Chama cha Ushirika mkoani Pwani kimesema kinatarajia kuboresha ukulima wa zao hilo kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ndege zisizo na rubani (drones) kupulizia mikorosho yote dawa ya Sulphur ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, akizindua kampeni ya upandaji wa miche mipya ya mikorosho mkoani humo mwaka juzi.

Akiongea na JAMHURI, Mwenyekiti wa chama hicho, Rajabu Ng’onoma, amesema utaratibu huo wa teknolojia ya kisasa utaanza katika Mkoa wa Pwani na utasaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuinua hali za wakulima.

Sambamba na hilo, ameongeza kusema kuwa wana mkakati wa kuwapatia wakulima miche mipya ya mikorosho ili kuongeza kasi ya kupanuka kwa kilimo hicho ili kuinua uzalishaji.

Amedai kwa sasa wanatarajia kuboresha uzalishaji wa zao hilo kwa njia ya kisasa, kwani serikali imeahidi kuwapa mamlaka ya kushughulika na wakulima hao kwa kila kitu, ili kuondoa migogoro iliyokuwepo hapo awali ya vyama na baadhi ya wakulima.

Ng’onoma amesema katika msimu ujao wakulima wote watapatiwa pembejeo za kilimo kwa kupitia vyama hivyo vya msingi ili kuondoa adha ya mkulima kusubiri pembejeo hizo kwa muda mrefu na pengine hata kuzikosa kabisa kutoka kwa mawakala walioteuliwa na serikali.

Amesema kwa sasa vyama vya msingi ndivyo vitakavyoshughulika na kila kitu, kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya na mkoa na kuweka utaratibu mzuri wa kuboresha zao hilo katika mkoa mzima.

“Chini ya utaratibu huu hata ikitokea mkulima anataka kufanya ujanja wake hawezi kufanya hivyo kutokana na udhibiti wa karibu,” anafafanua.

Mbali na uboreshaji huo, chama hicho kinatarajia kuanza kujenga kiwanda cha kutengeneza magunia katika mkoa huo ili kupunguza upungufu wa zana hizo. Wakati mwingine korosho huharibika kutokana na kutokuwepo kwa magunia ya kutosha kuzihifadhi vizuri.

Amesema kiwanda hicho kitasaidia kuongeza ubora wa zao hilo, kwa sababu korosho zitahifadhiwa vizuri na kuongeza soko la ajira kwa vijana.

“Vijana kutoka miongoni mwetu ndio watapewa kipaumbele cha ajira katika kiwanda hicho,” anasema.

628 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!