Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Sh milioni 50 kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Maria Mtakatifu Mwana wa Mungu Kibwigwa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma ambapo kiasi cha Sh milioni 250.2 kilichangwa katika harambee hiyo.
Akitangaza matokeo ya harambee hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli (TRC), Masanja Kadogoda ambaye mgeni rasmi alichangia Sh milioni 20. Alisema Rais Samia kwa mapenzi mema amechangia ujenzi huo baada ya kuombwa kufanya hivyo na askofu wa jimbo la Kigoma Mhashamu Askofu Mlola.
Kadogosa alisema kuwa katika harambee hiyo Rais Samia pia aliungwa mkono na Mwenyekiti wa kampuni ya GSM, Gharib Mohamed huku wapenzi wa timu za Simba na Yanga waumini wa kanisa hilo wakichangia kiasi cha Sh 890,000 ambapo wapenzi wa Yanga walichangia Sh 528,000 na wapenzi wa Simba Sh 362,000.

Awali Askofu wa jimbo Katoliki la Kigoma, Mhashamu Joseph Mlola alimshukuru Rais Samia kwa mchango huo na kuongeza kuwa ni kiongozi anayejali watu kwa hali yeyote sambamba na kuwashukuru wote waliofaanikisha harambee hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa kanisa hilo Katibu wa Kamati ya ujenzi, Joseph Kahene alisema kuwa kanisa hilo lilianzishwa 1933 ambapo hata hivyo hakukuwa na idadi kubwa ya waumini kama sasa ambapo kwa sasa kanisa hilo lina waumini 14,000 hivyo kufanya kanisa linalotumika sasa kuwa dogo na lililozeeka hivyo kunahitajika ujenzi wa kanisa jipya.
Kahene alisema kuwa malengo ya mradi huo wa kanisa jipya unahitajika kiasi cha Sh bilioni 4 ili kuwezesha kanisa kukamilika likiwa na uwezo wa kuchukua waumini 1800 kwa wakati mmoja hivyo michango kutoka kwa watu mbalimbali inahitajika kufanikisha mradi huo.

