Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Kukua kwa kasi na kuimarika kwa sekta ya utalii nchini kunachagizwa kwa kiwango fulani na kuwapo kwa huduma bora za kijamii, ikiwemo uhakika wa usalama kwa wageni.
Tanzania ni moja ya mataifa yenye kuvutia utalii wa aina mbalimbali, wengi wakiisifu kwa amani, utulivu na ukarimu wa wenyeji.
Akizungumza jijini Arusha wiki iliyopita, Mkuu wa Kitengo cha Polisi na Diplomasia, SP Waziri Tenga, anasema taarifa za uhalifu dhidi ya watalii zimepungua kwa kiwango kikubwa kwa sasa.
“Kikosi cha Polisi Utalii na Diplomasia ni maalumu kuhudumia watalii, kikiwa kimepata mafunzo nje ya nchi kuimarisha uwezo wa maofisa wake na ndio maana sasa usalama wa watalii na watoa huduma za utalii umeboreka. Uhalifu umedhibitiwa,” amesema SP Tenga.

Anataja mbinu wanazotumia kuwa ni kuzikabili changamoto kabla ya kutokea kwa kutoa kipaumbele katika usalama wa watalii hata kabla hawajaingia nchini.
Huduma zinazotolewa na polisi wa utalii ni za aina yake ambazo hazipo mahali pengine popote barani Afrika, hivyo kuifanya sekta ya utalii Tanzania kuwa ya kuvutia zaidi, huku mapato kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na serikali yakiongezeka.
“Tunashirikiana na mabalozi wa mataifa mbalimbali kukusanya taarifa za awali kuhusu raia wao wanaotembelea nchini, ni kuwahudumia,” amesema.
Mbali na watalii kufika Kituo cha Polisi na Diplomasia kilichopoo jijini Arusha, pia vipo vituo vingine maeneo mbalimbali vinavyotoa huduma huku mawasiliano ya kimtandao nayo yakikubalika.
“Watalii wanaweza kutuma taarifa moja kwa moja kupitia tovuti ya kikosi au baruapepe kutaka kufahamu chochote kuhusu usalama wao au iwapo mawakala wa utalii wanaowapa huduma wamesajiiliwa. Hii imeondoa utapeli uliokuwapo awali,” amesema.
Maofisa na askari wa kikosi hiki hutoa ulinzi kwa wageni kwa kuwapa ulinzi na kuwasindikiza (escort) kutoka viwanja vya ndege hadi wanakoelekea, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwapo ‘Tanzania Association of Tour Operators (TATO).

Mbali na doria za kawaida katika maeneo wanayoishi au kutembelea watalii, makachero na maofisa wa Polisi Utalii na Diplomasia hufanya doria mtandaoni kubaini matapeli.
“Pia tumekuwa na vizuizi barabarani na ‘check points’. Arusha kuna vituo vya ukaguzi maalumu kwa magari ya utalii kuwawezesha wageni kutoa taarifa ya tabia au mwenendo wa dereva na changamoto zozote walizopata.
“Hizo tumeziweka makusudi kabisa, kwa ajili ya usalama wa wageni. Inawezekana mgeni amepoteza nyaraka (kama pasipoti). Huyu halazimiki kusafiri mpaka hapa kituoni! Anaweza kutoa taarifa kwenye vituo vyetu huko huko ‘field’,” anasema.
Awali, tatizo la kupotea kwa nyaraka muhimu kama pasipoti, lilizua usumbufu mkubwa kwa wageni, lakini sasa, kwa kuripoti upotevu huo, kikosi cha Polisi Utalii na Diplomasia huingilia kati haraka kwa kuwasiliana na ubalozi husika na kutoa ‘loss report’ kuwezesha Idara ya Uhamiaji/ubalozi kutoa nyaraka za dharura, hivyo mgeni kuendelea na utalii bila shaka yoyote.
Afande Tenga anasema changamoto kubwa ilikuwa ni utapeli wa kwa kutumia teknolojia, ambapo wahalifu husajili kampuni bandia ikijifanya inatoa huduma kama kukodisha magari.
“Wataalamu wetu wa teknolojia ya habari hawashughuliki na kugundua ulaghai pekee, bali huungana na polisi wa nchi husika kuwashughulikia matapeli. Tumeshawakamata wahalifu wengi kwa njia hii,” anasema Tenga.
Anasema wapo pia baadhi ya watalii wasio waaminifu ambao hutengeneza matukio ili walipwe bima wanaporejea makwao, tatizo ambalo limetoweka kutokana na uchunguzi wa kina unaofanywa na kikosi cha Polisi Utalii na Diplomasia.

“Huja hapa kutaka ‘loss report’, sasa sisi hatuitoi mpaka tujiridhishe kweli ameibiwa? Kutoa ‘loss report’ bila kujiridhisha ni sawa na kuutangazia ulimwengu kwamba nchi yetu si salama; na watu wetu ni wezi,” anasema.
Kwa upande mwingine, Tenga anasema ili kuboresha huduma kwa watalii, kikosi kwa kushirikiana na wadau kina mkakati wa kuanzisha ‘vituo vya huduma za pamoja’ (one stop center).
Vituo hivyo vitakuwa na vifaa vya kisasa na wataalamu wenye weledi kushughulikia changamoto za usalama kwa watalii na wato huduma.
“Kwa mfano, tuwe na sehemu ambayo kutakuwa na watu wa Uhamiaji kwa ajili ya kutoa nyaraka za kusafiria wakati sisi tunatoa ‘loss report’ baada ya kupokea taarifa ya mgeni kupoteza pasipoti,” anasema Tenga.
Mara vitakapoanzishwa vituo hivyo, Tenga anasema vitakuwa vinafanya kazi kwa saa 24 kuhakikisha wageni wanafanya shughuli iliyowaleta nchini, utalii, bila kikwazo chochote huku mgeni akihakikishiwa kuwa yupo kwenye mikono salama.
Kikosi hiki chini ya Mrakibu wa Polisi, Waziri Tenga, kimekuwa nguzo muhimu katika sekta ya utalii nchini, kikitoka kwenye utekelezaji wa sheria tu na kutoa huduma kamili ya usalama na uhakikisho wa kidiplomasia kwa watalii.
Tangu kuanzishwa kwake, kikosi cha Polisi Utalii na Diplomasia kimetembelewa na kusifiwa na mabalozi mbalimbali wanaowakilisha mataifa yao nchini, huku wageni wakikiandikia baruapepe kukiri kuridhishwa na huduma walizopewa.


