Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Moshi
JESHI la Polisi nchini limesema halitamvumilia mtu yeyote au kikundi chochote ambacho kitajihusisha na vurugu wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Aidha, jeshi hilo limesema liko tayari kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani, utulivu na kwa haki katika mchakato wake mzima.
Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Awadhi Juma Haji ametoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo ya uongozi mdogo kwa jeshi hilo ngazi ya Sajini iliyofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania Moshi (TPS-Moshi) mkoani Kilimanjaro.
“Hatutakuwa na muhali na mtu yeyote au kikundi chochote ambacho kitataka kuvuruga uchaguzi wakati wote wa kampeni, siku ya uchaguzi na hata baada ya uchaguzi, jeshi litatimiza wajibu wake ili wahusika wachukuliwe hatua zinazostahili kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Haji alitoa wito kwa wahitimu wa mafunzo hayo kushirikiana na maofisa wenzao wa jeshi hilo ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao ili wananchi wapate fursa ya kutimiza haki zao za kuchagua na kuchaguliwa.
Alitoa rai kwa wahitimu hao kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili na weledi mkubwa ikiwemo kutekeleza mikakati ambayo italenga kupunguza na hatimae kumaliza changamoto ya ajali za barabarani.
Katika hafla hiyo aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuliboresha Jeshi la Polisi nchini jambo ambalo alisema limechangia ufanisi wa jeshi hilo kutekeleza majukumu yake.
“Serikali imetoa na inaendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuliboresha jeshi la polisi; hili limepelekea jeshi kutekeleza majukumu yake kwa weledi wa hali ya juu,” alisema.
Akitoa taarifa ya mafunzo hayo, Kamanda wa TPS-Moshi, Ramadhan Mungi alisema wanafunzi 2,068 wamehitimu mafunzo hayo kati ya 2,078 walioanza mafunzo hayo Machi, mwaka huu.
“Tisa kati ya wanafunzi walionza mafunzo hayo Machi 14, 2025, waliondolewa mafunzoni kwa kukiuka maadili ya mafunzo ikiwemo mahudhurio hafifu,” alisema na kuongeza mmoja alifariki dunia kwa ajali.
