Katibu Mtendaji wa NEEC Bw. Jabiri Makame amefanya kikao kazi cha mwelekeo wa NEEC katika utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Dira 2050.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Idara, Vitengo na Sehemu wa Taasisi kwa lengo la kuangalia ni namna gani Taasisi inavyoweza kufanya kazi kwa kasi na Ufanisi zaidi katika kuisimamia na kutekeleza Sera na kuyafikia malengo ya Dira 2050.
Kikao hicho kimefanyika katika hoteli ya SANAAN Mkoani Dodoma ambapo wajumbe walipata fursa ya kuwasilisha taarifa zao mbele ya Katibu Mtendaji na kujadiliwa kwa pamoja.
Kikao pia kililenga kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu , na kufahamu mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Taasisi lakini pia kufahamu changamoto zilizopo katika kutekeleza majukumu na kuzipatia utatuzi kwa namna moja ama nyingine.
Baada ya mawasilisho tofauti yaliyofuatiwa na mijadala baina ya wajumbe, Katibu Mtendaji aliwataka wajumbe kuyafanyia kazi yale yote yaliyojadiliwa lakini pia kuupokea ushauri uliotolewa na wajumbe na kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya sita ili kumsaidia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuifikia Dira 2050.
“Lengo ni kuifanya Taasisi ikuwe kwa namna moja au nyingine, idara moja ikifanikiwa kwa namna moja au nyingine ina maana kuwa Taasisi nayo itakuwa imepiga hatua” aliongeza Katibu Mtendaji.
Katibu Mtendaji aliwataka wajumbe kuona namna ya kuifanyia Tathmini Sera ya Uwezeshaji Kiuchumi ya mwaka 2004 kuona kama kuna kuna haja ya kuifanyia mapitio ili iendane na Dira 2050.
“Niwaombe wote tuisimamie Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Kiuchumi ili kuhakikisha Watanzania wanainuka Kiuchumi lakini pia wananufaika na Uchumi na Uwekezaji uliopo nchini bila kukiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi” alisisitiza Katibu Mtendaji.
Sambamba na yote Kikao pia kiliazimia kuwashirikisha wadau wote wa Uwezeshaji nchini ikiwemo Wizara, Idara, Wakala, Mamlaka Mashirika binafsi, Asasi za Kiraia, Makampuni na sekta nyingine mtambuka ili kuhakikisha Uchumi wa Watanzania unaimarika.



