DAR ES SALAAM 

Na Aziza Nangwa

Kauli ya ofa iliyotolewa wiki iliyopita na Rais Samia Suluhu Hassan kwa wapangaji wa Magomeni Kota imepokewa kwa mitazamo tofauti; JAMHURI limeambiwa.

Akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa nyumba za Magomeni Kota wiki iliyopita, Rais Samia amesema ameridhia ombi la kuwafanya wawe wapangaji – wanunuzi, na kwamba wanaweza kuanza mara moja kulipa kidogo kidogo gharama za ununuzi.

Nyumba hizo zenye uwezo wa kuchukua kaya 644 zimejengwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA) kwa gharama ya Sh bilioni 52.

“Hatutawatoza gharama ya ardhi kwa sababu tukifanya hivyo mtashindwa kuzinunua,” amesema Rais Samia.

Wakizungumza na JAMHURI kuhusu ofa hiyo ya Rais, baadhi ya wakazi wa Magomeni wanaonyesha shaka, wakisema hawana uwezo, wakiiomba TBA kupunguza bei.

Mmoja wa wakazi hao, Ramadhan Biliwa, amesema wengi wa wapangaji ni wajane na wastaafu na si rahisi kumudu gharama za ununuzi.

“Ukipiga hesabu utakuta kila nyumba inapaswa kuuzwa kwa Sh milioni 80 hivi. Hii ni kwa kuwa TBA wametumia Sh bilioni 52 kujenga nyumba 644.

“Sasa katika mazingira tuliyo nayo sisi hatuwezi kumudu kulipa Sh milioni 80. Ni kiwango kikubwa sana hiki. Hata ingekuwa Sh milioni 20! Maisha tunayoishi tunayajua wenyewe. Ninachojua kuna watu watakaa kwa muda kisha wataondoka,” amesema Biliwa.

Hata hivyo, pamoja na hofu yake, TBA bado hawajaweka hadharani gharama za ununuzi na muda wa kulipa kwa anayetaka kununua. Biliwa ameiomba serikali kuwatazama kwa jicho la huruma zaidi wajane na wastaafu wa Magomeni Kota. 

Akizungumza na JAMHURI, Kaimu Mkurugenzi wa TBA Idara ya Miliki, Saidi Mndeme, amesema mchakato wa gharama za ununuzi wa nyumba hizo unaendelea.

“Maelekezo yametolewa kwetu ghafla (na Rais). Baada ya kukamilika kwa mchakato, gharama zitatolewa kwa wahusika,” amesema Mndeme.

Amesema TBA ilijenga nyumba hizo kwa kutazamia kuzipangisha, lakini sasa wameelekezwa kuwauzia wapangaji wao.

“Aliloelekeza Rais ni jambo zuri sana kwa wananchi, kwani ameonyesha huruma na kuwajali kulingana na hali zao,” amesema.

Kabla ya tamko la Rais, wapangaji wa Magomeni Kota walikuwa wamejiandaa kuishi bure kwa miaka mitano kisha kuanza kulipa kodi za kila mwezi, kama walivyokuwa wameahidiwa na mtangulizi wa Rais Samia, Dk. John Magufuli.

Katika hotuba yake, Rais Samia ameipongeza TBA kwa ubunifu wa kuweka eneo la biashara ndogondogo (Machinga Complex), masoko ya kisasa (supermarkets) na maegesho ya magari.

Akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa TBA, Daud Kondoro, amesema kazi za ubunifu, usanifu, ujenzi na usimamizi zimetekelezwa na TBA kwa kushirikiana na TEMESA kwa kutumia wataalamu wa ndani.

“Kazi yenyewe ilizingatia mabadiliko chanya ya ukuaji wa sekta muhimu, kanuni na viwango bora vya ujenzi vya serikali.

“Ujenzi ulianza Oktoba 2016, ambapo eneo lililojengwa hivi sasa lina ukubwa wa ekari tisa, likigharimu Sh bilioni 52.19 na sasa mradi umekamilika kwa asilimia 100,” amesema.

By Jamhuri