa ndugu zetu Waislamu haki hii. Hapa mimi nasema tunamkaribisha twiga kwenye nyumba ya mabua. Tutakuwa tumefanya kosa kubwa mno, tukidhani misingi ya nchi yetu imejengwa kwa zege na nondo.
Sitanii, ipo hadithi ya twiga. Mvua ilikuwa inanyesha. Twiga akaomba hifadhi kwenye nyumba ya mkulima aliyekuwa anaishi karibu na mbuga. Nyumba yake ilikuwa imejengwa kwa mabua ya mahindi. Twiga akamwambia anasikia baridi sana, hivyo anaomba msaada ahifadhi japo kichwa tu ndani ya nyumba hiyo.
Mkulima akamuonea imani twiga yule. Akamruhusu aingize kichwa. Baada ya kichwa, twiga akasema mabega yanasikia baridi sana, kwa kuwa mkulima ameishaamua kumsaidia, amruhusu aingize na mabega. Mkulima akasema sawa. Kisha akasema mgongo unanyeshewa vibaya, mkulima akasema sawa, ila akamhoji, utawezaje kuingiza mgogo na urefu wako huu?
Twiga kwa unyenyekevu mkubwa, akamwambia atachuchumaa. Baada ya kauli hiyo, mwenye nyumba akasema sawa. Twiga akajipinda kwa tabu na kuingia kwenye kibanda hicho cha mabua. Baada ya muda, miguua aliyoipinda twiga ikauma. Kwa kujisahau tu, akaamua kujinyoosha kwa kusimama juu. Kwa uamuzi huo, twiga akakifumua kibanda.
Sitanii, haikuwa nia ya twiga kuvunja kibanda kile, bali uhalisia kuwa kumkunja twiga aingie kwenye banda la mabua, ulikuwa uamuzi ambao haukuona mbali. Nikiacha mfano huo, nikusafirishe msomaji wangu na kukupeleka Uganda.
Mwaka 1986 Rais Yoweri Kaguta Museveni alipoingia madarakani nchini Uganda, alirejesha utawala wa kifalme katika eneo la Buganda. Mfalme Kabaki, aliamua kumtambua tena, baada ya utawala wa Kabaka kuwa umefutwa na marais waliotangulia. Museveni alidhani kwa kumpa Kabaka hadhi yake ya ufalme wangeishi kwa amani zaidi.
Miaka minne baadae, maafisa wa kodi walipokwenda kukusanya kodi katika eneo la Buganda, ambalo linahusisha jiji la Kampala, wakaambiwa Rais Museveni hana mamlaka juu ya eneo hilo. Wakasema kama ni kodi wanalipa kwa Kabaka. Tatizo hilo kati ya Kabaka na Serikali kuu lipo hadi leo Uganda. Serikali inalazimika kupigana vita ya ndani kwa ndani kwa sababu tu, Mfalme Kabaka hatambui mamlaka ya Serikali Kuu hadi leo.
Kwa hapa Tanzania, mwaka 1963 Mwalimu Nyerere alifuta ufalme. Zipo koo au makabila yenye kutamani sana ufalme urejeshwe katika nchi hii. Wanatamani kumuona Mangi, Rukamba, Mkwawa wakiwa na mamlaka ya kifalme. Tukiruhusu ujio wa Mahakama ya Kadhi, nini kitazuia ujio wa ufalme katika nchi yetu?
Sitanii, nafahamu tatizo hili lilikoanzia. Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ni taasisi ya kidini. BAKWATA ni sawa na ilivyo TEC. Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) linawakilisha Wakatoliki. Haijapata kutokea Anglikana, Walutheli au Walokole wakaambiwa mwakilishi wao halali ni TEC. Hawa wote wanatambuliwa.
Hatua ya Serikali kwa upande wa Waislamu kutambua BAKWATA kama chombo pekee cha kuwakilisha Waislamu, ni kero. Hatua ya Serikali kumlipa mshahara Mufti, kuipa magari BAKWATA ni wazi Serikali imejingiza katika dini. Haifanyi hivyo kwa Suni, Answar Suni, Ismailia au madhehebu mengine ya Kiislamu. Hii ni hatari.
Nchi yetu inapaswa kukubali msimamo na tamko la kikataba kuwa Serikali haitajiingiza katika uendeshaji wa shughuli za kidini, lakini inachofanya kwa BAKWATA, kinaacha maswali mengi. Inawezekana matendo ya Serikali kwa BAKWATA ndio yanawashawishi Waislamu kuona umuhimu wa wao kuwa na chombo cha kuamua kesi zao.
Sitanii, nikirejea katika mada ya msingi, nia ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi inaweza kuwa njema, lakini mkondo wa kuiendesha kwa kutumia kodi za wananchi, kwa ama hukumu za mahakama hiyo kusajiliwa katika Mahakama Kuu au Waziri mwenye dhamana na masuala ya sheria kuthibitisha maamuzi ya mahakama hiyo ni kuingiza dini katika utandaji wa Serikali.
Dini zinapaswa kujiendesha kwa sadaka au michango ya waumini wao. Leo kama Mahakama ya Kadhi itaanzishwa, Kanisa Katoliki kwa mfano linazo sheria zake. Sheria hizi zinafahamika kama Canon Laws. Sheria hizi ni kali mno. Kwa Wakristo wanaokengeuka, huadhibiwa kwa kunyimwa huduma za kanisa (excommunication).
Kama tutaruhusu ujio wa Mahakama ya Kadhi, tujue tunafungua mlango wa Wakristo kutaka kesi zao ziishie kanisani. Nchi hii haitatawalika. Maelezo kwamba kesi za Waislamu zikihukumiwa na mahakimu au majaji Wakristo hawazifahamu vyema sheria za Kiislamu hayana mashiko. Sheria ya Kiislamu (Islamic Law) kwa yeyote aliyesoma sheria anaisoma.
Mfumo wetu wa kutoa haki, ambao Ibara ya 107A ya Katiba ya Tanzania tumeutumia kwa miaka zaidi ya 50 sasa, haujawa na kasoro. Tukiingiza imani katika uendeshaji wa nchi kwa matarajio kuwa ama tutapigiwa kura na Wakristo au Waislamu, tutaitumbukiza nchi katika vurugu.
Maneno kwamba Tanzania inaendeshwa kwa mfumo Kristo hayana mashiko. Leo naamini kama Rais angekuwa Mkristo, Makamu wa Rais akawa Mkristo, Rais wa Zanzibar akwa Mkristo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Pili ambao ni viongozi wakuu watano wakawa Wakristo, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi na wengine watendaji wakuu wangekuwa Wakristo, lisingekosekana neno.
Ni katika kuvumiliana, Wakristo wanachukulia uwepo wa viongozi hawa wakuu katika nafasi hizi kuwa zimeshikiliwa na Watanzania na si kwa dini zao. Ikiwa Tanzania hatuwezi kuliona hili, leo tukaanza kuchokonoa mtungi uliotuhifadhia maji miaka mingi, tutajikuta pabaya.
Pinda inawezekana anadhani kauli hizi za kuonekana anaunga mkono Waislamu zitamsaidia kupata urais katika tangazo lake la kimyakimya. Na hasa kule Zanzibar, alikowambia Zanzibar sio nchi. Mimi nasema bora Tanzania ibaki, Pinda akose urais ikiwa nia yake ni hiyo ya kupata urais kwa kuchana umoja wa kitaifa.
Sitanii, maaskofu wametoa tamko la kupinga Mahakama ya Kadhi. Nimesikia baadhi ya viongozi wanawabeza. Wanasema waachane na siasa. Wiki iliyopita, nimeandika kuwa miaka 313 baada ya Kristo, Mfalme Constantine alisitisha mauaji na unyanyasaji kwa Wakatoliki katika taifa la Roma. Constantine alikuwa mtoto wa Mtakatifu Hellen.
Nchi nyingi duniani, ziliona tabu ya kuchanganya dini na utawala wa kiserikali. Ndio maana kwa busara za wahenga wakasema dini zikae huko zijiendeshe kwa sadaka na misaada, kisha kama Kaizari alivyokuwa akikusanya kodi, ya Mungu yabaki kwa Mungu na ya Kaizari yabaki kwa Kaizari.
Nahitimisha makala hii kwa angalizo kwa Rais Jakaya Kikwete. Rais Kikwete umebakiza chini ya miezi sita kuhitimisha uongozi wako. Haya majipu wanayokutengenezea marafiki zako, likiwamo hili la kuanzisha Mahakama ya Kadhi yaangalie kwa jicho la ziada. Usiruhusu wewe kuwa Rais wa mwisho kutawala Tanzania yenye amani.
Baadhi ya watendaji na wagombea watarajiwa, hupenda kutumia saa za mwisho za uongozi kupitisha mambo yao. Ukiyaruhusu, utaingia kwenye vitabu vya historia ya viongozi walioshindwa, wakati tayari uliishajiandikia historia iliyotukuka ya kuboresha uhuru wa mawazo, uhuru wa imani, miundombinu kama barabara na mengine mengi.
Sitanii, maaskofu hawajakurupuka. Tanzania haijawa tayari kwa Mahakama ya Kadhi. Kuanzishwa kwake, kutakuwa chimbuko la vurugu za kidini. Tunayo matatizo mengi ya kiuchumi. Siamini kama Tanzania ina tatizo la imani kwa sasa. Matatizo yetu ni ujinga, maradhi na umasikini. Tushughulikie hayo, badala ya kulitumbukiza taifa letu katika udini.

 

2608 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!