Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

JESHI la Polisi kupitia Kikosi cha Polisi Wanamaji limefanikiwa kukamata majahazi yakiwa na mafuta ya kupikia dumu 1731.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji, ACP Moshi Sokoro amesema katika ufuatiliaji kikosi kazi cha Polisi Wanamaji Dar es salaam kikitumia boti za Polisi walifanikiwa kukamata majahazi mawili, MV. UKIMAINDI POA na jahazi lingine lisilokuwa na jina wala namba za usajili katika bahari ya Hindi, Dar es Salaam yakiwa na watuhumiwa wanne akiwepo Nahodha Masoud Rajabu.

“Walikuwa wamebeba mafuta ya kupikia dumu 1731 zenye ujazo wa lita 20 kila moja wakiwa na nia ya kukwepa ushuru wa forodha.

“Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini watuhumiwa hao hawakuwa na nyaraka zinazothibitisha uhalali wa umiliki wa mizigo hiyo ya mafuta ya kupikia pamoja na nyaraka za usafirishaji,” amesema.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji katika kipindi cha Mei hadi Juni, mwaka huu wamefanikiwa kukamata faiba boti nane (8) ambazo hazina usajili wala majina na zikiwa zinajihusisha na usafirishaji wa abiria kwa njia hatarishi katika fukwe ya Kigamboni na soko la Samaki feri.

“Pia Kikosi cha Polisi Wanamaji Dar es salaam tumefanikiwa kupeleka kesi saba mahakamani ambazo zipo katika hatua mbalimbali za kimahakama, na moja kati hizo mtuhumiwa amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili au faini ya sh. milioni mbili kwa makosa ya uvuvi haramu.

“Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa wafanyabiashara wasio waadilifu kuacha kusafirisha mizigo kwa njia ya bahari bila kuwa na nyaraka za mizigo hiyo. Pia kwa wavuvi haramu na wamiliki wa boti pamoja na manahodha wanaobeba abiria kwa boti ambazo sio salama maeneo ya feri Kigamboni na feri Magogoni, Jeshi la Polisi halitasita kuchua hatua kwa wahalifu wote wanaojihusisha na uhalifu huo,” amesema.

Alitoa wito kwa kwa wananchi wote wanaochukia uhalifu na kuendelea kutoa taarifa za wahalifu kwa Jeshi la Polisi ili zifanyiwe kazi haraka na kuweza kutokomeza uhalifu kwa pamoja.

Mwisho