Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Arusha

Serikali ya Norway imeipongeza Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga – World Vegetable Centre (WorldVeg), Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, iliyopo Tengeru, mkoani Arusha kwa kazi kubwa ya utafiti na uhifadhi wa mbegu za mbogamboga za asili ya Afrika ili kukuza sekta ya kilimo barani Afrika.

Pongezi hizo zimetolewa na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Tone Tinnes Alhamisi, wakati alipotembelea kituo hicho Alhamisi kwa ajili ya kushuhudia hafla ya usafirishaji wa mbegu kwenda kwenye Hifadhi ya Kimataifa ya Mbegu ya Svalbard iliyopo nchini Norway.

Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bi. Tone Tinnes, (katikati) akionyeshwa mojawapo ya aina ya mbegu ya mbogamboga ambayo ni miongoni mwa mbegu itakayosafirishwa, kwenda Hifadhi ya Kimataifa ya Mbegu ya Svalbard nchini Norway, wakati wa hafla fupi ya usafirishaji wa mbegu kutoka kwenye Taasisi hiyo iliyofanyika jana Tengeru mkoani Arusha. Wapili kushoto ni  Meneja wa Programu Tanzania  wa WorldVeg, Bi. Colleta Ndunguru, na kulia ni mtafiti na Mtaalamu wa uzalishaji na Uhifadhi mbogamboga asili, Dkt. Sognigbe N’Danikou.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Balozi Tinnes alisema kuwa serikali ya Norway kupitia Shirika lake la Maendeleo la NORAD, inajivunia kuwa sehemu ya wadau wanaofadhili jitihada hizo za kuhifadhi urithi wa kilimo cha mbogamboga barani Afrika.

“Hii ni hatua kubwa sana katika kulinda na kuhifadhi urithi wa mbogamboga asilia za Kiafrika. Mbegu hizi ni muhimu kwa usalama wa chakula kwa vizazi vijavyo,” alisema Balozi Tinnes.

Alisifu mchango wa mradi huo katika kuimarisha usalama wa chakula na lishe, uundaji wa ajira, pamoja na kuwawezesha wanawake na vijana nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Kupitia mradi huu, angalau sampuli 3,000 za mbegu kutoka Tanzania zitahifadhiwa kwa usalama katika benki hiyo ya uhifadhi mbegu ya Svalbard ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025.

Meneja wa Programu WorldVeg (Tanzania) , Bi Colleta Ndunguru, alisema kuwa kituo hicho pia kinakusudia kusambaza takriban pakiti 1,000 za mbegu kila mwaka kwa wakulima wadogo waliopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ili kuwawezesha kupata mazao yenye lishe na yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya kuboresha lishe na kipato chao.

Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bi. Tone Tinnes, (katikati) akifunga moja ya sanduku lililohifadhia mbegu za mbogamboga wakati wa hafla fupi ya usafirishaji wa mbegu kutoka kwenye Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable Centre) kulia kwake ni Meneja wa Programu Tanzania  wa WorldVeg, Bi. Colleta Ndunguru, na kushoto kwake ni Mtaalamu wa uzalishaji na Uhifadhi mbogamboga asili, Dkt. Sognigbe N’Danikou. Iliyofanyika jana, Tengeru mkoani Arusha.


Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na kuendeleza ubunifu katika utafiti wa mbogamboga ili kukuza kilimo barani Afrika.

Mradi wa dola za Kimarekani 660,000 unaoongozwa na WorldVeg unalenga kulinda urithi wa mimea ya mbogamboga barani Afrika, kwa kuhakikisha kwamba mazao yenye lishe na yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi yanahifadhiwa na kupatikana kwa vizazi vijavyo.

Usafirishaji wa mbegu hizo ni sehemu ya mradi unaojulikana kama ‘Kuokoa, Kuhifadhi na Kutumia Urithi wa Mboga za Kiafrika’, ambao unatekelezwa kwa ushirikiano wa kimataifa kupitia Mkataba wa Kimataifa wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) kuhusu Rasilimali za Mimea kwa Chakula na Kilimo (ITPGRFA).

Taasisi ya WorldVeg imefanikiwa kukusanya na kuhifadhi aina zaidi ya mbegu 10,500 za mboga mboga, nyingi zikiwa ni za asili ya Kiafrika na nyingine kutoka maeneo mengine duniani.

Mbegu hizo ni matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa ndani na nje ya nchi kwa muda mrefu katika kituo hicho cha Arusha.

Mtaalamu wa uzalishaji na uhifadhi wa mbogamboga za asili kutoka WorldVeg, Dkt. Sognigbe N’Danikou, alisema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano baina ya taasisi, vyuo vikuu, watafiti na jamii za wakulima wa maeneo mbalimbali.

Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bi. Tone Tinnes, (kulia) akizungumza na Meneja wa Programu Tanzania wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable Centre) , Bi. Colleta Ndunguru, wakati wa hafla fupi ya usafirishaji wa mbegu kutoka kwenye Taasisi hiyo kwenda Hifadhi ya Kimataifa ya Mbegu ya Svalbard nchini Norway, iliyofanyika jana kwenye kituo hicho kilichopo Tengeru mkoani Arusha.

“Mbegu hizi si tu kwa ajili ya mboga, bali pia zina thamani kubwa ya lishe katika mnyororo wa thamani. Baadhi ya mbegu hutumika kama nafaka na unga wake unaweza kutengeneza vyakula kama mikate, keki na bidhaa nyingine zenye lishe bora,” alisema Dkt. N’Danikou.

Aliongeza kuwa kwa sasa taasisi hiyo inaendelea kufanya tafiti zaidi ili kubaini uwezo wa mbegu hizo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, magonjwa ya mimea na kupunguza utegemezi wa mbegu za kigeni.

WorldVeg pia imekuwa ikitoa mafunzo kwa wataalamu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Malawi na Zambia, ili kuhakikisha uendelevu wa utafiti na uhifadhi wa mbegu hizo za mbogamboga.

Katika hafla hiyo, wageni mbalimbali kutoka serikalini, mashirika ya kimataifa, vyuo vikuu na mashirika ya kilimo walijionea namna mbegu hizo zilivyofungwa kitaalamu kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Norway kwa ajili ya uhifadhi ya muda mrefu.