Ndugu Rais na haya ndiyo maombi ya watu wako

Ndugu Rais kwa jitihada zako binafsi wengi wameona nidhamu katika kazi imeanza kurejea. Utendaji kazi kwa baadhi ya viongozi katika awamu iliyopita ulikuwa ni wa hovyo sana! Wananchi wanaona leo unatumbua hapa, kesho unapalilia pale na ukiona vipi, unasema liwalo na liwe, unafukua kabisa kaburi lenyewe! Unahangaikia nchi yako! Mwenyezi akutangulie!
Kazi hii baba elewa kuwa unaifanya peke yako! Wengi walio karibu yako wako hapo kimwili tu. Shambani kwako kuna mazao mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi, mwombe Muumba wako, Bwana wa mavuno akupatie wafanyakazi wasio wanafiki. Wafanyakazi wajasiri walioiweka nchi kwanza na watu wake. Watu wenye ujasiri mkubwa ambao fikra zao na mawazo yao yako juu ya vyama vya siasa!
Wale walio na ukweli kutoka vifuani mwao ambao wanaweza kukushauri hata lile ambalo wanaamini Maulana atalipenda hata kama wanajua kwa ubinadamu tu unaweza usilifurahie sana! Watu hao Mungu katujalia, wapo! Wapo wengi tu katika hii! Mwanadamu kwa udhaifu wake mara nyingi hujikuta amekaa mbali nao!

Ndugu Rais, mtoto asipomfurahia baba yake, akacheka naye, hata akafanya utani naye hapa duniani, atafurahi na nani mwingine? Wape fursa wanao ya kukuheshimu, lakini wasikuogope! Wako baba wengine ambao pindi watokezapo nyumbani watoto hukosa amani. Baba hacheki na wanae hata kama ni Krismas au sikukuu ya Idi! Akiamua kusema nao, yeye ni kufokafoka tu mwaka mzima!
Ndiyo, wako watoto watundu, wakorofi hata wezi na wavuta bangi, lakini ndiyo wanao hao! Si ajabu wengine umewalazimisha mwenyewe wawe hivyo kutokana na ukaliukali wako wa kuwazuia wasifanye kila kitu! Kama hutaki kusema na wanao, wanapohitaji ushauri waupate kutoka kwa nani?

Wanaoruka ukuta si wote wanataka kufanya hivyo! Ni baada ya kufungiwa milango na madirisha. Huo ni ubaba wa bahati mbaya! Namwomba Mwenyezi Mungu aniepushe na mkosi wa ubaba kama huo!
Ndugu Rais, nina binti yangu ambaye tangu chekechea mpaka amehitimu kidato cha nne mwaka jana, alikuwa shule za kutwa. Anaondoka asubuhi kwenda shule, jioni anarudi nyumbani ingawaje shule zote zilikuwa na mabweni. Lengo langu lilikuwa ni kuhakikisha nafuatilia maendeleo ya masomo yake siku kwa siku huku nikiamini kuwa mwalimu mkuu wa kwanza wa mtoto yeyote ni wazazi wake! Mungu apewe sifa kwa kumjalia ufaulu wa divisheni ‘one’ ya alama 13.

Ndugu Rais Jumatatu ya tarehe 17-7-2017 mama yake na kaka yake
walimpeleka Ifakara huko Morogoro kuanza kidato cha tano. Waliniambia alikuwa mchangamfu na mwenye furaha njia nzima hata matroni wake alimpokea kwa furaha na akawa anamtolea mfano kwa wenzake kwa kuwa fomu zake za kujiunga na shule zilijazwa kwa usahihi kabisa.
Akinisimulia safari yao, mama yake aliniambia baada tu ya kumpa mkono wa kwaheri binti yangu alianza kumwaga machozi! Alipoulizwa unalia nini?
Binti yangu aliwajibu, “Nitammisi baba yangu!” Na mimi machozi, yalinitoka!
Ndugu Rais na wewe wafanye Watanzania wakumisi wanapokuwa hawakuoni au hawakusikii! Hujisikia faraja kutangulia kuliona jua miaka saba kabla ya Rais wangu; lakini baba katika nchi hii wako wazee wetu wengi wenye umri mkubwa wa kuweza kuwa hata babu zetu. Lakini wewe ndiye Rais wa nchi hii! Na kwa dhamana hiyo wewe ndiye baba yao na ndiye baba yetu sisi wote! Baba, tufanye na sisi tukumisi!
Inachosha kila siku kusikia watu walewale, leo wamewekwa mahabusu!

Kesho walewale wameitwa polisi kuhojiwa! Na kule kwingine walewale wanahukumiwa na baadhi ya mahakimu wasio heshimu taaluma yao! Inatia kichefuchefu kuona mtu yuleyule anafunguliwa kesi zaidi ya kumi na zote hakuna anayoshindwa! Inaleta picha ya uonevu na kukomoa katika nchi! Hali hii ikiachwa iendelee makubwa yote yanayofanywa yatapoteza maana kwa sababu ubaya huvuma zaidi kuliko wema. Yawezekana kuna wanafiki hawasemi ukweli kuwa hapa hapana kosa la kumshtaki mtu!
Wanataka wananchi wakuoneje? Baba, tufanye na sisi tukumisi!
Turudishie umoja wetu! Turudishie utaifa wetu! Turudishie undugu wetu nasi tutakumisi!
Lakini ndugu Rais, wakati mwingine na wewe baba una mikwara mizito!
Ulipomwambia Mkuu wa Polisi (IGP) aliyepita kuwa, “Nasikia ulipigiwa simu nyingi sana ukitakiwa uwaachie waliokuwa wamekamatwa kwa tuhuma za madawa ya kulevya. Nakupongeza sana hukuwasikiliza. Ungewasikiliza, nadhani hata wewe leo usingekuwa hapa!”

Zamani watoto wa mjini wangesema kamba za baba ni za kufungia meli! Kwani zilipita siku nyingi! Leo hata hatujui IGP aliyepita yuko wapi! Huyu aliyemrithi, siku hiyo alikuwapo. Katika hali kama hii atatenda kazi kwa nidhamu au kwa hofu na woga? Nidhamu ya kazi na woga au hofu katika kazi ni vitu tofauti, lakini vinafanana sana kitabia! Wengi wanashindwa kuvitofautisha. Mwenye nidhamu ya kazi na mwenye hofu ya kazi yake, tabia zao ni zile zile kwa kazi zao.

Ndugu Rais, hata hivyo Watanzania lazima wakushukuru kwa kuwapatia IGP mpya. Mwanamwema huyu, huko alikotokea ameonyesha pasipo kuacha shaka, hofu yake aliyonayo juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu! Hata katika kipindi chake kigumu pale alipozushiwa tuhuma nzito tena hadharani mbele ya Waziri Mkuu kuwa alipokea rushwa kutoka kwa wauza shisha, bado hakuufungua moyo wake kuonyesha maumivu aliyoyapata! Kwa hakika kwa hili alionyesha ujasiri mkubwa. Na kama isingekuwa busara kubwa alioionyesha Waziri Mkuu wetu siku hiyo, huenda na yeye leo asingekuwa hapa! Ah! Nyongo mkaa na ini!
Ndugu Rais, ni matarajio ya walio wengi kuwa kwa ukomavu aliouonyesha, IGP mpya atakuwa msaada mkubwa kwako. Kijana mwema ni yule anayekuwa mwepesi kufukia mashimo anayofukua bosi wake katika jamii kwa bahati mbaya! Nawe ukiwa ndiyo nguvu ya baba itumie kwa weledi, busara na hekima ili utuunganishe wana wake katika upendo, umoja na mshikamano kama Taifa moja, ili siku moja na sisi tuje tujisikie kummisi baba yetu!

PASCHALLY MAYEGA
SIMU: 0713 334 239