*Adaiwa kula njama wawekezaji wasilipe kodi

*Aendesha kikao bila Kagasheki kuwa na taarifa

*Bodi ya TANAPA yakataa mapendekezo yake

Mgogoro ulioripotiwa na Gazeti hili la JAMHURI wiki iliyopita kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheni na Naibu wake, Lazaro Nyalandu, sasa umechukua sura mpya.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu, ameingia matatani tena baada ya kubainika kuwa anashinikiza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) lisianze kutoza ‘concession fee’ katika hoteli za kitalii nchini, JAMHURI limebaini.

Uamuzi huo unaikosesha Serikali mapato yanayofikia Sh bilioni 17 kwa mwaka. Jaribio la kwanza la Nyalandu kufanikisha mpango wake liligonga mwamba kwenye kikao chake na menejimenti ya TANAPA, kilichofanyika Juni 8, mwaka huu mjini Moshi.

Nyalandu, kwa wadhifa wake wa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, alitaka TANAPA isaini makubaliano (MoU) na wenye hoteli ili waendelee kulipa asilimia 10 ya mapato kwa kila kichwa cha mgeni anayelala katika hoteli zao.

TANAPA imeweka wazi kuwa malipo kwa kila kichwa yanapaswa kuwa dola za Marekani kuanzia 20 hadi 50 kulingana na mambo makuu matatu – aina ya huduma, mahali hoteli ilipo, na hadhi ya hoteli husika.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, zinasema kwamba Nyalandu mara zote amekuwa akiwatetea wenye hoteli ambao wengi ni wawekezaji wenye asili ya Kiasia na wamefungua kesi kupinga ‘Concession fee’ zilizotangazwa na TANAPA.
Kwa shinikizo hilo, Nyalandu aliitisha kikao cha menejimenti ya TANAPA Juni 8, mwaka huu, na yeye akajipa mamlaka ya kuwa Mwenyekiti ili aweze kufanikisha mpango huo wa wenye hoteli.

Hata hivyo, kwa ujasiri menejimenti ilikataa shinikizo la Nyalandu la kuweka saini MoU na wenye hoteli, badala yake ikapendekeza uamuzi huo utolewe na Bodi ya TANAPA inayoongozwa na Modestus Lilungulu.

Wajumbe wa Bodi hiyo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Saidi Ali Mwema, Dk. Marcellina Chijoriga, Jenista Mhagama, Michael Laizer, Ruth Mollel, Hajjat Riziki Lulida, Winfrida Nshangeki, George Fumbuka, Nyambari Nyangwine, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori na Mtendaji Mkuu wa TANAPA ambaye ni Katibu wa Bodi.

Kikao cha Bodi ya TANAPA kiliketi na kukataa ombi la Nyalandu. Hayo ni kwa mujibu wa waraka uliovuja wa Bodi hiyo kwenda kwa Nyalandu. Barua hiyo ilikuwa na kichwa cha habari ‘Kikao kati ya TANAPA na Wawekezaji kuhusu Kesi ya Mahakama Kuu namba 25/2011.’

Barua hiyo ambayo JAMHURI imeipata kutoka ofisi ya Nyalandu (ilitumwa kwa barua pepe), inasomeka; ‘Mnamo tarehe 08 Juni 2012 kilifanyika kikao tajwa hapo juu ambacho wewe ulikuwa Mwenyekiti wake. Katika kikao hicho yalitolewa mapendekezo kadhaa ambayo yalihitaji uamuzi wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA.

“Bodi ya Wadhamini ya TANAPA katika kikao chake cha kawaida cha 175 kilichofanyika tarehe 15 na 16 Juni 2012 katika Hoteli ya Sal Salinero, Moshi, ilipitia kwa makini muhtasari wa kikao hicho na kuamua kama ifuatavyo:

“1. Bodi ya Wadhamini iliamua kuwa malipo ya ‘concession’ yatafanyika kwa mfumo wa ‘fixed rate’ kama ilivyokuwa imeidhinishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii tangu mwaka 2007. Viwango vilivyopendekezwa hadi sasa ni vya mwaka 2007 na havijabadilishwa. Hivyo ni vizuri viwango hivyo vikaendelea na kama kuna haja ya kuvibadili vitajadiliwa na mwekezaji mmoja mmoja na siyo kundi, kwani mikataba iliyopo ni kati ya TANAPA na mwekezaji mmoja mmoja.

“2. Vile vile Bodi iliona kuwa hakuna umuhimu wa kufanya utafiti kwa kushirikiana na wawekezaji kuhusu viwango vya ‘concession fee’, kwa sababu Bodi ya Wadhamini pamoja na Menejimenti ya TANAPA walishafanya utafiti huo na taarifa itafikishwa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii hivi karibuni.

“Taarifa ya utafiti huo itakuwa ndiyo kigezo cha kufanya makubaliano kati ya TANAPA na wawekezaji juu ya namna ya kulipa ‘concession fee’, kwenye mfumo wa ‘fixed rate’ iwapo tu wawekezaji wataiondoa kesi iliyopo Mahakama Kuu (kesi namba 25/2011).

“3. Bodi ya Wadhamini ya TANAPA haikubaliana na utaratibu wa kusaini ‘Memorandum of Understanding’ iliyopendekezwa na kikao hicho kwani ni kurudisha nyuma mchakato mzima ambao umekuwa ukikumbana na vikwazo mbalimbali toka mwaka 2007.

“4. Bodi ya Wadhamini inaona kwamba kwenye masuala ya msingi kwa maendeleo ya Taifa ni vyema kuwa na uamuzi wa Serikali kuliko kuyumbishwa na wafanyabiashara wachache kwa maslahi yao.” Mwisho wa kunukuhu.

Barua hiyo imesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Allan Kijazi, ingawa yeye mwenyewe alipoulizwa hakuwa tayari kukubali wala kukataa.

Alipoulizwa na JAMHURI, Kijazi alisema; “Masuala ya Bodi yanabaki kuwa ya Bodi, sina mamlaka ya kuyasema nje ya mtiririko wa vikao husika.”

Hata hivyo, JAMHURI ilipombana ili aeleze imekuwaje taarifa hiyo aandikiwe Naibu Waziri na si Waziri, Kijazi alisema; “Naomba umwulize Mwenyekiti wa Bodi, yeye ndiye msemaji wa masuala yote hayo unayoniuliza.”

Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa Bodi hiyo aliiambia JAMHURI kwamba barua hiyo ya msimamo wa TANAPA aliandikiwa Nyalandu kwa sababu yeye ndiye aliyeshinikiza binafsi apewa taarifa.

Alichukulia kigezo cha kuwa Mwenyekiti wa kikao cha Juni 8, akataka majibu ya msimamo wa Bodi apewe yeye, sisi tusingeweza kupinga hilo ingawa tulijua si utaratibu wa kawaida,” kimesema chanzo hicho.

Mmoja wa watu waliowahi kuwa wajumbe wa Bodi hiyo wakati Nyalandu naye akiwa mjumbe, ameiambia JAMHURI kwamba mara zote mwanasiasa huyo kijana amekuwa mtetezi mkuu wa wafanyabiashara wageni wanaopinga “concession fee”.

“Tukiwa naye kwenye Bodi alikuwa mtetezi mkuu wa Wahindi wenye hoteli, aliacha ujumbe baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, kwa hiyo kitendo cha sasa kupelekwa kwenye wizara hiyo kinamaanisha kuwa ataendelea kuwatetea wenye hoteli ili wasilipe viwango vipya,” amesema.

Mapato yanavyopotea

Wenye hoteli wanakataa kulipa “concession fee” kwa sababu wanajua kwa kufanya hivyo watakuwa wamekosa mwanya wa kuiumiza serikali kimapato. Kwa mfano, kwa utaratibu wa sasa, endapo mwenye hoteli atasema mgeni amelipa dola 50 za Marekani, kiasi kinachotakiwa kulipwa serikalini kupitia TANAPA ni dola tano tu. Ujanja huo unafanywa huku baadhi ya hoteli zikiwa zinatoza dola 500, dola 700 au zaidi.

Utaratibu mpya uliopendekezwa na kukubaliwa na Bodi ya TANAPA ni kwamba kila kichwa kinapaswa kulipiwa kuanzia dola 20 hadi 50 kwa usiku mmoja kulingana na aina ya huduma, mahali ilipo hoteli na kiwango chake.

Kwa utaratibu huo, hoteli nyingi za mikoa ya kusini ambako utalii haujapamba moto, zinaweza kulipa wastani wa dola 20 za Marekani kwa kichwa; ilhali ukanda wa kaskazini ambako kuna wageni wengi, malipo yanapaswa kuwa kati ya dola 40 hadi 50 kwa kichwa.

Kwa muda mrefu sasa, wenye hoteli wamekuwa wakitumia mwanya huo kuihadaa serikali na hivyo kuikosesha mapato. Lakini wenye ‘campsite’ wamekuwa wakilipa viwango hivyo vipya.

Utaratibu wa zamani unaopingwa na TANAPA kwa sasa unaiingizia wastani wa Sh bilioni nne hadi tano kwa mwaka. Kama wenye hoteli watalipa ‘concession fee’ kama ilivyoamuriwa na TANAPA, mapato ya Serikali yatapanda hadi Sh. bilioni 21 kwa mwaka.

Hii ina maana kwamba kwa msimamo wa sasa wa wenye hoteli unaoungwa mkono na Nyalandu, Serikali inakoseshwa mapato ya wastani wa Sh bilioni 17 kwa mwaka.

Nyalandu hapatikani

Taarifa za awali zilieleza kuwa Nyalandu alikuwa safarini kuelekea nchini Urusi kwa ajili ya mkutano wa Tanzania kuishawishi jumuiya ya kimataifa ikubali uchimbaji wa madini ya urani katika mbunga ya Selous. Hata baada ya kumpigia simu mara nyingi ilikuwa haipatikani. Pamoja na kutumiwa ujumbe wa maneno hakujibu.

Wiki iliyopita alizungumza na JAMHURI na kusema kuwa angekuwa safarini Urusi na msuguano wake na Waziri Kagasheki alisema haupo, ila yeye alikwenda kusuluhisha mgogoro. Katika mgogoro ulioripotiwa na gazeti hili ilielezwa kuwa Nyalandu alimchimba Kagasheki mbele ya wafanyakazi wa TANAPA, akidai kuwa alikurupuka kusimamisha kazi wafanyakazi 28 walioshiriki kuua faru.

Waziri Kagasheki alisema angemhoji, na jana tulipokwenda ofisini kwake Dar es Salaam, JAMHURI ilijulishwa kuwa naye Kagasheki alikuwa kwenye ndege akielekeza Urusi kwa nia ya kushawishi jumuiya ya kimataifa ikubali uchimbaji wa madini ya urani.

By Jamhuri