Kuna haja ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, kuangalia uwezekano wa kuziba pengo lililoachwa wazi na wanachama wa unaoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) katika Bunge Maalum la Katiba.

Kwa sababu, wanachama wa Umoja huo wameendelea kusisitiza kwa nyakati tofauti kwamba hawatarejea kushiriki vikao vya bunge hilo, vitakavyorejea kuendelea kujadili upatikanaji wa Katiba mpya Agosti, mwaka huu.

Wameendelea kusisitiza hivyo licha ya Rais na wananchi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, kuwasihi warudi bungeni kushirikiana na wajumbe wengine kujadili mchakato wa Katiba mpya itakayokidhi matakwa ya Watanzania.

UKAWA, inayoongozwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, inaundwa na wanachama wa vyama vikuu vya upinzani hapa nchini — Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi. Hao ni miongoni mwa walioteuliwa na Rais Kikwete kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Pamoja na mengine, wana UKAWA wamekuwa wakitaja sababu za kususia vikao vya bunge hilo kuwa ni baada ya kuona wanadharauliwa na kukerwa na hoja za baadhi ya wajumbe wa bunge hilo, zinazotetea muundo wa serikali mbili badala ya muundo wa serikali tatu uliopendekezwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji (mstaafu) Joseph Warioba.

Kwa kuwa uamuzi wa Rais Kikwete wa kuanzisha mchakato wa Katiba mpya ulikuwa na dhamira nzuri ya kuendeleza jitihada za kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya Muungano, kuna haja ya kuziba nafasi zilizoachwa wazi na wana UKAWA ili kuepusha hali inayoweza kukwaza jitihada hizo.

Tunakumbuka kwamba Machi 21, mwaka huu wakati akizindua Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, Rais Kikwete aliwaasa wajumbe wa bunge hilo kuepuka kuingiza misukumo na tofauti zao za kisiasa wakati wa kujadili rasimu ya Katiba hiyo kwa manufaa ya umma.

Hata hivyo, katika hali ambayo haikutarajiwa, baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka vyama hivyo vya siasa waliibuka na kutangaza Umoja huo na baadaye kuamua kususia vikao vya bunge hilo siku chache baadaye.

Katika hotuba yake kwa Taifa kupitia hafla ya kilele cha matembezi ya wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Rais Kikwete hakusita kuwakosoa waliosusia vikao vya Bunge Maalum la Katiba, akisema hawawatendei haki wananchi waliowachagua, yeye mwenyewe na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, waliowateua.

“Ndugu zangu, lazima nikiri kwamba sikufurahishwa hata kidogo kusikia kwamba baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba [wanaounda UKAWA] wamesusia vikao vya bunge hilo… huko walikokwenda siko…”

Wiki iliyopita, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alikaririwa na vyombo vya habari akitaka wana UKAWA wasibembelezwe kurejea kushirikiana na wajumbe wengine wa bunge hilo kujadili rasimu ya Katiba mpya.

Kitendo cha wajumbe hao kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba kimelaaniwa na wananchi mbalimbali wakisema ni cha usaliti, matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma.

Ndiyo maana kwa kuzingatia umuhimu wa Katiba mpya inayosubiriwa na Watanzania kwa shauku kubwa, FALSAFA HAI inamshauri Rais Kikwete kuangalia uwezekano wa kutengua uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba waliojitangazia UKAWA ili ateue wengine watakaoziba nafasi hizo kwa maslahi ya umma.

Suala la kuziba nafasi hizo halina budi kuzingatiwa ili kukamilisha idadi ya wajumbe iliyokusudiwa kisheria, kujadili upatikanaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kama alivyosema Nape, hakuna sababu ya kuendelea kuwabembeleza hao walioamua kukimbia uwanja wa mapambano, kwa kisingizio kwamba washindani wao wanatumia silaha kali. Hao ni watu wasiojua kwamba huwezi kushinda vita kwa kukimbia uwanja wa mapambano.

Ninaamini kwamba Rais Kikwete ana mamlaka ya kushirikiana na wasaidizi wake kuziba nafasi hizo kwa kuteua wajumbe wengine watakaowawakilisha vema wananchi katika mchakato huo wa Katiba mpya.

 

1015 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!