Naibu Msajili wa Hazina, Lightness Mauki, amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa uwekezaji wa umma ili kuhakikisha rasilimali zilizowekezwa katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni zenye hisa za Serikali zinaendelea kuleta tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Bi. Mauki amesema hayo leo Juni 15, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Morocco Square jijini Dar es Salaam, ambapo alitangaza rasmi kufanyika kwa Siku ya Gawio 2026 itakayofanyika Juni 30, 2026 katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Alisema mgeni rasmi katika hafla hiyo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye atapokea gawio na michango mbalimbali kutoka taasisi za umma pamoja na kampuni ambazo Serikali imewekeza.

“Tunawashukuru sana waandishi wa habari kwa kuendelea kuitikia mwito wetu na kuonesha thamani yenu kama wadau muhimu wa uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa uwekezaji wa Serikali.

Kupitia kazi yenu mnasaidia wananchi kufahamu kile kinachoendelea katika uwekezaji wa Serikali,” amesema Bi. Mauki.
Amesema kaulimbiu ya Siku ya Gawio 2026 ni “Uwekezaji wa Umma wenye Matokeo: Nguzo ya Uchumi Shindani na Maendeleo Endelevu kuelekea Dira ya Taifa 2050”, akieleza kuwa inalenga kuhamasisha ufanisi, tija na uwajibikaji katika usimamizi wa mali za umma.

Kwa mujibu wa Bi. Mauki, uwekezaji wa Serikali katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni zenye hisa za Serikali umefikia takribani shilingi trilioni 95, hatua inayodhihirisha umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

Alisema Siku ya Gawio ni jukwaa muhimu la kuonesha matokeo ya uwekezaji wa Serikali, kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya mali za umma pamoja na kuthibitisha mchango wa taasisi za umma katika kukuza uchumi wa taifa.

Aidha, Bi. Mauki aliwapongeza viongozi wa taasisi na mashirika ambayo tayari yamewasilisha gawio na michango yao serikalini, huku akizihimiza taasisi ambazo bado hazijakamilisha zoezi hilo kuhakikisha zinawasilisha kwa wakati kabla ya Juni 30, 2026.

Bi. Mauki amesema taasisi zitakazoonesha utendaji bora na kutoa gawio kubwa zaidi zitatambuliwa na kutunukiwa tuzo maalum na Rais Samia Suluhu Hassan, hatua inayolenga kuhamasisha ushindani chanya, uwajibikaji na utamaduni wa utendaji unaozingatia matokeo.

Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kufuatilia kwa karibu taarifa za uwekezaji wa umma ili kuelewa namna rasilimali za taifa zinavyosimamiwa na matokeo yake katika sekta mbalimbali muhimu zikiwemo afya, elimu, nishati na miundombinu.

Akihitimisha, Bi. Mauki aliwataka Watanzania kujitokeza kufuatilia Siku ya Gawio 2026, akisema tukio hilo ni fursa muhimu ya kuona namna uwekezaji wa Serikali unavyoendelea kuchangia maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi.