Rais wa U.S Donald Trump anatarajiwa kukamilisha pendekezo la mpango wa amani wa Gaza anapokutana Jumatatu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, huku Israel ikizidi kuishambulia Gaza City.
Tawi hilo la kijeshi la Hamas kupitia Brigedi zake za Al-Qassam limewatolea wito wanajeshi wa Israel jana Jumapili kuondoka na kusitisha mashambulizi huko Gaza City kwa angalau masaa 24 ili wanamgambo hao wapate nafasi ya kuwasaka mateka hao ambao hatima yao inaweza kuibua kiwingu kwenye mkutano huu wa leo kati ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais Trump.
Trump ameliambia shirika la habari la Reuters kupitia mahojiano kwa njia ya simu kwamba amepata mwitikio mzuri mno kutoka Israel na kwa viongozi wa mataifa ya Kiarabu kuelekea pendekezo la mpango wa amani wa Gaza na kwa maana hiyo ni dhahiri kwamba kila mmoja sasa anataka kufikia makubaliano.
Kundi la Hamas hata hivyo limesema halijapata bado pendekezo lolote ama kutoka kwa Trump au kwa wasuluhishi.
Israel ilianzisha mashambulizi makubwa ya ardhini huko Gaza City ikiangusha majengo na kuwaagiza maelfu ya wakaazi kuondoka katika kile ambacho Netanyahu anasema ni jaribio la kuliangamiza kundi la Hamas. Lakini hata hivyo, katika siku chache zilizopita kumeshuhudiwa kuongezeka kwa mazungumzo ya suluhu ya kidiplomasia katika vita hivyo vilivyodumu kwa karibu miaka miwili sasa.
