Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka dhidi ya watu wanaotumia mitandao na teknolojia vibaya. Aidha, amekemea vikali wingi wa wanaharakati kutoka nje ya nchi wanaojaribu kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania na kuhatarisha amani.
Akizungumza leo Mei 19, 2025, wakati wa uzinduzi wa Sera mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la Mwaka 2024), Rais Dkt. Samia amesema kuwa sera hiyo sasa ina misingi minane badala ya saba. Mabadiliko hayo yamelenga kuvutia uwekezaji mkubwa wa mitaji ili kuchochea biashara na kukuza hadhi ya taifa kimataifa kwa kutumia vizuri rasilimali za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.
Ameonya dhidi ya watu kutoka nje ya nchi wanaokuja kuvuruga amani na utulivu wa Tanzania, akisisitiza kuwa:
“Tusiwe shamba la bibi, mtu hawezi kuja Tanzania na kusema analotaka bila mipaka. Tumeshuhudia wanaharakati wakianza kuvamia na kuingilia mambo yetu. Wameshavuruga kwao, tusikubali watuharibie hapa kwetu.”
Rais Dkt. Samia pia amesema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakimsema vibaya, akisisitiza kuwa:
“Ninalolifanya ni kulinda nchi yangu, hatutatoa nafasi kwa yeyote kutoka nje au wa ndani kuja kutuvuruga.”
Amezitaka wizara husika kutoa ufafanuzi wa mara kwa mara kuhusu taarifa mbalimbali zinazotolewa na wanaharakati na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa endapo kuna ukweli wowote unaohusu sekta zao.