Home Makala NINA NDOTO (29)

NINA NDOTO (29)

by Jamhuri

Kufanana ndoto si kufana matendo

 

Watu wawili kuwa na ndoto moja haimaanishi kuwa kila watakachofanya kitafanana. Kuna aliyewahi kuimba akisema, “Hata vidole havilingani”. Vyote ni vidole, lakini vinatofautiana kwa urefu.

Hata watu ambao tunawaita mapacha wanaofanana bado kuna vitu wanatofautiana. Ndoto yaweza kufanana na ya mtu mwingine, lakini mwishowe wakafanya mambo tofauti na pia wakawa na matokeo tofauti.

Wakati Farao anaota ndoto kuna watu wengi walikuwa nauwezo wa kutafsiri, lakini wote walishindwa isipokuwa Yusufu. Kufanana kwa ndoto si kufanana kwa matendo.

Unaweza kuwa na ndoto ya kuwa kiongozi mkubwa, lakini haimaanishi ukiwa kiongozi uige staili fulani ya  mtu fulani anavyoongoza. Kila mtu ana kitu maalumu ambacho Mungu amekiweka ndani yake kitakachomfanya aonekane wa thamani katika dunia hii.

Unapokuwa na ndoto  ambayo inafanana na ya watu wengine siku zote kumbukakuwa ndani yako kuna utofauti umeubeba ambao yakupasa uuonyeshe. Bila kufanya hivyo tambua kuwa kiwango chako cha mafanikio kitakuwa kidogo.

Adolf na Rudolf Dassler ni ndugu wawili wa damu waliokuwa na ndoto ya kuwa na kampuni kubwa ya kutengeneza viatu. Walianzisha kampuni  miaka ya 1920. Baada ya Vita ya Pili ya Dunia ndugu hawa  walikuwa na ugomvi ambao haufahamiki nini chanzo chake (Ingawa wengi wansema ni mawasiliano mabovu).

Ugomvi huo ulisababisha kuwapo  mpasuko mkubwa katika kampuni, lakini kila mtu alikuwa na ndoto na nia ya kutengeneza viatu. Hawakuwa na njia nyingine isipokuwa kila mmoja  akaanzisha kampuni yake.

Adolf ambaye alipenda sana kuitwa Adi aliipa jina la biashara yake –Adidas akiunganisha jina lake la kwanza na la pili, Rudolf alijaribu hivyo pia kama alivyojiita ndugu yake na kujipa jina Ruda ambalo baadaye lilibadilishwa na kuwa Puma.

Leo hii tukizungumzia kampuni za Puma na Adidas tunazungumzia kampuni kubwa sana duniani ambazo zinatengeneza viatu. Viatu vinavyotengenezwa na Puma havifanani na vile vinavyotengenezwa na Adidas. Ndoto za ndugu hawa wawili zilifanana, lakini walitoa matokeo tofauti kwa maana ya kutengeneza viatu visivyofanana.

Katika historia hii jambo la kushangaza zaidi ni kwamba wakati ndugu hawa wawili wametengana viwanda vyao vilikuwa vikitazamana, lakini bado walitengeneza bidhaa  zinazotofautiana.

Leo hii Adidas na Puma wameliteka soko la michezo ingawa wanazalisha viatu vya aina nyingine pia.

Utofauti wa unachokifanya ndicho kitakachokufanya ubaki sokoni muda mrefu. Tumeona kampuni hizi zimedumu miaka zaidi ya 70.

Njia nzuri ya kuwa na ndoto yenye matendo ya tofauti ni kuwa bora, kama anavyosema mchekeshaji Steve Martin, “Kuwa bora kiasi kwamba hawawezi kukuchulia poa.”

Unapokuwa bora watu watakusikiliza, watu watakufuatilia, watu watapenda bidhaa zako, watakutaja  wengine ili nao waje kutazama kile unachokifanya (hakuna tangazo zuri kama tangazo la watu kukutaja kwa wengine).

Kuna watu walikuwa wanajua kukaanga kuku, lakini Colonel Sanders alijua kuwakaanga kuku kwa ubora wa hali ya juu. Leo hii kuna KFC kila kona ya dunia.

Ukiona ndoto yako inafanana na ya watu wengine jua kwamba hiyo ni honi ya wewe kuongeza ubora wa kile unachokifanya.

Njia nyingine ya kuwa na matendo tofauti pale ndoto zinapofanana ni kutazama kile ambacho wengine hawafanyi. Tommy Berry anasema, “Ikiwa unataka kuishi maisha ya kushangaza, jua mambo ambayo watu wa kawaida hufanya na usiyafanye”.

Naye mwandishi Zig Ziglar anasema, “Hakuna msongamano kwenye maili ya ziada.”

Utofauti wako utakuja pale utakapokwenda hatua ya ziad, ipo wazi kuwa watu wengi hawataki kufanya zaidi ya walipofikia, ukipiga hatua moja usisimame – piga hatua zaidi. Usipumbazwe na mafanikio ya jana, piga hatua zaidi kila iitwapo leo.

Samuel Moore Walton (Sam Walton) alikuwa  mjasiriamali wa Amerika ambaye alianzisha stoo za Wal-Mart zilizokuwa zikiuza bidhaa mbalimbali. Mojawapo ya kitu muhimu na cha kipekee ambacho alikifanya ni kwamba siku za wikiendi alikwenda kununua bidhaa kwenye stoo za jirani na za kwake na kutazama walivyouza kuanzia bei hadi huduma ilivyotolewa.

Aliporudi kwenye biashara yake aliboresha zaidi, hii ilimmfanya awe mtu tajiri zaidi duniani mwaka 1985.

You may also like