Baada ya sala ya Jumapili katika Kanisa Katoliki Jumapili, Papa Francis ametoa wito tena wa ulinzi wa raia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya mashambulizi ambayo yameua mamia katika wiki za hivi karibuni.

“Habari za kusikitisha za mashambulizi na mauaji zinaendelea kutoka eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” alisema mkuu wa Kanisa Katoliki.

Papa Francis alitembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwanzoni mwa mwaka jana ambapo aliiomba dunia “kuondoa mikono yake kutoka Congo”, akiishutumu kwa kupora maliasili na kusababisha vita vya ndani kutokwisha.

“Ninatoa wito kwa mamlaka za mitaa na jumuiya ya kimataifa kufanya kila linalowezekana kukomesha uhalifu na kulinda maisha ya raia,” alisema Jumapili.

Aliongeza kuwa wale wanaouawa “wengi ni Wakristo, wanauawa kwa sababu ya chuki ya imani. Hao ni mashahidi”.

Mauaji ya hivi karibuni katika eneo la Lubero huko Kivu Kaskazini yamefanya kundi ADF kunyooshewa kidole kwa sababu hawashiriki imani yao.

Kundi hili linalodai kufuata dini ya Kiislamu, dini isiyokubali matendo kama yao, linadai kuwa linafanya kazi na kundi la Islamic State, ambalo wote wameorodheshwa kuwa makundi ya kigaidi na nchi mbalimbali.

Wiki iliyopita, picha za kutisha za miili ya raia iliyokatwa viungo vyao ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto huko Lubero zimeendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

ADF imelaumiwa kwa kuwaua watu hao katika maeneo tofauti ya Lubero na Beni, ambapo shirika la habari la AFP linasema kuwa takribani watu 150 wameuawa katika muda wa wiki mbili pekee mwezi huu.

Papa Francis pia alitoa wito wa amani katika maeneo mengine ya dunia ikiwa ni pamoja na Sudan, Myanmar, Ukraine, “na kila mahali watu wanakoteseka kutokana na vita”.