Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Kufuatia kuongezeka kwa matukio ya ukatili na vitendo vya kihalifu katika vyuo vikuu mkoani Dodoma, kumelilazimu Jeshi la Polisi mkoani hapa kushirikiana na viongozi wa Serikali za wanafunzi kutoka Vyuo mbalimbali vya elimu ya juu ili kutafuta suluhu ya kudumu.

Katika mkutano uliofanyika Mei 15, 2025 jijini Dodoma, baadhi ya makosa yaliyotajwa kutokea vyuoni ni pamoja na usagaji, ubakaji, ushawishi wa imani kali za kidini unaowafanya wanafunzi kutoweka chuoni kwa muda mrefu, kuiga mitindo hatarishi ya maisha, kujihusisha na siasa, utupaji wa watoto, wizi wa kimtandao na mahusiano yasiyofaa.

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa wa Polisi ASP Komeya Stephen ameeleza kuwa moja ya mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo ni kutengeneza mpango kazi wa kiusalama utakaowajumuisha wanafunzi katika elimu ya ngono salama kuepuka mimba zisizotarajiwa, ushiriki katika mfumo wa haki jinai, pamoja na kutoa elimu dhidi ya uhalifu wa kimtandao.

Aidha, Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma limeeleza dhamira yake ya kuimarisha mahusiano na wanafunzi kupitia dhana ya ulinzi shirikishi ili kuzuia na kugundua mapema matukio ya kihalifu ambayo yanaweza kuzuilika kabla ya kusababisha madhara.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP George Katabazi, amesema kuwa jeshi lake limeanza rasmi kushirikiana na vyuo vyote vilivyopo mkoani humo kwa lengo la kuimarisha usalama na kudhibiti uhalifu, hasa baada ya kushuhudiwa ongezeko la matukio ya ukatili kwenye baadhi ya taasisi hizo.

Akitolea mfano, Kamanda Katabazi amegusia tukio la karibuni katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambapo mwanafunzi mmoja alipoteza maisha baada ya ugomvi na mwenzake, akisisitiza kuwa tukio hilo limeamsha hitaji la hatua madhubuti.

“Hali hii haipo UDOM pekee, bali hata katika vyuo vingine ingawa viwango vya uhalifu vinatofautiana. Tunatoa wito kwa wanafunzi kutoshiriki uhalifu wa aina yoyote na badala yake wawe mabalozi wa amani,” alisema.

Ameongeza kuwa kupuuza uhalifu ni hatari kwa sababu unaweza kumdhuru mtu yeyote. “Uhalifu hauna mipaka. Ukikaa kimya bila kukemea au kutoa taarifa, nawe unakuwa sehemu ya tatizo. Toeni taarifa kwa vyombo husika kuhusu vitendo hivyo ili kuepusha madhara zaidi,” alisisitiza.

Kamanda Katabazi pia amewaasa wanafunzi kuepuka kujihusisha na vurugu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, akiwakumbusha kuwa bado wana jukumu kubwa la kujenga maisha yao ya baadaye.

“Niwaombe viongozi wa serikali za wanafunzi kuhakikisha ushirikiano huu na Jeshi la Polisi unakuwa wa kudumu. Tushirikiane katika programu mbalimbali, ikiwemo michezo ya pamoja, kwa lengo la kuimarisha mshikamano na kuzuia uhalifu,” ameongeza.

Naye Mchungaji Rev. Ivo Livingstone Augustino kutoka Chuo Kikuu cha St. John’s amependekeza kuwepo kwa ufuatiliaji wa karibu wa kesi zinazowahusu wanafunzi wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali, ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wote.

Pia amesisitiza umuhimu wa kupewa kipaumbele suala la usalama barabarani, hasa kwa wanafunzi wa Chuo cha Mipango wanaosafiri kwa wingi, akibainisha kuwa mazingira salama huongeza tija katika elimu