Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Singida
Benki ya NMB imetunukiwa tuzo tano muhimu kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) katika Maadhimisho ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi kwa mwaka 2025, hatua inayodhihirisha juhudi za benki hiyo katika kuhakikisha mazingira salama na yenye afya kwa wafanyakazi wake.
Katika hafla hiyo iliyofanyika mkoani Singida, NMB ilitambuliwa kama Kampuni Bora kwenye Sekta ya Fedha na Bima kupitia Makao Makuu yake kwa kupata Tuzo ya Kwanza, na pia kutwaa Tuzo ya Pili kupitia Kanda ya Kati. Benki hiyo ilipata pia Tuzo ya Tatu kama Mshiriki Bora wa Maonesho ya OSHA, pamoja na Tuzo nyingine ya Tatu kwa kuwa Kampuni Iliyoibeba Vizuri Kaulimbiu ya Mwaka. Aidha, NMB ilipokea Tuzo Maalum ya Kutambuliwa kwa Mchango wake katika kufanikisha Maonesho ya OSHA 2025.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, ambaye aliipongeza NMB pamoja na taasisi na makampuni mengine yaliyoshiriki. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Kikwete alisema kuwa Serikali itaendelea kuthamini na kuboresha mfumo wa utoaji tuzo za OSHA ili kuhamasisha uboreshaji wa usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.
Aidha, alizishukuru taasisi na kampuni zote zilizojitokeza kushiriki, akisisitiza kuwa ushiriki wao unaonesha utayari wa kupitia ukaguzi wa OSHA kama sehemu ya kuhakikisha viwango vya usalama na afya kazini vinazingatiwa.
Benki ya NMB iliwakilishwa na Meneja Mwandamizi wa Usalama Mahala pa Kazi, Abamwesiga Beneth, aliyefuatana na baadhi ya wafanyakazi kutoka matawi mbalimbali ya benki hiyo. Ushiriki na ushindi wa tuzo hizi ni ishara ya dhamira ya benki katika kuendeleza ustawi wa wafanyakazi wake na kuimarisha utamaduni wa usalama kazini.







