MagufuliiJe, tangu Uhuru hadi mwaka jana wakati wengi wetu tukidai mabadiliko ya sheria, taratibu na kanuni; havikuwapo? Iwapo sheria tena na Katiba ambayo kimsingi ni sheria kuu vipo; iweje Watanzania tudai mabadiliko?

Inawezekana waliomtangulia rais wa sasa hawakuvuruga hayo yote; na kama hivyo ndivyo iweje tumekuwa tunalalamika kuwa mambo hayaendi vizuri, mafisadi wamezidi, na wauza “unga” kuwa tishio kwa uhai wa taifa letu wakati huduma za kijamii zikizorota mno?

Kwa mtazamo wangu, iwapo inaoneka Rais wetu kwa hatua anazozichukua anavuruga sheria, kanuni na taratibu na pia kulazimisha mambo (dikteta), ni bora kufanya hivyo kwa faida ya wengi kuliko kuona sheria zipo tena kwa miaka mingi tu, lakini hazinufaishi walio wengi.

Baadhi ya wafanyabiashara wanaokwepa kodi wakati sheria zipo na hazifanyi kazi si bora zivujwe, lakini wanaotakiwa kulipa kodi walipe kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa serikali katika kutoa huduma za kijamii kwa wananchi wake?

Wanaodai sheria zinavurugwa na kusema Rais ni dikteta yeye mwenyewe (Rais) amejibu kwa kusema “mimi ni mpole” pia ana akili timamu, lakini inafika mahali anafumba macho na kusema: “Lazima nifanye, na kazi hiyo ni ngumu sana kwa kuwa yanayofanyika ndani ya serikali ni ya ajabu sana. Ndiyo maana unaweza kufika mahali ukaona ugumu wa kuongoza nchi ambayo iliingiliwa na wadudu wa kila aina.” (Gazeti Mwananchi toleo namba 5670 Ijumaa Februari 5, 2016 uk.4.

Tunalilia kufuata sheria, kanuni na taratibu wakati tukijua kuwa kwa hali tuliyokuwa nayo kuwapo na sheria ni jambo moja, lakini utekelezaji wake umekuwa kitendawili.

Ndiyo maana kelele zimekuwa nyingi na baadhi yetu tukisema “tunaporwa rasilimali zetu; nchi inauzwa; wageni wananufaika zaidi kuliko wenyeji (wazawa); ufisadi umezidi, wizi wa mali za umma kushamiri; rushwa kuongezeka; na kadhalika. Unapotaka kujenga barabara nzuri lazima uvuruge iliyopo au utifue na kuichimbua ardhi na pengine kuharibu maliasili itakayokuwapo hapo unapotaka kupitisha barabara.

Ujenzi ukimalizika ‘tutatesa’ sasa tuna barabara nzuri, lakini tujiulize imetokana na nini? Kuna usemi: “Usione vinaelea, vimeundwa” kwa maneno mengine vimefanyiwa kazi tena kazi ngumu. Hiyo ndiyo kazi anayoifanya Rais wa Awamu ya Tano.

Kama ‘amevuga sheria’ anafanya hivyo kwa misingi ya kutaka sheria zitekelezwe kwa faida ya wengi. Iwapo amevuruga taratibu, vilevile kama ameingiza udikteta na kulazimisha mambo na wakati huo huo mapato ya Serikali yakaongezeka au huduma za kijamii zikaimarika, si bora mara mia kuliko kuwa kinyume chake? Kusema kweli Rais anachokifanya ni kutekeleza sheria inavyotakiwa na katika dhamira ya “Hapa Kazi Tu”.

Watanzania tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kumpata Rais huyu ambaye anaonyesha dhamira ya kweli ya kutaka kuinua hali za maisha kwa Watanzania wengi maskini. Hata kama kuna baadhi yetu hawaoni kama kuna kitu kizuri anachokifanya kusema ni “yale yale hakuna mabadiliko”; ukweli unabaki pale pale kwamba “mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni”.

Tukubali kuwa kwa muda mfupi sana ameonyesha kuwa anaweza na kama ni kuvurunga sheria, taratibu na kanuni hayo ni mapito ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuleta mabadiliko yaliyokusudiwa.

Kuubadilisha mfumo wa kiutawala ambao umekuwapo kwa muda mrefu si kazi ndogo. Ni kubwa na ngumu sana. Kwa hali hiyo tuwe na subira na wenye matumaini ya kuiona Tanzania mpya kwa muda mfupi ujao. Kadhalika tumwombe sana Mwenyezi Mungu amtie nguvu na amjaze hekima na busara hata hayo ambayo baadhi yetu wanayalalamikia; kwa kipindi cha mwaka mmoja waweze kuona kuwa kweli tunaye Rais anayefaa kuliongoza taifa letu.

Siku zilizopita, kama sikosei, marehemu Christopher Mtikila, aliwahi kusema “Saa ya Ukombozi ni Sasa”. Nami nakubaliana na usemi kama huo kwamba wakati wa mabadiliko ndani ya Tanzania ni sasa kupitia kwa Dk. John Magufuli. Iwapo baadhi yetu hatupendi kuona kunakuwapo mabadiliko ya kweli nchini Tanzania kupitia serikali iliyopo madarakani, ni vizuri tukasubiri maana miaka mitano siyo kipindi kirefu sana.

Kusema kuwa “nchi haiendeshwi kibabe au kwa amri”; na kadhalika ni masuala ya kawaida lakini kwa kuwa “nyumba yetu inavamiwa na watu kwa kupitia madirishani (wenyeji na wageni) wakati milango ya nyumba iko wazi” ukiwa mwenye nyumba huwezi kukaa kimya. Lazima uchukue hatua kurekebisha hali hiyo.

Itakubidi ukemee na kuhakikisha tabia hiyo mbaya inakwisha haraka iwezekanavyo. Haiwezekani ukabaki unashangilia unapoona watu wanakurupushana madirishani eti waingie ndani na wakishaingia wafanye wanayotaka. Kwa hali hiyo lazima mwenye nyumba uamrishe na kukemea kwa nguvu zote, vinginevyo unatiwa “mfukoni”.

Tabia kama hizo zinajitokeza kutokana na kumomonyoka kwa maadili na baadhi yetu kuwa na ubinafsi ulioshamiri kuliko kuwapo hali ya utaifa na uzalendo kwa nchi letu.

Tusimkatishe tamaa Rais wetu, bali turudi kwenye uhalisia na tumuunge mkono ili wote kwa pamoja tuweze kuyafaidi matunda yatokanayo ra rasilimali tulizonazo.

Kwa kuwa wengi tumeishachoshwa na vitendo vya kifisadi, rushwa, wizi, ubadhilifu wa mali za umma, kero nyingi katika huduma za kijamii; basi tuungane na Rais Magufuli katika vita hii ngumu ili kwa pamoja tupate ushindi. Kama ambavyo yamkini tumekuwa tukisema kwamba haiwezekani Tanzania iwe maskini wakati imesheheni mbuga za wanyamapori kuliko mataifa mengine duniani; pia tunayo rasilimali misitu kwa wingi (zaidi ya hekta milioni 35); kuna ukanda wa pwani kwenye Bahari ya Hindi kwa takribani kilomita 800; tunamiliki mlima mrefu kuliko yote barani Afrika (Kilimanjaro); ipo Hifadhi nzuri ya Ngorongoro (moja ya maajabu ya dunia); zipo Bandari (Dar es Salaam; Lindi, Mtwara na Tanga) zenye uwezo wa kufanya biashara nzuri na nchi jirani.

Vilevile, kuna fursa za kuweka bandari Bagamoyo, Kilwa na Lindi  pia ipo mito na maziwa na ukanda wa kilomita 200 katika Bahari ya Hindi ambao pamoja na mito na maziwa, kuna rasilimali samaki. Pamoja na kuwapo rasilimali zote hizo, bado tunalia na hali ya umaskini wa kipato, lakini pia masuala ya ujinga na maradhi bado vinasumbua jamii kwa kiasi kikubwa.

Hali hiyo ilijitokeza kwa sababu uwazi na ukweli kuhusu matumizi ya rasilimali zetu umekuwa siyo wa kuridhisha, hivyo kusababisha usimamizi kwa “shamba letu” kuwa dhaifu.

Kimsingi tunaangalia suala zima la maslahi mapana ya taifa letu na watu wake. Kinachotakiwa hapa ni kuona dhana hii inajengeka zaidi ndani ya fikra za viongozi wetu. Wanaochaguliwa kuliongoza taifa letu waelewe fika kuwa wanawekwa kwenye nafasi watakazozipata kwa ajili ya maslahi ya wananchi na si kuona kama ni fursa kwao kujinufaisha zaidi kwa kukumbatia maovu kama ufisadi na rushwa.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kutuasa kwamba ili taifa liweze kuwa na maendeleo endelevu tunatakiwa a tuwe na vitu vine- ardhi (ambayo tunayo); watu (ambao wapo); siasa safi na uongozi bora.

  

>>ITAENDELEA….

Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician Kilahama, ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Mstaafu katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

By Jamhuri