Na Pascal Mwanache, TEC
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima, ameongoza Misa Takatifu ya shukrani kwa mara ya kwanza leo, Juni 3, 2025, baada ya kutoka hospitalini alikokuwa amelazwa kwa takribani mwezi mmoja kufuatia tukio la kushambuliwa.
Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili lililopo makao makuu ya TEC-Kurasini, jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na mapadri, watawa pamoja na wafanyakazi wa Sekretarieti ya TEC, ikiwa ni ishara ya shukrani kwa Mungu kwa uponyaji wake.
Akihubiri katika misa hiyo, Padri Kitima alionesha ujasiri na shukrani kwa Mungu kwa kumponya dhidi ya jaribio la kukatisha uhai wake, huku pia akiwashukuru wote waliomuombea na kumtumia salamu za pole wakati wa matibabu.
“Tunamshukuru Mungu kwa wema wake. Pia tunawashukuru wote walioguswa na tukio lile. Tuombe Kanisa lizidi kuwa imara bila kutetereka. Kanisa Katoliki ni taasisi inayotegemewa na wengi, ni sauti ya wasio na sauti, ni msindikizaji wa wanyonge,” alisema Padri Kitima kwa sauti ya matumaini.
Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa pamoja na changamoto, Kanisa linapaswa kuendelea kuwa mwanga na tumaini kwa Watanzania, akiwataka wafanyakazi wa Sekretarieti ya TEC kuyapokea yaliyotokea kwa jicho la imani.
“Mungu hatakaa kimya; atajibu sala zetu. Tuwe imara katika kazi zetu. Tukumbuke kuwa hata mitume walipata misukosuko, lakini hawakurudi nyuma. Nasi tusirudi nyuma, tubaki thabiti katika imani,” aliongeza kwa msisitizo.
Ibada hiyo imeacha alama ya mshikamano na imani miongoni mwa washiriki, huku wengi wakiona kurejea kwake kama ishara ya ushindi wa imani dhidi ya hofu.


