Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeongeza bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu hadi kufikia shilingi bilioni 45 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kutoka shilingi bilioni 35 mwaka wa fedha 2025/2026, sawa na ongezeko la takriban asilimia 29.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 21 Oktoba 2026, katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Sita kwa miaka ya 2024, 2025 na 2026, iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Zanzibar.

Amesema ongezeko hilo ni dhamira ya Serikali kupanua fursa za elimu ya juu kwa wanafunzi wenye sifa na kupunguza vikwazo vya kifedha vinavyoweza kuwazuia kuendelea na masomo.

Dkt. Mwinyi amesema Serikali itatoa ufadhili wa shahada ya kwanza kwa wanafunzi 143 waliofanya vizuri katika Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Sita mwaka huu kupitia Mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ Scholarship).

Amesema kwa mwaka 2026, wanafunzi waliopata Daraja la Kwanza kwa pointi 3 hadi 5 watapatiwa ufadhili wa Serikali, kwa kutambua juhudi na ufaulu wao, kuwaondolea mzigo wa gharama za elimu ya juu na kuwapa nafasi ya kuendelea na masomo bila kuathiriwa na changamoto za kifedha.

Rais Dkt. Mwinyi amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha changamoto za kiuchumi haziwazuii vijana wenye uwezo kutimiza ndoto zao za kielimu. Ameyataka mashirika ya fedha, makampuni na wadau wengine wa maendeleo kuongeza mchango wao katika elimu, hususan kwa kuwasaidia wanafunzi wenye uwezo mkubwa kitaaluma wanaotoka katika mazingira yenye changamoto.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuweka mkakati mahsusi wa kukabiliana na changamoto ya wanafunzi wanaopata Daraja Sifuri na Daraja la Nne, kwa kufanya uchambuzi wa kina wa matokeo, kubaini sababu za kufanya vibaya na kuimarisha ufundishaji wa masomo yenye changamoto.

Aidha, amewapongeza walimu kwa mchango wao katika kuimarisha ufaulu wa wanafunzi na kuwataka kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uzalendo na kujituma. Amewataka pia wazazi na walezi kuongeza usimamizi wa watoto wao, kuwajengea utamaduni wa kusoma na kusimamia nidhamu.

Rais Dkt. Mwinyi amesema mafanikio ya wanafunzi yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, walimu, wazazi na walezi katika kujenga mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia na kuhakikisha kila mtoto anapata elimu yenye ubora.

Akiwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri, Rais Dkt. Mwinyi amewataka kuendeleza juhudi zao, akieleza kuwa mafanikio waliyoyapata yawe chachu ya kujituma zaidi na kufikia malengo makubwa katika hatua zinazofuata za elimu.

Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Leila Mohd Mussa, amesema Wizara imeweka mikakati ya kuimarisha ubora wa elimu, ikiwemo kupunguza na hatimaye kutokomeza idadi ya wanafunzi wanaopata Daraja Sifuri katika mitihani ya Kidato cha Nne na Sita, sambamba na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata Daraja la Kwanza.