Rais William Ruto amesema kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ni hasara kubwa kwake binafsi, akimtaja marehemu kiongozi wa upinzani kama mtu muhimu katika maisha ya kisiasa na kitaifa ya Kenya.
Akizungumza wakati wa hafla ya mazishi ya Raila katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST) eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya, Rais Ruto alikiri kwamba wengi wamegusia jinsi hasara hiyo inavyomuathiri kisiasa, lakini akasema uchungu anaohisi ni wa kibinafsi.
“Wachambuzi wengi kwenye magazeti na vyombo vya habari wanasema hili ni pigo kubwa kwangu.
Ndiyo, ni pigo kubwa sana,” Ruto alisema. Matamshi ya Rais yalionyesha heshima na mshikamano wa kisiasa uliokuwa umestawi kati ya viongozi hao wawili katika miezi ya hivi karibuni, kufuatia miaka mingi ya uhasama.
