Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limeshiriki katika kuingia kwa mabavu katika eneo la biashara la kampuni ya uuzaji mafuta ya Petrofuel (T) Limited na Isa Limited, hali ambayo ni kinyume cha utaratibu.

Askari Polisi, waliotumika kuingia katika eneo hilo ni wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), katika eneo linalosadikiwa kuwa na ugomvi wa kibiashara. Pamoja na kuondolewa kwa mabavu, hapakuwa na nyaraka zozote za kisheria zilizoruhusu kuondolewa.

Kampuni hizo mbili ni wapangaji katika eneo linalosadikiwa kumilikiwa na Hasham Kassam and Sons Limited. Kampuni ya Petrofuel ambayo inajihusisha na biashara ya mafuta ya jumla, inayo matangi ya kuhifadhia mafuta katika eneo, mpaka siku ya tukio matangi hayo yalikuwa na lita za ujazo zipatazo 200,000 za mafuta ya dizeli.

“Hatukuwahi kuhusishwa katika shauri lolote mahakamani, vilevile hatukuwahi kupatiwa amri ya kuondoka katika eneo la kitalu namba 12B, kitalu E, Plot namba 20, vilivyoko barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Juni, mwaka huu mawakili wawili wa upande wa kampuni ya Educational Books Publishers Limited, waliingia kwa nguvu katika eneo letu la biashara na kutuondoa kwa kutumia kikosi cha kutuliza ghasia, hakuna hatua zozote za kiusalama zilizochukuliwa hasa ikizingatiwa eneo husika lina mafuta, tumesababishiwa hasara kubwa,” inasomeka sehemu ya taarifa ya kampuni hiyo.

Akizungumza na JAMHURI, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, anasema hawezi kuongea zaidi kuhusu tukio hilo na kwamba, amejipangia utaratibu wa kuongea na waandishi wa habari.

“Samahani siwezi kukujibu maswali yako…nilishaweka utaratibu wa kuongea na waandishi mara tatu kwa wiki, leo ni weekend, nitafute wiki ijayo,” anasema Sirro

Hata hivyo, kampuni hiyo imetoa taarifa kwa umma, kwamba ardhi inayojulikana kwa namba na hati iliyotajwa muda wote imekuwa ni mali ya kampuni ya Hasham Kassam and Sons Limited.

“Kwa njia ambayo inaleta mashaka sana, inasemekana iliuzwa kwa kampuni ya Educational Books Publishers Limited, katika kile kilichoitwa utekelezaji wa hukumu katika shauri la kazi na.298 la 1998, Sirilly Lushinga na wenzake, dhidi ya H. K. Foam Limited, kampuni ambayo ni tofauti na kampuni ya Hasham Kassam and Sons Limited,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema, hati halisi ya kumiliki ardhi hiyo na.186074/21 wanayo Hasham Kassam and Sons Limited na hapajakuwa na amri ya Mahakama ikiwaagiza Hasham Kassam and Sons Limited au wapangaji wake Petrofuel (T) Limited na Isa Limited kuhama na kukabidhi  majengo kwenye ardhi hiyo kwa Educational Books Publishers Limited.

Lakini, Juni 24, mwaka huu, Educational Books Publishers Limited walitumia nguvu kuingia katika eneo hilo bila kuwa na amri halali ya Mahakama, na kuwafungia nje wapangaji  wa eneo hilo, Petrofuel (T) Limited na Isa Limited, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Uhalali wa mauzo ya mali hiyo kwa Mohamed Suleiman Mohamed na kuandikishwa kwa Educational Books Publishers Limited kuwa mwenye ardhi hiyo kunabishaniwa mahakamani sasa.

Umma kwa ujumla unaalifiwa kuwa yeyote atakayeingia katika mazungumzo ya aina yoyote na Educational Books Publishers Limited au mawakala wake kuhusiana na ardhi ijulikanayo kama kitalu namba 12 B Block E, Plot 20, sehemu ya barabara ya Pugu, jijini Dar es Salaam. 

Agosti, mwaka huu JAMHURI iliandika kuhusiana na mgogoro huu, huku likiainisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukosa mapato yanayokadiriwa kufikia Sh bilioni 3 hadi Sh bilioni 4 kwa mwezi.

Petrofuel (T) Limited, ni mpangaji katika kiwanja kinaachodaiwa kumilikiwa na kampuni ya Educational Books Publishers Limited, kiwanja namba 12B, sehemu ya E.P Lot 20, kilichoko Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya Educational Books Publisher, inamilikiwa na mfanyabiashara Mohamed Suleiman Mohamed (Osama), anayetajwa kuwa na vitegauchumi kadhaa jijini Dar es Salaam.

Osama, ameingia kwenye mvutano wa umiliki wa kiwanja hicho na mfanyabiashara Hasham Kassam, ambaye anadai kuwa na umiliki halali wa kiwanja hicho chenye hati Na. 186074/21. Kassam ndiye aliyeingia mkataba wa kukodisha eneo hilo kwa kampuni ya Petrofuel.

Pamoja na kutolipwa kwa kodi hiyo, wakili wa kampuni hiyo ameiambia Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuwa maelfu ya wananchi walio jirani na maghala ya kampuni hiyo wanakabiliwa na janga la moto ambao huenda ukasababishwa na matangi ya mafuta ambayo wataalamu wa Petrofuel wamezuiwa kuyasogelea ili kuhakiki usalama wake.

Kwa mujibu ya nyaraka ambazo JAMHURI imeziona, kampuni hiyo imejikuta ikiondolewa katika eneo hilo licha ya kuingia mkataba halali wa upangaji na mmiliki.

Nje ya Mahakama, imeelezwa kuwa juhudi za uongozi wa Petrofuel, za kuomba mamlaka za kidola zisaidie kuepusha hatari ya mlipuko huo zimegonga mwamba baada ya kukosa ushirikiano katika ngazi ya Polisi na Mkoa wa Dar es Salaam.

Pia kitendo cha kutumiwa kwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwenye operesheni hiyo, nacho kimeelezwa kuwa si cha kawaida katika mazingira ambayo hayakuwa na ukinzani kutoka kwa anayehamishwa.

Hivi karibuni, kampuni ya udalali ya Yono ilikwenda kutekeleza amri ya kufunga ofisi za kampuni hiyo katika mazingira ambayo bado yanaibua maswali kadhaa.

Kwenye operesheni hiyo, Petrofuel wanalalamika mali kadhaa kuibwa, vikiwamo vifaa na fedha taslimu.

“Operesheni ya kufunga ofisi za kampuni ya Petrofuel (T) Limited zilisimamiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia, pamoja na watumishi wa kampuni ya udalali…hawakuonesha nyaraka zinazowaruhusu kufanya hicho walichokifanya,” kimesema chanzo chetu.

Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama, shauri hilo lilisikilizwa na Jaji Lugano Mwandambo, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Julai 21, mwaka huu. Uamuzi wa, au kutoa, au kutotoa hati ya zuio unatajiwa kutekelezwa wiki mbili zijazo.

Katika shauri hilo, kampuni ya Petrofuel (T) Limited inasema kuna matangi sita ya mafuta ya dizeli yenye lita 278,000 pamoja na vipuri vya mitambo na magari kwa ajili ya migodi ya madini.

Kampuni hiyo inasema endapo haitaruhusiwa kuokoa mali hizo, itafilisika kutokana na kutopewa fidia na taasisi za kifedha.

“Tunashauri kwamba namna bora ya kushughulikia hayo matangi ya mafuta kunahitajika utaalamu mahsusi ambao hao tunaowashtaki hawana, hivyo matangi hayo yanaweza kulipuka,” inasomeka sehemu ya shauri hilo.

2973 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!