Leo nitawapitisha wajasiriamali katika somo muhimu kuhusu rangi. Je, unafahamu chimbuko la neno yeboyebo hapa nchini? Twende pamoja.


Miaka michache iliyopita, kampuni moja ya hapa Tanzania ilitambulisha bidhaa zake za juisi zilizokuwa zikifahamika kama “Yebo”. Juhudi kubwa ilielekezwa katika kuitangaza kwa watumiaji.


Juisi ile ilikuwa ni ya rangi ya njano na katika matangazo ya kwenye televisheni walitumika watu waliovaa kandambili za plastiki zenye rangi ya njano. Kwa kuwa kandambili hizo ndiyo kwanza zilikuwa zinaingia sokoni zikabatizwa jina la yebo yebo.


Haikuishia hapo, neno ‘yebo yebo’ likawa linatumika kwa kila kilichoonekana kutumia ama kuwa na rangi ya njano. Timu ya mpira ya Yanga ilikuwa miongoni mwa waathirika wa hali hiyo kwani ilibatizwa jina la Yebo yebo!


Yebo yebo ikajipatia urasmi wa ‘kiaina’ kutumika kumaanisha kitu kinachopatikana kwa wingi, kisicho na thamani kubwa na kinachodharaulika. Sina uhakika kampuni husika ilichukua hatua gani baada ya hapo kujisalimisha na hatari ya bidhaa zao kuchukuliwa ‘poa’ kutokana na matangazo waliyobuni.


Ukifuatilia maarifa katika sayansi ya biashara utabaini kuwa kuzuka kwa neno ‘yebo yebo’ hakukuwa katika kandambili za plastiki wala neno hilo halikuwa katika ubora wa bidhaa (kwa maana ya juisi yenyewe ukitoa ufungashaji), bali tatizo lilianzia katika rangi ya njano. Rangi ya njano ilipelekea kuzaliwa kwa dhana ya u-yebo yebo kutokana na namna inavyotafsiriwa katika ubongo wa mtu.


Unapoona bidhaa yoyote ikiwa imefungashiwa kwa rangi za aina fulani, basi ujue hilo halifanyiki kwa bahati mbaya bali linabeba maana kwa mtumiaji hata kama mtumiaji hajijui kwa nini anatumia bidhaa za rangi fulani na asitumie za rangi nyingine.


Ukiangalia soda ya ‘Seven Up’ kutoka kampuni ya Pepsi, pamoja na soda ya Sprite kutoka kampuni ya Coca Cola, utaona kuwa soda hizi zina rangi nyeupe lakini zinafungashwa katika chupa za kijani, kwa nini?


Katika nchi nyingi maskini ikiwemo Tanzania, kampuni na wajasiriamali wengi wamekuwa hawatilii mkazo suala la rangi katika biashara zao. Hii inajumuisha bidhaa, mazingira ya huduma pamoja na rangi zitumikazo katika majengo ya kuzitengeneza. Kupuuza suala la umuhimu wa rangi katika biashara kumepelekea wafanyabiashara na kampuni nyingi kushindwa kukubalika kwa baadhi ya watumiaji.


Si kila rangi inafaa kupakwa katika kuta za duka wala kutumika kuandika maandishi kwenye vifungashio vya bidhaa. Umakini wa kuzingatia athari za rangi miongoni mwa watumiaji kunatajwa kuwa ni moja ya sababu za bidhaa kutoka nje ya Tanzania kupendwa ukilinganishwa na za hapa nyumbani.


Kimsingi rangi zimethibitishwa kuwa na uwezo wa kushawishi saikolojia na tabia za watu.

 

Mtaalamu wa saikolojia, Ward, aliwahi kuulizwa njia za kuwezesha wafanyakazi kupunguza misongo wakiwa kazini.  Alijibu, “Haihitaji semina wala mafunzo, jambo la msingi ni kupaka rangi sahihi katika kuta za vyumba wanamofanyia kazi, ambayo itaweka hamasiko ama mfifio kwa mabadiliko yanayohitajika.”


Kwa mujibu wa mtafiti mwingine wa mambo ya biashara katika masoko, Wexner, rangi nyekundu kwa mfano inatajwa kuwa inaambatana na hisia za kuhamasika, machungwa inaambatana na kukatishwa tamaa na kudharauliwa. Zambarau inaonesha hali ya kuthaminiwa, njano inawakilisha hali ya furaha, mzaha na kicheko na nyeusi inaonesha nguvu, umiliki na uimara.


Makampuni na biashara mbalimbali duniani, kila siku zinakazana kutafuta njia za kuwezesha mwonekano na nguvu za nembo zao. Njia thabiti zinapovumbuliwa mikakati ya kimasoko huwekwa kuhakikisha nembo hizo zinakuwa katika akili na fikra za wateja.


Tofauti za kiutamaduni, kiuchumi, kijamii na nyinginezo zinaleta changamoto ya ugumu kwa biashara na kampuni kufahamu kwa usahihi aina moja ya nembo ambayo itawaridhisha na kuwapendezesha wateja wote.


Hivyo biashara nyingi hasa za kimataifa zinajikuta kuwa zinalazimika kuwa na nembo moja katika miundo tofauti kufanikisha ufikaji wa bidhaa kama ilivyokusudiwa.

 

Mbinu mmojawapo ya kimasoko inayotumika na waendesha masoko, hasa kimataifa bila kujali eneo ama watu watakaotumia bidhaa hizo ni rangi. Rangi ni moja ya vifaa ambavyo mameneja masoko hutumia katika kutengeneza, kuimarisha na kurekebisha mwonekano wa nembo katika ufahamu wa mteja. Umuhimu wa rangi kuwasilisha maana fulani kwa walengwa kunathibitishwa hata katika taratibu na sheria mbalimbali duniani.

 

Kwa mfano, nchini Marekani kuna sheria inayofahamika kama ‘Lanham Act’ inayolinda rangi za bidhaa kama nembo halali za kibiashara. Rangi zinafahamika kuwa zinabeba chembechembe za kihisia na kisaikolojia.

 

Maana zinazoambatana na rangi tofauti zina umaana mkubwa kwa watu wanaohusika na masoko katika bidhaa ama huduma za kampuni mbalimbali kwa sababu mbinu za kutangaza bidhaa ndizo huamua ukubalikaji wa bidhaa yenyewe.

 

Kwa mfano, ua la waridi (rose) litabaki kuwa hivyo katika mataifa na tamaduni mbalimbali, lakini rangi za maua hayo zinakuwa na maana tofauti kutoka utamaduni, taifa moja kwenda jingine. Wajapani wanapendelea maua hayo yenye rangi nyeupe wakati watumiaji kutoka Hong Kong wanapendelea kutumia maua hayo ya rangi nyekundu.


Mtu anapotaka kununua gari, rangi inatajwa na wataalamu wa masuala ya biashara kuwa inashika nafasi ya tatu katika orodha ya vigezo vya bei na ubora. Rangi pia ina umuhimu mkubwa sana katika ujenzi wa nembo ikiwemo logo, ufungaji na uoneshaji.

 

Mtaalamu na mtafiti wa mambo ya masoko, Wagner, kupitia taasisi yake ya utafiti wa uhusiano wa rangi na biashara, ijulikanayo kama ‘Wagner Color Research Institute’, alijaribu kuthibitisha dhana yake  maarufu, ‘Colors are associated with certain images’ (rangi inaambatana na taswira fulani). Wagner alitumia kampuni inayoendesha migahawa iitwayo: Wiener schnitzel, yenye matawi zaidi ya 350 nchini Marekani.

 

Wagner aliishauri kampuni hii kuongeza rangi ya njano kidogo katika rangi zinazopamba majengo ya migahawa yao, ili kuwasilisha ujumbe kuwa kampuni hiyo kupitia matawi yake inauza vyakula vya bei rahisi. Baada ya kubadilisha rangi, kampuni hiyo iliripoti ongezeko la mauzo kwa asilimia saba.


Kwa ujumla rangi zinaambatana na taswira fulani kila zinapoonekana na kufikiriwa katika fikra za mteja. Kwa mfano, rangi ya bluu mahali pengi huambatana na maana na taswira ya utajiri, uaminifu na usalama. Ndiyo maana ukifuatilia kwa umakini utagundua kuwa benki nyingi zinapenda kutumia ama kujumuisha rangi ya bluu katika nembo na machapisho yao.

 

Hii inaingiza taswira miongoni mwa wateja kuwa benki ipo imara (utajiri mkubwa), ina uamininifu (hivyo akaunti zake haziwezi kufanyiwa hujuma) na usalama (kimbilio sahihi la kutunza hazina zake). Wakati rangi ya njano inabeba mwonekano wa kitu cha bei rahisi.

 

Wasimamizi wa masuala ya masoko katika kampuni na biashara wanapaswa kufahamu maana tofauti zinazoambatana na rangi, ambapo maana hizo zitawezesha kugawanya na kupoka fursa mbalimbali za kimasoko kwenye jamii na tamaduni mbalimbali. Muunganiko wa rangi katika kufungasha bidhaa nao una umuhimu mkubwa ili kuwateka wateja.

 

Upo mfano mwingine wa kampuni ya kutengeneza vifaa vya kompyuta ya Apple, kupitia bidhaa zake za iMac, inafungasha kutumia muunganiko wa rangi tano ambazo zina maana tofauti katika mataifa mbalimbali.  Rangi hizo ni kijani, dhahabu, nyeupe, bluu na njano.

 

Bidhaa za iMac zinapoingia Taiwan zinatafsiriwa kuwa ni amani, rafiki (kijani), zisizo na madhara (bluu na nyeupe), endelevu (dhahabu), zinazosisimua, zinazofanya kazi kwa haraka na kwa ufanisi (njano).

 

Muunganiko huo wa rangi unapoingia China tafsiri inakuwa ni nyingine kabisa, lakini bado tafsiri inaisaidia na kuiwezesha kampuni kuuza bidhaa zake vizuri. Kule China bidhaa za iMac huleta maana ya; amani (kijani), nzuri na zinazoleta urembo (njano) wakati nyeupe huwakilisha vitu vilivyo katika mpangilio na vinavyofafanulika.

 

Kuna changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wa Tanzania hasa katika wakati huu ambao tupo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Namna bidhaa zetu zinavyotengenezwa na kufungashwa zinaamua jinsi zinavyoweza kushindana katika masoko ya kimataifa.


Hata wafanyabiashara wadogo wadogo katika maduka na vibanda vyao, ni vema wakawa na ufahamu wa namna ya kupaka rangi zitakazowavutia wateja na kuongeza uhakika wa kushinda changamoto za kiushindani!

[email protected], 0719 127 901.

By Jamhuri