Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amehimiza ushiriki wa taasisi za umma, sekta binafsi, pamoja na watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) katika kufanikisha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Toleo la 2024, kwa kuihusisha katika mipango yao ya maendeleo, diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kimataifa.
Rais Dkt. Samia ametoa rai hiyo leo katika hafla ya uzinduzi wa Sera hiyo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa maboresho ya Sera iliyozinduliwa yamechagizwa na mabadiliko makubwa ndani na nje ya nchi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, yaliyolazimu mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001.
Rais Dkt. Samia amesema Sera hiyo ya Mambo ya Nje ambayo ni mwendelezo wa Sera za ndani ya nchi ni nyenzo muhimu ya kuiwezesha Tanzania kushiriki kwa ufanisi katika siasa, uchumi na majukwaa ya kimataifa, huku ikilinda maslahi ya Taifa na kusimamia misingi ya uhuru, usawa, ujirani mwema na ushirikiano wa Afrika na dunia kwa ujumla.
Baadhi ya maeneo yaliyoboreshwa kwenye Toleo la 2024 ni kuimarisha diplomasia ya uchumi, kushirikisha Watanzania waishio nje, kuongeza ushawishi wa Tanzania duniani na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto mpya.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Sera iliyozinduliwa inatokana na mjadala mpana wa kitaifa uliohusisha wananchi na wadau mbalimbali na inatoa dira ya taifa kuhusu masuala ya nje katika mazingira mapya ya dunia yenye ushindani mkubwa wa rasilimali, teknolojia, ushawishi na usalama.
Kwa kuzingatia hayo, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania haiwezi kuendelea kutumia mbinu za zamani katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi, na kuwa Sera iliyoboreshwa itaiwezesha nchi kujipanga kwa maarifa mapya na mikakati Madhubuti zaidi.
Vilevile, Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa Sera hiyo inalenga kukuza diplomasia ya uchumi kwa kuvutia mitaji mikubwa na ushiriki wa sekta binafsi ndani na nje ya nchi, sambamba na kuitangaza Tanzania kupitia utajiri wake wa utamaduni, mila na lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya ushawishi wa kitaifa.
Aidha, Rais Dkt Samia amebainishwa kuwa kwa mara ya kwanza misingi ya Sera ya Mambo ya Nje imeongezwa kutoka saba hadi nane kwa kuingizwa msingi mpya wa kulinda na kuendeleza maadili, mila na utamaduni wa Mtanzania ikiwemo kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili, jambo linaloonesha dhamira ya kulinda utambulisho wa Taifa katika dunia yenye mabadiliko ya kijamii na kiutamaduni.