Ndugu Rais, naiona kesho yetu iliyopangwa na Baba. Kesho ya heshima iliyopangwa na Baba. Kesho ya neema, kesho yetu ya ushindi liyopangwa na Mungu. Sitaki kuitazama leo yetu. Leo yetu ni ya shida. Kuna majira hufika mambo yakawa magumu. Hata tukisukwasukwa vipi kamwe tusimuache Baba kwa kuwa kasema tuione kesho yetu aliyotuwekea.
Hata kwa macho ya nyama tu utaona ni kiasi gani Watanzania wamechoka. Lakini amesema tuitazame kesho iliyo njema iliyopangwa na Baba.
Miaka mitano inapita kwa kasi kama maji ya mto huku bei ya mafuta nayo ikizidi kupanda kwa kasi vilevile. Na sasa imefikia kiwango kinachoumiza sana. Unapopandisha bei ya mafuta unapandisha bei ya kila kitu. Maisha ya Mtanzania ni magumu zaidi. Katika hali kama hii kusimama hadharani na kusema kuna maendeleo kunahitaji moyo mpana. Jasiri peke yake analiweza hili.
Wakati tunasifia mambo makubwa mwanamwema Charles kutoka Pugu, Dar es Salaam aliandika ujumbe ufuatao, “Wasomaji wa JAMHURI hamjambo. Leo nimempeleka mwanangu Chanika Hospital. Aliumia mbavuni wakicheza na wenzake. Huduma ya X-ray, bomba la sindano na baadhi ya dawa hakuna. Jamani hizi SIFA!’’
Baba wa Taifa alisema, “Tulipoanza tulifanya ujinga kuingalia North America na Europe, tulipoyaona maghorofa, ndege na reli zao tukadhani hayo ndiyo maendeleo’’. Baba wa Taifa anasema walifanya ujinga.
Tunapodhani tunafanya mambo makubwa lazima tuweke katika fahamu zetu kuwa maendeleo ya kweli lazima yalenge watu. Na yawalenge watu katika nyanja za afya, elimu na ustawi. Kukimbilia kusema eti kuna watu huko duniani wanatuonea wivu kunaweza kuwafanya wengine wasione upana wa fikra zetu. Tanzania siyo kisiwa.
Katika mitandao ya kidunia zipo habari kuwa Rais wa Benki ya Dunia, Bwana Kim, akijibu swali aliloulizwa na msikilizaji wake alisema, pamoja na kuzuiwa na mikataba yao mbalimbali inayowataka wasiingilie mambo ya nchi, lakini yako mambo yanahitaji majadiliano. Akasema, “Acha niseme bila kuficha kitu, kuwa tunafadhaishwa, sana na baadhi ya mambo yanayotokea Tanzania. Kuna mambo yanatokea ambayo yanatusikitisha sana. Na tumejiweka wazi kuwa hatuwezi kuendelea kuyavumilia.’’
Sisi tunasema kirahisi tu kuwa wanatuonea wivu. Siyo lazima tuzagae katika kila pembe ya dunia kama tulivyozoea zamani, lakini kujua yanayosemwa na dunia juu yetu sisi ni muhimu sana.
Tungekuwa na Azimio la Arusha kiu ya katiba mpya ingekuwapo, lakini isingekuwa ya kuumiza kama inavyoumiza sasa. Baadhi ya wenzetu wamegangamara hawataki kusikia cha Azimio la Arusha wala cha katiba mpya. Wanashangaza wanapoendelea kulitaja jina la Mwenyezi Mungu hadharani. Walioungana kuliua Azimio la Arusha ndio hao hao waliungana kutaka katiba mpya isiwe, lakini sasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu fukuto limeanza kuwatafuna wenyewe. Wanaparurana hadharani kwa uroho wa madaraka. Wasiyonayo wanayataka huku waliyonayo wanayang’ang’ania madaraka waliyonayo.
Maendeleo ya watu yatatoka wapi? Yawezekana wanaosema sasa kuwa maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa mageuzi ya kweli yangepatikana kama CCM ingemeguka na kuwa vipande viwili wakawa na fikra sahihi kuwa sasa yanatimia! Lakini wa kuratibu mpasuko huu atakuwa nani? Mparurano huu ndiyo utakaotoa mwelekeo wa Tanzania ijayo.
Wenzetu wa Kenya walikuwa na KANU yenye nguvu. Ilipasuka. Imekwisha kwenda. Leo Kenya kuna Jubilee na NASA. Kwa pamoja wanaijenga Kenya yao na wananchi wa Kenya. Wakenya sasa wanajua kuwa Kenya ni nchi yao wote katika umoja wao na kwa usawa.
Wakati wenzetu Wakenya wanaziondoa tofauti zao, sisi hapa kuna watu wanazipalilia. Sijui nani katuletea mkosi huu katika nchi yetu.
Naiona kesho yetu. Kesho iliyojaa upendo. Kesho yenye matumaini mapya. Kesho angavu. Kesho ya Watanzania wenye umoja na mshikamano waliojaa furaha. Sitaki kuitazama leo yetu. Leo yetu ni ya shida. Imejaa hofu!
Imejaa utetemeshi. Leo yetu imefunikwa na kivuli cha umauti. Wananchi wamegawanywa katika makundi ili watawaliwe badala ya kuongozwa. Hawa wanaabudu vyama vyao. Wamesahau kuwa nchi ni moja na ni yao wote waliopewa na Muumba wao katika umoja wao.
Wakati mafundisho ya dini zote yanaelekeza kuwapenda jirani zetu wenye imani haba ya dini zao wanaamini kuwa uzalendo lazima uanzie nyumbani. Imani ya umimi
haijawahi kuistawisha jamii yoyote, bali kuiparaganyisha.
Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu Muumba wetu atuongoze tumchague kiongozi wa kutuongoza ili atuunganishe tuishi kwa furaha katika nchi yetu kama tulivyokuwa zamani. Wakutaka kututawala hatufai. Wanaoanza kuonyesha uchu wa madaraka sasa hawatufai, tuwaache waendelee kuparurana, lakini tusiwachague.
Mwaka 2020 tukamchague mtu siyo chama chake. Mtu atakayekuwa na ufahamu wa kutambua kuwa atakuwa mtumishi wa wananchi wote kutoka katika kifua chake siyo kutoka mdomoni. Kiongozi atakayewatanguliza Watanzania mbele. Atakayetambua kuwa kiu ya wananchi ndiyo kiu ya nchi hivyo kuibeza ni kosa kubwa.
Ndugu Rais, duniani hakuna rais nusu. Rais ni rais tu kama ilivyo hela. Hela ni hela tofauti yake iko katika uthamani wake. Kuna shilingi mia na kuna senti hamsini – zote ni hela.
Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa Rais wetu alituambia kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa sawa na Mlima Kilimanjaro huku yeye akijifananisha na kichuguu. Unyenyekevu ni kati ya sifa zinazomwonyesha mtu anayeamini katika uwepo wa Mwenyezi Mungu. Kama Rais Mwinyi alikuwa na haki ya kusema hivyo, basi akija kutokea rais mwingine akasema kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa sawa na Mlima Kilimanjaro huku yeye akijifananisha na Mlima Everest, mlima mrefu zaidi duniani, naye atakuwa sawa kusema hivyo. Mungu atuepushe na huko kwa kuwa kiburi na umimi ni sifa zinazomtambulisha shetani. Naiona kesho yangu.
Kama Nyerere aliona ni sawa Stigler’s Gorge iwe sehemu ya urithi wa dunia huku sisi tunataka kuibomoa ni sawa. Tofauti ni katika uthamani wetu. Wakati Nyerere akiombewa kwa hili atangazwe kuwa mtakatifu makaburi yetu yanaweza kuja kufukuliwa wananchi wapate kuyahakiki mafuvu yetu. Wosia wa Baba Askofu Everist Chengula kuwa tumtathimini mtu kabla ya kumchagua lazima uzingatiwe.