Na Abdala Sifi WMJJWM – Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt Samia Hassan Suluhu ametoa zawadi kwa Watoto wanaolelewa katika makao mbalimbali nchini kwa lengo la kuwapa faraja na upendo msimu huu wa sikukuu.
Zawadi hizo zimetolewa na Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Mussa Mkamate kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. John Jingu.
Akikabidhi zawadi hizo Kamishna Mkamate amesema zawadi hizo zimetolewa na Rais kwa lengo la kuwapa faraja na upendo watoto na kusherehekea kwa furaha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa matunzo ya Watoto Rais Samia ametoa zawadi hizo katika vituo vya vinavyotoa huduma ya malezi ya Watoto ambavyo ni Kijiji cha Matumaini pamoja na Kituo cha KISEDET vilivyopo Mkoani Dodoma .
“Napenda kukabidhi zawadi hizi zikiwemo mchele, maharage, sukari vinywaji pamoja na mbuzi ambazo zimetolewa na Mheshimiwa Rais, kwa lengo la kuwatakia heri watoto hawa na kusherekea vyema mwaka mpya”amesema Mkamate.
Aidha ameongeza kwamba jamii inapaswa kuwalea na kuwatunza watoto kwa kuwapa mahitaji yao ya msingi, kudumishi amani na upendo katika familia ili kuepusha migogoro ambayo ndiyo imekuwa miongoni mwa sababu za kutelekeza watoto.
Naye Msimamizi wa Kituo cha Kijiji cha Matumaini Vicent Bosseli amemshukuru Rais Samia kupitia Wizara pamoja na Ofisi ya Mkuu Mkoa wa Dodoma kwa kutoa zawadi hizo kwa ajili ya watoto kwani zitaleta faraja katika kusheherekea Sikukuu ya Mwaka mpya kwa watoto hao.



