Polisi yanasa silaha ya kivita, watuhumiwa wafariki kwa kurushiana risasi na Polisi

Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao umri wao haujafahamika wamefariki wakati wakisharushiana risasi na askari Polisi waliokuwa doria wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma ambapo inadaiwa walikuwa wakienda kufanya uharifu kijiji cha Msabula Kata ya Muhuwesi wilayani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 15,2024, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Alfredi Huseini amesema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 14, mwaka huu, majira ya saa 3:30 usiku huko katika kijiji cha Msagula nje kidogo ya makao makuu ya Wilaya ya Tunduru.

Amesema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio mapema Jeshi la Polisi mkoani humo kupitia Udara ya Upelelezi wa kesi za jinai katika kuzuia na kutanzua uharifu walipata taarifa toka kwa wasiri wao kuwa huko katika kijiji cha Msagula kuwa kuna watu wawili wenye silaha wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na pikipiki aina ya TVS rangi nyeusi ambayo haina namba za usajili wakitokea Tunduru kwenda kijiji cha Msagula walikuwa wamejiandaa kwenda kufanya uhalifu wa unyang’anyi wa kutumia silaha katika maduka ya huduma za fedha kwenye kijiji hicho.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Alfred Hussein akionesha aina ya siraha iliyokuwa ikitumiwa na majambazi aina ya AK47

Kaimu Kamanda wa Polisi Alfredi Husein amefafanua kuwa baada ya Polisi kupata taarifa hiyo walianza ufuatiliaji wa haraka ambapo waliandaa mtego na baada ya watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kufika kwenye eneo lililokusudiwa kufanya uhalifu waligundua kuwa wanafuatiliwa na askari Polisi ndipo walianza kufyatua risasi hewani na askari Polisi walianza kijibizana nao na kufanikiwa kuwajeruhi kwa kuwapiga risasi maeneo mbalimbali ya miili yao na kufanikiwa kuwakamata wote wawili wakiwa na silaha moja ya kivita aina ya AK 47 ambayo imefutwa namba za usajili ambayo ilikuwa na risasi 14 ndani ya magazine pamoja na simu mbili aina ya ITEL viswaswadu.

Ameeleza zaidi kuwa jitihada za kuwakimbiza majeruhi hao kwenda Hospitali ya Wilaya ya Tunduru kwa matibabu zilifanyika na kwa bahati mbaya inadaiwa kuwa walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu na kwamba miili ya marehemu hao ambao hawakutambulika majina yao na mahali wanakoishi imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhiwa maiti Hospitali ya Tunduru.

Kamanda Huseini amesema kuwa Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya uhalifu na ametoa rai kwa wananchi wote wa Mkoa wa Ruvuma kuendelea kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu ili waweze kushugulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Alfred Hussein akiwaonesha waandishi wa habari hawapo pichani aina ya usafiri wa pikipiki waliyokuwa wakitumia majambazi Wilayani Tunduru.