Katika kuendeleza diplomasia ya utamaduni na kuthamini kahawa kama urithi wa pamoja, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuimarisha urafiki, maelewano na ushirikiano wa kudumu kati ya wananchi wa Tanzania na Jamhuri ya Korea, hatua inayolenga kufungua fursa zaidi za kiuchumi, utalii na biashara kati ya mataifa hayo mawili.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Tamasha la Kahawa la Gongneung Forest Trail 2026 nchini Korea Kusini, Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea, Mheshimiwa Noel Kaganda, amesema kuwa tamasha hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kupitia kahawa yake bora pamoja na urithi wake wa kiutamaduni.
Mheshimiwa Kaganda alieleza kuwa Tanzania huzalisha takribani tani 100,000 za kahawa kila mwaka, huku sekta hiyo ikisaidia maelfu ya wakulima na kuchangia kati ya dola za Marekani milioni 200 hadi 300 katika uchumi wa taifa.
Aidha, alisisitiza kuwa kahawa si zao la biashara pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuimarisha uchumi, kujenga urafiki kati ya mataifa na kukuza ubadilishanaji wa tamaduni huku akiongeza kuwa kupitia zao hilo, Tanzania na Korea zinaendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.
Mbali na kuitangaza kahawa ya Tanzania, Balozi Kaganda aliwaalika washiriki wa tamasha hilo pamoja na wageni wengine kutoka Korea Kusini kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na visiwa vya Zanzibar, ambavyo vinatambulika duniani kwa uzuri wake wa kipekee na vivutio vya asili.
Alibainisha kuwa kupitia diplomasia ya utamaduni na matumizi ya kahawa kama daraja la kuunganisha watu, Tanzania inaendelea kujenga mahusiano imara ya urafiki, maelewano na ushirikiano wa muda mrefu na Jamhuri ya Korea, huku ikifungua milango ya fursa mpya za uwekezaji, biashara na utalii kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.






