Timu ya taifa ya Ujerumani imetoa onyo kali kwa wapinzani wao kwenye Kombe la Dunia baada ya kuanza kampeni yao kwa ushindi mnono wa 7–1 dhidi ya Curacao katika mchezo wa ufunguzi.

Licha ya kuanza kwa kusuasua na kuruhusu bao la kusawazisha, vijana wa Julian Nagelsmann walionyesha ubora wao kwa kuongeza kasi na kutawala mchezo ipasavyo.

Ujerumani walikwenda mapumzikoni wakiwa mbele 3–1, na waliporejea kipindi cha pili waliongeza ari na nidhamu ya juu, huku wakifunga mabao manne zaidi na kuonyesha kiwango kinachotarajiwa kutoka kwa timu inayolenga kutwaa taji lao la tano la Kombe la dunia.

Kocha Nagelsmann alisifu kikosi chake kwa utulivu na ubunifu wao, ingawa alisisitiza kuwa kasi na umakini ulioonekana kipindi cha pili ndicho kiwango wanachopaswa kukidumisha ili kufika mbali kwenye mashindano hayo.

Ujerumani sasa wanaelekeza nguvu kwa mchezo wao ujao dhidi ya Ivory Coast, utakaopigwa Toronto siku ya Jumamosi. Ushindi mwingine utawaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya mtoano.