Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda ametoa mwito kwa wananchi wasikubali kuhadaiwa na viongozi wanaotafuta madaraka kwa kutoa rushwa.

Alisema hayo jana wakati akitoa salamu za pole kwa familia ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya na wananchi wa Mwanga.

“Viongozi wetu wametuasa, tuwakatae wanaogawa vihela huku na huko ili waje watuhudumie. Sasa kama nia yako ni kutoa huduma una haja gani ya kutoa rushwa? Sisi tutakupima kwa kazi utakayoifanya,” alisema Pinda.

Pinda alisema viongozi wengi walipenda kukutana na kuzungumza na Msuya ili kuchota busara zake na kupata la kuzungumza.

Alisema Msuya amefanya mambo mengi mazuri ikiwamo kupenda kusema ukweli hata katika mazingira magumu.

Pinda alisema alichagua kuja Mwanga kutokana na historia ya yale yaliyowahi kutokea na kupitia kwa kiongozi huyo aliyeheshimisha Mwanga na taifa kwa ujumla.

Aidha, alisema Mwanga ni kama nyumbani kwa sababu baadhi ya wajukuu zake wanasoma katika wilaya hiyo.

Alisema ujumbe huo ambao awali ulitolewa na Askofu mteule wa Dayosisi ya Mwanga, Daniel Mono unafaa kwa watu wote wenye ndoto za kutafuta uongozi katika ngazi ya ubunge na udiwani.

Aliwashukuru viongozi wa dini kutokana na utaratibu wao wa kuliombea taifa na viongozi wake katika matukio mengi ya kitaifa.