Na Mwandishi wetu, Mirerani
WACHIMBAJI wa madini nchini wametakiwa kuwalipia wafanyakazi wao asilimia 0.5 ya mishahara yao ili kuwachangia kwenye mfuko wa fidia kwa wafanyakazi utakaowanufaisha pindi wakipata madhila kupitia mafao saba.
Mwakilishi wa Meneja mkuu wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) Naanjela Msangi ameeleza hayo akizungumza na viongozi wa wachimbaji madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Msangi ameeleza kuwa endapo wamiliki wa migodi wakiwalipia wafanyakazi wao asilimia 0.5 ya mishahara yao kila mwezi watanufaika na mambo mengi ikiwemo kujikinga na kuzuia vihatarishi vya ajali.
Amesema endapo wafanyakazi wakichangiwa watanufaika kwa kulipwa fidia katika sekta rasmi wanaopata ajali, ugonjwa ama kufariki dunia.
“Katika kuteketeza jukumu hili WCF inatoa jumla ya mafao saba ambayo ni huduma ya matibabu, malipo ya ulemavu wa muda na wa kudumu na malipo kwa anayemhudumia mgonjwa,” amesema Msangi.
Ametaja mafao mengine ni huduma za utengemao, msaada wa mazishi na malipo kwa wategemezi endapo mfanyakazi atafariki.
Amesema pamoja na mambo mengine muhimu WCF tuna wajibu wa kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu njia bora za kujilinda au kuepukana na vihatarishi vya ajali au magonjwa yanayotokana na kazi.
“Kumbukeni mwajiri anatakiwa kulipia asilimia 0.5 TU ya mshahara kwa kila mfanyakazi wake na mkitekeleza jukumu hiki la kisheria mnakuwa mmechangia kwa kiasi kikubwa kulinda nguvu kazi ya Taifa,” amesema Msangi.
Amesema pamoja mambo mengine mpango huo unazitaka taasisi za umma kupanga mpango katika bajeti zao kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu na kutoa taarifa juu ya utekelezaji wake.
“Ndiyo maana WCF tukaona tutumie sehemu ya bajeti yetu ya kurejesha kwa jamii (CSR) kutoa msaada wa barakoa ili kusaidia kupunguza magonjwa, ajali au vifo vinavyotokana na kazi katika eneo hili la migodi ya madini ya Tanzanite,” amesema.
Makamu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini wanawake Tanzania (TAWOMA) Rachel Njau amesema mfuko huo utakuwa ukombozi kwa wachimbaji madini nchini.
Njau amesema viongozi wa WCF wanatakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji katika ngazi mbalimbali wakiwemo wamiliki wa migodi, mameneja na wachimbaji wenyewe ili wafahamu faida za mfuko huo.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Tariq James amesema mpango huo ni mzuri japokuwa wachimbaji wa Tanzanite hawalipani mshahara ila wanalipana asilimia 10 baada ya kupata madini.
“Hata kama hawalipani mshahara ila wamiliki wanaweza kupiga hesabu ya kima cha chini cha mshahara Sh500,000 wanalipa asilimia 0.5 ni Sh2,500 kila mwezi ili kuwachangia,” amesema Tariq.
Mmoja kati ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite, Zephania Joseph amesema mpango huo ni mzuri kwa wachimbaji hivyo unapaswa kupokewa kwa mikono miwili.




