Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimeongeza idadi ya wahitimu wa fani mbalimbali kupitia mfumo wa elimu ya mtandao na masafa, kutoka 62,217 kwa mwaka 2023/2024 hadi 67,359 mwaka 2025.
Ongezeko hilo limetokana na kuhitimu kwa wanafunzi 5,142 zaidi, wakiwemo 49 waliotunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD), kati yao wanaume 40 na wanawake 9.
Akizungumza katika mahafali ya 44 ya chuo hicho yaliyofanyika Novemba 27, 2025 -Bungo, wilayani Kibaha, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Kayanza Peter Pinda, ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuthamini na kutumia mfumo wa elimu huria ya mtandao na masafa akisema ni njia bora na rahisi ya kupanua wigo wa elimu ya juu nchini.

Pinda alisema, elimu huria ya masafa imekuwa msingi muhimu katika kufanikisha malengo ya Taifa kuelekea uchumi wa kati na viwanda, huku akibainisha kuwa mfumo huo unatumiwa duniani kote ikiwemo India, China na Botswana ambako alitembelea hivi karibuni kuona maeneo ya ushirikiano.
Alieleza ,ongezeko la idadi ya wahitimu kila mwaka linampa faraja, na kwamba hatua ya chuo kuendesha mahafali katika mikoa mbalimbali imekuwa kichocheo kikubwa cha kukitangaza na kuongeza ushawishi kwa wanafunzi wapya.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Alex Makulilo, alifafanua OUT bado haina miundombinu ya kudumu katika mikoa ya Tabora, Tanga, Songwe, Katavi, Mara na Unguja, na hivyo imekuwa ikitegemea majengo ya kupangisha, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji.

Alibainisha kuwa ,mawasiliano yanaendelea kati ya chuo na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutafuta ufadhili wa ujenzi wa ofisi katika mikoa hiyo.
Aidha, aliitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kutunga sera itakayopunguza gharama za huduma za mtandao kwa taasisi za elimu zinazotoa huduma kwa manufaa ya umma na si kibiashara.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa LATRA na mhitimu wa Shahada ya Uzamivu, Dkt. Habibu Suluo, alieleza elimu haina mwisho na kwamba hata viongozi hawapaswi kukata tamaa ya kujiendeleza.

“Licha ya majukumu yangu, sikukata tamaa. Tumetunukiwa PhD 49 mwaka huu na tafiti yangu imekuwa bora kwa mwaka 2025,” alieleza Suluo.
Mhitimu mwingine, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Juma Chikoka, anasema elimu aliyoipata ni mwanzo wa historia mpya kwenye safari yake ya uongozi, na ametaja dhamira ya kuitekeleza kwa vitendo kupitia uongozi wa kimkakati na ubunifu kwa manufaa ya wananchi.






