Ndugu Rais safari yangu ya kwanza kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC ilinifanya niwaamini waliosema, tenda wema nenda zako, usingoje shukrani.

Ujio wa Rais wa DRC ndugu Félix Tshisekedi umenikumbusha yaliyonitokea huko baada ya Rais Laurent Kabila kuikomboa Zaire kutoka kwa Mobutu Sesseseko. Kazad Nyembwe maarufu kama Didy au Mtoto wa Bwana aliniambia, “Mayega njoo Zaire upate kuelewa power (nguvu) maana yake ni nini. Sikumuelewa, lakini nilienda DRC.

Baba, wanaosema ulinzi wako unatisha hawakuuona ulinzi wa hayati Rais Laurent Kabila. Aliingia madarakani kwa bunduki. Kwa wema wako umekuwa ukiwakirimia watu wako fedha taslimu katika ziara unazofanya. Ziara inapokuwa ndefu ni wazi na masanduku ya fedha yatakuwa mengi. Mbunge Kingu aliliomba Bunge likuongezee ulinzi. Sintofahamu ni wanaosema ni joto la uchaguzi mkuu. Kwamba wanufaika wamepangwa. Utaratibu wa serikali kuwasaidia wenye uhitaji unajulikana. Hata wakisema sehemu ya fedha hizo zinamrudia mtoaji, baba ikikupendeza, tuwapuuze!

Nilipotua uwanja wa ndege wa Njilii, (kama Mwalimu Nyerere kwetu) askari walinipokea walinipitisha chumba cha watu maarufu, VIP. Hapa kwetu mimi ni kati ya malapulapu ambao ni marufuku kuingia VIP. Kumbe hata ndani ya VIP kuna VIP zaidi inayotumiwa na rais wa nchi. Basi baba fikiria, niliwekwa humo!

Baadaye nilipelekwa nyumbani kwa wazazi wake. Nikamkuta akiwa na mama yake na hayati baba yake. Mama aliruka kwa furaha akanikumbatia na kuniambia, “Mwanangu umemfuata mwenzako? Wewe ndiye ulikuwa rafiki yake wa kweli kule Tanzania wakati alikuwa hana kitu. Karibu sana!’’ Akaingia jikoni akatusongea ugali. Tulikula kwa kutoelea. Ugali sahani moja na mboga na mchuzi wake katika bakuli moja. Unanawa tu unamega tonge lako. Baba alifurahi zaidi. Alipokuwa hapa alikuwa hana rafiki. Hivyo, alinifanya mimi rafiki yake. Masikini nilipokwenda mara nyingine nilikuta amefariki dunia. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi!

Baada ya kula tukaanza safari kwenda nyumbani kwake. Baba ilikuwa ni ‘convoy.’ Mbele yetu yalitangulia magari matatu yaliyojaa askari wenye silaha za kivita. Nyuma yetu kulikuwa na msururu wa magari mengi zaidi yaliyojaa askari. Akalazimisha tukae katika gari moja. Kazad asante kwa kunijengea kumbukumbu itakayobaki katika kifua changu daima kwa mapokezi yale!

Nimeenda Kinshasa zaidi ya mara kumi. Safari ya kwanza sikumwambia mtu yeyote. Nilikaa huko wiki mbili nikila na kunywa vya kwao, mazao ya nchi ya DRC. Kwa mshangao mkubwa niliporudi Mbagala, nikakuta heshima yangu imepanda juu sana. Hata wengine bila kuwa na sababu wakaanza kuniogopa. Kumbe kuna mwanajeshi mmoja wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania mwenye cheo cha meja alikuwa katika kundi la wanajeshi waliopelekwa DRC kulinda amani. Aliniona huko akaja kusimulia hali aliyonikuta nayo. Ni jirani yangu na vikao vya jioni mara nyingi tunakuwa pamoja. Walipomuuliza mlipokutana huko mlisalimiana? Alijibu, “Kwa ulinzi aliokuwa nao ungepita wapi mpaka umfikie?’’ Huyu alikuwa meja, sijui hao walinzi wangu walikuwa na vyeo gani.

Nyumbani kwake, shughuli ya kukumbushana, vicheko, na furaha nyingi ikaanza! Ni zaidi ya miaka kumi imepita tangu haya yanitokee! Sijawahi kuyaandika popote. Mpaka nayasimulia hapa, baba, ujue nimeguswa sana na meseji ya Rais Tshisekedi.

Katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, “Kupanda mlima mkali kunahitaji kuanza na hatua za polepole. Njia yetu ya maisha sasa ni mwinuko mkali. Tukilielekezea jua macho yetu kamwe hatutaona kivuli. Hivyo lazima tuweke fikra zetu katika urari. Jana yetu imekwishapita, hivyo ni kesho yetu ndiyo inatuita kwa ishara. Hatuwezi kuibadili jana yetu lakini tunaweza kuiboresha kesho yetu. Tuiangalie kesho yetu kwa sababu huko ndiko tutakapomalizia maisha yetu!’’

Baba, meseji ya Rais Tshisekedi ilisema, “Tarehe 24 Januari mwaka huu, kulitokea jambo kubwa sana katika nchi yetu. Mimi nikiwa mpinzani tulipokezana madaraka ya kuongoza nchi yetu na Rais Joseph Kabila aliyekuwa madarakani, kwa amani kabisa.’’ Meseji fikirishi tunapoelekea Uchaguzi Mkuu 2020. Nilipofika DRC nilimkuta Tshiseked baba yake huyu Rais Felix akiwa kiongozi mpinzani mwenye nguvu kubwa. Kwa maridhiano leo wamepokezana madaraka kwa amani! Watanzania, nchi kwanza! Achaneni na tofauti zenu za kisiasa. Kuweni wamoja muilinde amani ya nchi yenu. Asiyetaka maridhiano kabla ya uchaguzi mkuu, hawafai! Awe ni mwenyekiti, diwani, mbunge au yeyote yule, amekengeuka! Hawafai, muogopeni! Mkataeni kwa kura zenu na Mwenyezi Mungu ambae hakuwaumba kwa bahati mbaya, atawapigania dhidi yake!

Tumeshindwa kujifunza hata busara ya Rais Uhuru Kenyatta kwa maridhiano na mpinzani wake mkubwa, Raila Odinga. Kenya sasa ni amani na maendeleo. Joseph Kabila na Uhuru Kenyatta wangeshindwa nini kuwa na watu wasiojulikana. Wanayajua majuto yake! Kuondoka Balozi wa Jumuiya ya Ulaya, Roeland van de Geer, tumeiongezea dunia mshambuliaji muhimu dhidi yetu! Ushahidi usiokamilika ni sawa na ushahidi usiokuwapo. Kuwaweka watu magerezani kwa muda mrefu kwa ushahidi usiokuwapo, dunia ina haki kutuhukumu kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Wameshindwa kupeleleza watumbue! Maendeleo hayahitaji kubembelezana, lakini tusiuvue utu wetu. Pia tuuheshimu na utu wa wengine. Ulipoulizwa pale Chuo Kikuu, Waziri Kabudi kwa heshima akaomba akujibie, akisema akikosea, umuwajibishe. Safi! Lakini mteule wako yeyote atakayekiri hadharani kuwa ulimtoa jalalani ukamweka hapo alipo ambako yeye anapaona ni sawa na peponi, hakufai hata kidogo! Hawezi kukushauri hata kama ungekosea vipi. Aliishakwambia kuwa haikuwa sahihi kijana masikini kushushiwa kipigo cha mbwa koko pale Makambako mbele yako baba yake? Bango la kuwaombea maji wananchi wake wasio na mbunge anayeweza kumhoji rais, liliwazidishia hofu waliojaa hofu ya uchaguzi mkuu, wakadhani ni mpinzani! Abarikiwe aliyeuliza, “Mjinga ni nani, ni Nyerere aliyesema vyama vingi ni lazima vitakuja au ni nyinyi msiotaka vyama vingi?’’

1107 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!