Wiki iliyopita katika makala hii nimezungumzia umuhimu wa kuwa na wafanyabiashara. Nimeeleza wafanyabiashara walivyo na fursa ya kutumia miundombinu inayojengwa kama reli kwa kusafirisha mizigo ya biashara, ndege kuwahi vikao na barabara kwa malori kusafirisha mizigo kila siku tofauti na wafanyakazi wanaosafiri mara moja kwa mwaka.

Sitanii, katika muda wa miaka 8 niliyokuwa mwekezaji nimebaini mambo kadhaa. Nimebaini kuwa wapo wafanyabiashara na biashara nyingi hapa nchini, wanaofanya biashara bila kufahamu misingi ya kisheria ya jinsi ya kufanya biashara.

Kwa mfano katika eneo la Banana, Dar es Salaam, nimekutaka na kijana anayeendesha kioski, ambaye ana nia ya dhati kukata leseni ya biashara, lakini amekwamishwa kwa maelezo kuwa eneo analofanyia biashara amepewa na mtu tu, hana mkataba wa pango. Kijana huyu amebaki kuendesha biashara bila leseni, hivyo hata kidogo ambacho serikali ingekipata kinapotea.

Kijana mwingine baada ya kusoma makala yangu wiki iliyopita akanipigia simu. Akasema yeye kwa wiki anauza mbuzi 8. Kila mbuzi anamuuza Sh 70,000 au chini ya hapo. Kwa maana hiyo, akawa anataka akate leseni na kufanya biashara bila usumbufu.

Kijana huyu nilimuunganisha na mmoja wa viongozi wakuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini alipokwenda Tegeta TRA akaambiwa wanaangalia mzunguko wa fedha anazopata kwa mwaka (turnover). Wakapiga hesabu ya 70,000 x 8 x 52 akaambiwa pato lake ni Sh 29,912,000 kwa mwaka.

Kijana huyu alinipigia simu akisema mtaji wake ni Sh 1,000,000. Fedha walizomwambia akalipe kama kodi kwa mwaka zinazidi mtaji wake wote. Anasema yeye ananunua mbuzi na kuuza, ambapo anapata faida ya Sh 5,000 mpaka 7,000 kwa kila mbuzi. Sasa akahoji hayo makadirio yakoje?

Sitanii, nimejaribu kuingilia huo mzozo. Kigogo wa TRA akaniambia kinachoangaliwa ni turnover na si mtaji alionao. Kimsingi, nikasema hapa ndipo tunapoulia biashara. Hii turnover inapaswa kuangaliwa juu yake ina faida kiasi gani. Huyu kijana anaposema kupata Sh 7,000 kwa kila mbuzi, hajahesabu chakula cha mchana wala maji ya kunywa anapokwenda na kutoka mnadani.

Sasa mifano ya vijana hawa wawili ni mingi hapa nchini. Ukienda TRA ukasema unataka kuanza biashara, ofisa anayekusikiliza kumbe anatumia mazungumzo yako kukukadiria kodi. Nadhani sasa TRA iongezewe nguvu. Iwe na Kitengo cha Kuanzisha na Kukuza Biashara.

Kitengo hiki kitasaidia watu wenye nia ya kuanzisha au kufanya biashara kufahamishwa taratibu na sheria za kufanya biashara. Lakini pia kitengo hiki kiwe na kazi ya kutembelea maeneo anayotaka kufanya biashara mhusika na kumpa ushauri, kufahamu mtaji wake, kuijua biashara yake na kumshauri aina ya kodi zinazopaswa kulipwa kabla hajaanza.

Sitanii, nawafahamu wafanyabiashara wakubwa wenye matatizo makubwa ya kufahamu ni kodi ipi inalipwa na ipi haistahiki. Wakati mwingine hata wanaolipa kodi, wanajikuta hawajui kuwa kuna jukumu la kujaza fomu kadha wa kadha kuthibitisha ulipaji wao wa kodi.

Zipo kampuni nyingi ambazo zinalipa vizuri sana kodi kama SDL na PAYE, lakini hazijui kuwa zinao wajibu wa kupeleka ‘monthly au annual return’, kwa maana ya kila mwezi au kila baada ya miezi sita. Zipo kampuni tangu zimesajiliwa hazijawahi kupeleka ‘annual return’ Brela au kulipia hisa walizopeana siku wanaanzisha kampuni.

Sitanii, nimeyaeleza yote haya kujenga hoja kuwa Rais John Magufuli na Dk. Philip Mpango kauli yenu isiishie katika kupiga marufuku kufunga biashara pekee. Marufuku yenu hii, ijiongeze kidogo na kuwataka TRA kushiriki kujenga biashara. Wasitoze kodi kwa kuvizia, bali kiwepo kitengo cha kuwajengea uwezo walipa kodi watarajiwa. Nchi inaendelea pale tu wafanyabiashara wanapolipa kodi.

Tukianza kufundisha watu taratibu na sheria za kufungua biashara, taratibu za kulipa kodi, mihula ya kulipa kodi na tukawawekea viwango rafiki vya kulipa kodi, nchi hii itapata kodi nyingi. Wale waliopewa vitambulisho vya umachinga watakua na kuona ni heshima kulipa kodi. Nahitimisha kwa kusisitiza kuwa Kitengo cha Kuanzisha na Kukuza Biashara kwa TRA ni muhimu sasa kuliko wakati wowote.

Please follow and like us:
Pin Share