Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Kaliua

RAIS wa Awamu ya Sita Dk Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha ukosefu wa shule ya msingi kwa wakazi wa Kijiji cha Magele kata ya Usimba Wilayani Kaliua kwa kuamua kuwapelekea zaidi ya sh mil 360 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo mpya ya kisasa.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wakazi wa Kijiji hicho wamemshukuru Rais Samia kwa kuokoa maisha ya watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa kutembea umbali mrefu kufuata shule ya karibu iliyopo wilaya jirani ya Urambo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho Issa Katabhi amesema tangu waanze kuishi kijijini hapo miaka 35 iliyopita hawajawahi kuwa na shule ya msingi hali iliyopelekea watoto wao kutembea umbali wa zaidi ya 20 kwenda na kurudi shule jirani.

Amebainisha kuwa watoto wao wakiwemo wenye mahitaji maalumu walikuwa wanapata òshida sana hali iliyopelekea baadhi yao kuamua kuacha shule huku wengine wakiongopa kuwa wanaenda shule kumbe wanaishia njiani kutokana na uchovu hivyo kushindwa kuendelea na masomo.

‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kusikia kilio chetu na kuamua kutujengea shule mpya yenye ubora wa hali ya juu sana,’ amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Jerry Mwaga, Kaimu Afisa Elimu wa msingi John Moto amesema shule hiyo ni mkombozi kwa kuwa itasaidia kupunguza mlundikano wa watoto wanaosoma katika shule mama ya Usimba ambayo ina watoto zaidi ya 1300 na iko umbali mrefu sana kutoka kijijini hapo.

Amebainisha kuwa ujio wa shule hiyo na shule mpya ya sekondari ya kata hiyo iliyogharimu zaidi ya sh mil 600 ambazo zinatarajiwa kuanza mwezi Januari 2024 ni fursa muhimu kwa wakazi wa Kijiji hicho kwani watoto wao wakiwemo wenye ulemavu watapata fursa ya kupata elimu karibu na nyumbani.

Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Rashid Chuachua amefafanua kuwa ujenzi wa shule hizo unatokana na azma ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka watoto wote wakiwemo wenye ulemavu kupata elimu ili kuongeza idadi ya wataalamu katika sekta mbalimbali.

Amemshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kusikia kilio cha wakazi wa Kijiji hicho na kuwajengea shule ya viwango yenye miundombinu yote.

By Jamhuri