LLowassaeo bado siku 75 kabla ya Tanzania kufanya Uchaguzi Mkuu Oktoba 25. Muda unaweza kuonekana mwingi, lakini ni mchache. Matukio yanayoendelea katika ulingo wa siasa, uvumi na taarifa zinazosafiri kama moto wa nyasi kavu, yanatupasa kuwa makini na kuchambua pumba na mchele. 

Wiki iliyopita nimepata mshangao wa mwaka, na leo huo ndiyo utakaokuwa msingi wa makala hii.

Wiki mbili zilizopita nilihudhuria mikutano miwili. Mkutano wa kwanza ulikuwa wa waandishi wa habari na viongozi wa UKAWA pale makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), ulioitishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, na Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi.

Wenyeviti hawa katika tamko lililosomwa na Mbatia kwa niaba yao walimkaribisha UKAWA Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa. Waandishi tuliuliza maswali na moja ya maswali hayo lilijibiwa na Profesa Lipumba juu ya sura ya Lowassa katika upinzani ikirejewa kauli zao dhidi yake alipokuwa CCM kuhusiana na Richmond.

Prof. Lipumba alisema: “Lowassa ametoka serikalini mwaka 2008, tangu ametoka ufisadi umezidi kuwa mwingi kuliko hata wakati akiwa Waziri Mkuu. Lowassa amesema mwenyewe kuwa ikiwa kuna mtu ana ushahidi dhidi yake ampeleke mahakamani, na hadi hivi tunavyozungumza hawajampeleka mahakamani. Kwa hiyo, tunasema tatizo la rushwa ndani ya CCM si la mtu mmoja mmoja, bali tatizo ni mfumo. Sisi tunaamini Lowassa hana hatia hadi atakapotiwa hatiani na Mahakama.”

Siku tatu baadaye, Lipumba akahudhuria mkutano wa kumpokea Lowassa katika Hotel ya Bahari Beach, Dar es Salaam. Akakaa naye meza moja, akampongeza kwa uamuzi wa kujiunga na Chadema. Siku mbili baada ya mkutano huo, zikaanza kuvuma taarifa kuwa Lipumba anafanya vikao na watu wasiofahamika ndani ya CUF, huku akiashiria kuanza kuvuta miguu katika UKAWA.

Baada ya hapo, Uhuru, gazeti la Chama Cha Mapinduzi (CCM), likachapisha habari za uchunguzi wa kina likaijulisha jamii kuwa Prof. Lipumba atajiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya CUF. Mara ukaitishwa mkutano na waandishi wa habari, baadaye ukasitishwa na siku iliyofuata Lipumba akaambatana na watu waliovaa suti za Kaunda kwenda kutangaza kujiuzulu uenyekiti katika Hoteli ya Peacock!

Sitanii, nasema kweli kabisa kwamba binafsi nimesema na hapa narudia, kama nchi hii ina nia ya dhati kabisa ya kuleta maendeleo ya kweli, basi inapaswa kuwa na mfumo wa kisiasa unaoruhusu mawazo nje ya chama tawala. Mfumo huu utakuwa na nguvu kama vyama vya upinzani katika uchaguzi ujao vitakizuia chama tawala kushinda viti vingi kwa kiwango cha kufanya uamuzi kinachoutaka bila kuhitaji kura za wapinzani.

Si hilo tu, siombei itokee katika dunia hii leo kuwa upinzani upate ushindi wa kimbunga kwa kuwaondoa CCM madarakani kwa kupata wabunge wengi kwa uwiano sawa na walionao CCM kwa sasa, na CCM wakapata wabunge wachache kama ulivyo upinzani kwa sasa. Ikitokea hivyo, hakuna mabadiliko yoyote tutakayoyashuhudia zaidi ya tambo za kisiasa.

Kinachohitajika ni chama tawala kupata wabunge chini ya theluthi mbili au upinzani kupata wabunge chini ya theluthi mbili kwa maana kwamba kila hoja ikitaka kupitishwa bungeni zipigwe kura, na kura zikipigwa ushindi upatikane kwa maslahi ya Taifa. Ni kwa msingi huo, mipango ya maendeleo iliyojazwa kwenye makabrasha inaweza kutekelezwa kwa kina.

Sitanii, leo ni ukweli ulio wazi kuwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imejenga barabara za lami za kutosha. Hata hivyo, fedha zilizowekezwa kwenye barabara kama nusu yake zingewekezwa kwenye treni za umeme, ungekuwa uwekezaji wenye manufaa ya hali ya juu. Kama tungejenga reli ya umeme kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, Kigoma na Arusha, nchi hii ingepata faida kubwa.

Mizigo na makontena vingekuwa vinasafirishwa ndani ya saa 6 kutoka Dar hadi Kigoma na hivyo gharama za usafirishaji zingeshuka kwa kiwango kikubwa na mizigo ya kimataifa inayopitia hapa nchini (transit) ingeongezeka kwa kiasi kikubwa. Mwisho wa siku, uamuzi huu ungetuepusha na adha ya malori yanayobomoa barabara na kusababisha ajali. Niachane na hilo nirejee kwa Prof. Lipumba.

Siku moja baada ya Prof. Lipumba kujiuzulu, alipanda ndege na kwenda Ulaya. Lipo gazeti lililoandika kuwa ‘anaenda kula bata’. Wapo watu waliopo karibu na mke wake, wanasema gazeti hilo limemuonea kwani ameondoka kwenda kwenye matibabu. Nikiwaza kisheria, hapa yanakuja mambo mawili kichwani mwangu – mens rea na actus reus.

Haya ni maneno ya Kilatini. Mens rea, hii kisheria unapotokea uhalifu kama wizi au mauaji, ni lazima kuchunguza au kupima afya ya akili. Kwamba utimamu wa akili na fikra za mhusika wakati anatenda uhalifu fulani alikuwa anawaza nini. Uchunguzi unahusisha mambo gani aliyasema muda mfupi kabla tendo alilolitenda, alikuwa na akili timamu, kisha mwonekano wake kama alikuwa mchangamfu au mnyonge.

Si hayo tu, mhusika anachunguzwa mazingira yaliyokuwa yanamzunguka. Iwapo alikuwa mgonjwa, alipata shinikizo, maisha yake yalikuwa hatarini, alikuwa na msongo wa mawazo, iwapo alishawishiwa na kwa nini alishawishika, nia yake au njama, mwenendo wa maisha yake ndani ya miezi sita au mwaka mmoja, iwapo alikuwa na mikwaruzano, haki yake iliporwa, alipata kuwa na kesi au msigishano na anayehusika kabla ya alichokitenda na maswali mengine mengi.

Linapokuja suala la actus reus; hiki ni kitendo alichofanya mhusika baada ya kuchekecha akili yake kwa kina na kujiridhisha kuwa alikuwa katika mazingira fulani. Kama ni mauaji, hapa ndipo wanaposema mhusika aliua kwa kutumia nini. Kama ni panga, bunduki, alimpiga mtu ngumi, alimnyonga kwa kamba, alimpa sumu na mengine mengi ambayo yanahusishwa na muda kilipofanyika kitendo, kwamba kwa mfano kama ni sumu ilimchukua muda gani kuikoroga na kumtegeshea aliyemuua.

Sitanii, nikihamisha maswali hayo kwenye kifo cha kisiasa cha Prof. Lipumba, bado ninayo maswali mengi. Kwamba Prof. Lipumba baada ya kujiuzulu akasafiri nje ya nchi, kwamba Prof. Lipumba alipokutana na waandishi wa habari kutangaza kujiuzulu kwake hakuwa na wanachama wa CUF wanaofahamika?

Kwamba Prof. Lipumba alipokutana na waandishi wa habari akatangaza kujiuzulu kwake hakusema hata neno iwapo anaumwa na atasafiri nje ya nchi! kwamba kwa muda mrefu, Watanzania hawakusikia Prof. Lipumba aliumwa na kukimbizwa nje ya nchi kwa matibabu! kwamba Prof. Lipumba hakuondoka na wasaidizi kama mkewe na wengine kwenda kumsaidia katika kipindi cha matibabu!

Kwamba Prof. Lipumba hakusema iwapo alizuiwa kutoa tangazo la kujiuzulu kwake kwa kutumia ofisi za CUF! kwamba Prof. Lipumba hakuwajulisha Watanzania nani aliyelipia ukumbi wa Peacock alikofanyia mkutano wa kujiuzulu, kwamba Prof. Lipumba alimtetea Lowassa kuwa ni kiongozi safi; lakini leo anasema amepata msongo wa mawazo na kujiuliza kwa nini amekubali Lowassa ajiunge na UKAWA.

Kwamba Prof. Lipumba hakupata kuwaeleza Watanzania kuwa huwa ana tatizo katika ubongo wake ‘huwa zinahama kidogo’, hivyo wakati anamkaribisha Lowassa UKAWA na kumtetea mbele ya waandishi wa habari huenda zilikuwa zimehama kidogo! kwamba profesa huyu ndiyo sasa amebaini kuwa Lowassa alikuwa anatetea Katiba Inayopendekezwa hivyo kwa kumpitisha UKAWA, Katiba haitapatikana!

Kwamba profesa huyu hakupata kufikiri kuwa huenda Watanzania watahoji safari yake ya ‘matibabu’ siku moja baada ya kujiuzulu na hivyo angewaeleza nani analipia gharama za safari na matibabu kuepusha mikanganyiko katika jamii. Wapo wanaojiuliza profesa huyu aliyekuwa jemedari wa kupigania ‘ukombozi’ amepata wapi ujasiri wa kukimbia kikosi saa ya mapambano ya kweli?

Sitanii, sina uhakika kama Profesa Lipumba anao ujasiri wa kuruhusu Watanzania kukagua akaunti zake za benki na simu za mkono au madebe na mapipa nyumbani kwake kujiridhisha iwapo uamuzi huu haujatunisha pato lake. Kwa vyovyote iwavyo, mimi siwezi kumwita msaliti, ila wapo wanaoweza kushindwa kutenganisha alichokifanya na usaliti kwa wenzake.

Ni kwa mantiki hiyo, narudia, katika uchaguzi wa mwaka huu tunapaswa kuwa na vipaumbele ambavyo vinahusisha maendeleo ya jamii kama afya, barabara, treni ya umeme, shule, umeme, sayansi na teknolojia, demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari, haki ya kupata habari na mengine mengi ya aina hii, badala ya mchezo huu wa akina Lipumba kujiuzulu siku 80 kabla ya Uchaguzi Mkuu na kutengeneza habari za umbea wakiacha matatizo ya kweli ya Watanzania kama ununuzi wa meli katika maziwa ya Victoria na Nyasa na mengine mengi ya aina hiyo. 

 

Prof. Lipumba awaeleze Watanzania ukweli wote.

1778 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!