Ni ajabu na kweli, magari matano kati ya manane yaliyokuwa yanahusishwa na ‘papa wa unga’, yaliyokuwa yamehifadhiwa Kituo cha Polisi Oysterbay yameondolewa kituoni hapo kwa njia za utata.

Magari hayo ya kifahari ni mali ya Lwitiko Samson Adam (Maarufu kama Tikotiko), ambaye alikamatwa mwishoni mwa mwaka 2017 kisha kuachiwa kabla ya kukamatwa tena.

Magari hayo ya kifahari ambayo yamekuwa kwenye maegesho Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam, ‘yamechukuliwa’ kwa mchongo uliosukwa na baadhi ya vigogo wa Jeshi la Polisi, huku baadhi ya wakubwa wakidai hawajui lolote.

Miongoni mwa wanaosema hawafahamu kinachoendelea ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mussa Taibu, ambaye amehamishiwa Kinondoni hivi karibuni.

Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la JAMHURI katika kipindi cha miezi miwili umebaini kwamba magari hayo yaliondolewa kwa awamu tatu ndani ya mwezi Mei, mwaka huu huku gari namba T 874 CZZ ambalo ni Range Rover Sports (Lumma CLR RS) la rangi nyeupe ndilo lilianza kuchukuliwa mwanzoni.

Mei 16 magari matatu yaliondolewa kituoni hapo ambayo ni T 917 DBR (Lexus), T 635 BTJ (Renault) na T 499 ADW (Rav4). Baada ya wiki moja gari namba T 906 CHC (BMW X6) liliondolewa kituoni hapo.

Mpaka tunakwenda mitamboni ni magari matatu tu yamebaki kituoni hapo ambayo ni T 765 DAR, T 313 BXG na CA 146-605 aina ya Dodge.

Vyanzo vyeti vimeeleza kuwa magari hayo yameondolewa kituoni hapo kwa hati (nyaraka) inayoonyesha kuwa yameokotwa.

“Unajua kuna mambo yanashangaza. Haya magari ukiangalia kwenye vitabu vyetu yanaonyesha kuondolewa hapa kwa kuokotwa. Yaani juzi tu Rais Magufuli ameonyesha hasira zake kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ila ndani ya Polisi mambo ni kama kawaida.

“Sasa wakubwa wameona njia ya kuyaondoa hapa ni kufanya kama mali ya kuokotwa…tangu niajiliwe ndiyo kwanza nimesikia kwamba vidhibiti vilivyoko Polisi vinaweza kuwa mali iliyookotwa.

“Kiutaratibu magari hayo yalitakiwa kukabidhiwa kwa Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), lakini wakubwa hapa wamekuwa wanakwepa kuyakabidhi, kumbe lengo ni kuyanywa,” kinasema chanzo chetu ndani ya Polisi.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Mei 15 saa 12:30 jioni, magari ya Tikotiko yaliorodheshwa kama mali ya kuokotwa na haraka kesho yake mchongo wa kuyaondoa moja baada ya jingine ukaanza kufanyika. Taarifa kutoka ndani ya kituo hicho cha Polisi zinasema magari hayo ya ‘kuokotwa’ yamekuwa yanaondolewa kituoni hapo usiku.

JAMHURI limezungumza na Kamanda wa Polisi Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Mussa Taibu, ambaye baada ya kuulizwa kuhusu kuokotwa kwa magari hayo katika Kituo cha Polisi Oysterbay, alishtuka, kisha akaomba awasiliane kwanza na wasaidizi wake.

Baada ya kufanya mawasiliano na wasaidizi wake, Kamanda Taibu ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba Tikotiko alikamatwa na magari saba tu na kwamba magari manne kati ya hayo yalikuwa si yake, hivyo yamerudishwa kwa wamiliki wake.

“Magari yaliyoletwa hapa mengine yalikuwa ya watu ambao walimpelekea kwa ajili ya kuyanunua, lakini kabla hajayanunua (kufanya malipo), yalikamatwa na kuletwa hapa. Hivyo wenyewe walikuja kituoni na kuyachukua,” amesema Kamanda Taibu.

Hata hivyo amesema suala hilo atalifuatilia na kubaini iwapo kuna udanganyifu wowote uliofanyika kuhusu uondoshwaji wa magari hayo pamoja na wahusika.

Lwitiko

Rais John Magufuli alitoa maelekezo kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, akielekeza kuvunjwa kwa mtandao wa dawa za kulevya na kuwa anataka kuiona Tanzania isiyokuwa na wauzaji na watumiaji wa ‘unga’.

Rais alinukuliwa akisema haiwezekani wauza ‘unga’ wakawa na nguvu kuliko serikali. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi ilianzisha operesheni ya kuwakamata wafanyabiashara wote wanaohusishwa na dawa za kulevya jijini Dar es Salaam.

Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni ulifanya msako mkali wa kimyakimya kwa wafanyabiashara hao na kufanikiwa kumkamata Lwitiko Samson Adam, ambaye anasemekana kuwa kati ya mapapa waliokuwa wakisakwa kwa udi na uvumba.

Lwikito ambaye alikuwa na makazi nchini Afrika Kusini, alikamatwa nyumbani kwake Magomeni jijini Dar es Salaam akiishi maisha ya ya kifahari huku vyumba alivyokuwa akivitumia kwa makazi yake vikiwa ardhini (underground).

“Huwezi kuamini, Tiko aliishi maisha ya peponi. Ukiiona nyumba yake pale Magomeni, nje si nyumba ya maana, lakini ukiingia ndani utashangaa. Nyumba imejengwa chini ya ardhi (underground), huko kuna maisha yote yanayohitajika kwa mtu mwenye ukwasi wake.

Katika makazi yake chini ya ardhi, alikuwa na bwawa kubwa la kuogelea, baa na magari yote ya kifahari yapatayo manane yaliyokuwa yameegeshwa kwenye zuria.

Magari yaliyokuwa huko chini ya ardhi ambayo yana thamani hadi Sh milioni 600 kwa gari moja, magari hayo ni pamoja na BMW X6, Lexus, Lumma CLR RS, Cooper na mengine ya kifahari.

Kuvunjwa mtandao

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, alikabidhiwa orodha ya polisi wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ambapo majina hayo aliyakabidhi kwa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Inspekta Jenerali Ernest Mangu.

Baada ya Mangu kukabidhiwa majina hayo, aliwataka askari wa Oysterbay kumkabidhi orodha ya majina ya wauza ‘unga’ haraka.

Mpango huo ulienda sambamba na kuwapangua baadhi ya polisi walioonekana kushindwa kuukabili mtandao wa wauza ‘unga’.

Maofisa waliohamishwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Kinondoni, Camillius Wambura na Mkuu wa Utawala Kinondoni, pamoja na baadhi ya askari wa kitengo cha upelelezi na wengine kutoka idara mbalimbali.

Kuhamishwa kwao kulitokana na kushindwa kwao kudhibiti mtandao wa dawa za kulevya nchini, kiasi cha kuifanya Tanzania kuwekwa kwenye orodha ya nchi zinazojihusisha na biashara hiyo kwa kiwango cha juu.

Awali, kabla ya matukio hayo, Tanzania ilikuwa ikitumiwa kama njia ya kupitishia dawa za kulevya kwenda Afrika Kusini, Ulaya na Amerika, lakini kadiri siku zinavyokwenda inakuwa soko la dawa hizo.

Aprili 12, 2017 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ilikubali maombi ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe, ya kutaka Watanzania hao washikiliwe na kusafirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka ya kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya yanayowakabili nchini humo.

Baada ya uamuzi huo, kesho yake Aprili 13, mawakili wa Shikuba na wenzake; Hudson Ndusyepo, Majura Magafu na Adinani Chitale, waliwasilisha katika mahakama hiyo nia ya kukata rufaa na tayari waliwasilisha sababu za kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania kama sheria inavyowataka endapo hawakuridhika.

Aliyekuwa wakili wao, Ndusyepo alikaririwa akisema kwamba wateja wao waliondoka nchini usiku, huku serikali ikijua kwamba kuna rufaa Mahakama Kuu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, aliposoma uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, alisema mahakama kabla ya kuamua ilijiuliza maswali kadhaa, ikiwamo kama mashtaka wanayohusishwa nayo wajibu maombi yako katika utaratibu wa kubadilisha wahalifu.

Pia mahakama ilijiuliza na kubaini kuwa kuna makubaliano ya kubadilishana wahalifu kati ya nchi hizo mbili.

Mwakyembe aliwasilisha maombi Februari 15, 2017, akiomba mahakama hiyo kuamuru Shikuba, Mfuru na Adam washikiliwe wakati wakisubiri kibali cha kuwasafirisha kwenda Marekani kujibu tuhuma za kula njama, kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya nchini humo.

Ushahidi ulionyesha kwamba Marekani iliwachunguza watuhumiwa hao miaka minne na walitumia dola 10,000 kununua dawa hizo kutoka kwa taasisi yao ili kubaini ukweli.

Uchunguzi huo uliwabaini walikuwa wakisafirisha heroin pamoja na cocaine kwa kutumia magari, na wakifikisha dawa hizo Marekani huwatumia watu kusambaza kwa kutumia ndege binafsi na Shikuba ndiye kiongozi wa taasisi hiyo.

Kakolaki alidai maombi yaliambatana na kiapo kilichotolewa na Richard Magnes ambaye anadai wajibu maombi wanatuhumiwa kuingiza dawa za kulevya zaidi ya kilo 1.78 Marekani.
Shikuba amekuwa akihusishwa na biashara kubwa ya usafirishaji wa dawa za kulevya kati ya Afrika Mashariki, Asia, Ulaya na Marekani, alikamatwa mwaka 2014 nchini, akihusishwa na shehena ya kilo 210 za heroin zilizokamatwa mkoani Lindi mwaka 2012.

Serikali ya Marekani iliamua kutaifisha mali za mfanyabiashara huyo na kupiga marufuku kampuni za nchi hiyo kujihusisha na biashara zake.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Udhibiti wa Mali za Nje cha Wizara ya Fedha ya Marekani, ilieleza kuwa Shikuba ametambuliwa kama kinara wa usafirishaji wa dawa za kulevya kwa mujibu wa sheria ya utambuzi wa vinara wa dawa za kulevya wa nje ya nchi hiyo.
Inadaiwa kuwa tangu mwaka 2006, Shikuba amekuwa akiongoza mtandao wake kutuma shehena za dawa za kulevya kwenda sehemu kadhaa duniani kama China, Ulaya na Marekani.

2016 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!